Andrew Msechu Na Leonard Mang’oa – Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amemwomba Rais Dk. John Magufuli kukutana na vyama vya siasa pamoja na wadau wa siasa nchini, ili kubadilishana mawazo kuhusu mambo muhimu yanayoweza kufanyika ikiwamo kuboresha Tume ya Uchaguzi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuboresha na kusimamia uchaguzi ulio huru na haki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema ombi hilo ni sehemu ya kumsaidia Rais kutokana na ahadi yake aliyoitoa mbele ya mabalozi hivi karibuni, kuwa atahakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unakuwa huru na wa haki.
“Kwenye mkutano wake na mabalozi angeweza kuwaeleza kuwa Tanzania ni nchi huru na hawana haki ya kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania. Badala yake akatamka kuwa uchaguzi wa Oktoba 2020 utakuwa huru, wa haki na amani.
“CUF, chama cha wananchi kimefarijika na kauli hiyo ya Rais na kwamba uchaguzi huru na wa haki utasaidia kuendeleza amani na utulivu nchini.
“Tunaamini Rais hayuko tayari kuiingiza nchi kwenye machafuko yatokanayo na uchaguzi usio huru na wa haki. Kwa kuzingatia ukweli kwamba Rais ametuhakikishia hilo mbele ya wanadiplomasia, tunawajibika kuamini maneno yake,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema mambo muhimu yanayotakiwa kujadiliwa na kuandaliwa ili kuwa na mazingira mazuri ya uchaguzi huru na wa haki, ni kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani ili kutoa fursa kwa vyama vyote kufikisha sera na itikadi zao kwa wananchi katika kutafuta kuungwa mkono.
Profesa Lipumba alisema sheria ya vyama vya siasa inahitaji vyama vyote viwe na rejista ya wanachama na viongozi katika ngazi zote za chama.
“Utekelezaji wake unahitaji uhamasishaji kupata wanachama na uhakiki wa wanachama katika ngazi zote, hivyo kunahitajika kuwapo uhuru wa vyama kufanya mikutano ya hadhara, hivyo ni muhimu kuitekeleza sheria hiyo sura ya 258,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema pamoja na pendekezo kwa mkuu wa nchi kukutana na wadau wote wa siasa, ni muhimu kwa Watanzania kutambua kuwa mchakato wa kudai na kujenga demokrasia utafanikiwa kwa kushiriki katika siasa, hata kama mazingira ni magumu.
Kutokana na hali hiyo, tayari Baraza Kuu la Uongozi la chama chake limeshaamua kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu watasimamisha wagombea katika ngazi zote kuanzia urais, ubunge na udiwani katika maeneo yote ya uchaguzi Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu suala la muungano wa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo, Profesa Lipumba alisema kwa sasa wanajenga chama na kuandaa wagombea, lakini suala la ushirikiano ni jema na kwamba watakuwa tayari kushirikiana na wale wenye nia ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani na si vinginevyo.