28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Warioba azungumzia mchakato wa Katiba

Asha Bani -Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema yanayotokea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa si kitu kipya, na kwamba hakuna chama ambacho hakina vuguvugu kama ilivyo kwa chama hicho.

Jaji Warioba aliyasema hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha Konani kinachorushwa na Televisheni ya ITV ambapo alitakiwa kutoa maoni yake kutokana na yanayoendelea ndani ya CCM ya kuwahoji wanachama wake.

Kamati ya Maadili ya chama mwishoni mwa wiki iliwaita wanachama wake watatu kuwahoji ambao ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bernard Membe na waliokuwa makatibu wakuu wa chama hicho, Yusuf  Makamba na Abdulrahman Kinana.

Jaji Warioba alisema si kitu kipya kwa chama hicho kwa kilichotokea na kwamba hakuna chama ambacho hakina vuguvugu.

“Sio kitu kipya kwa CCM, hakuna chama ambacho hakitakuwa na vuguvugu na CCM imekuwa na hiyo kwa wakati wote tangu hata wakati wa Tanu, kwamba mnakuwa na majadiliano, mnazungumza na viongozi, hata huko nyuma walifanya hivyo na viongozi walipata kufukuzwa.

“Kwa hiyo sio kitu kipya na katika chama chochote kile sio tu CCM na mikusanyiko mingi inakuwa na hayo, kwa hiyo ni mambo ya kawaida, sio kitu cha kutisha,” alieleza Jaji Warioba.

Akizungumzia hali ya siasa nchini, alisema Tanzania ina bahati na ni nchi ya umoja na mshikamano, pia yenye amani na utulivu kwa hali hiyo Tanzania ni nzuri.

“Kwa sasa nchi inahangaika na maendeleo na sio sisi tu, ni dunia nzima wanahangaika na maendeleo ya nchi zao, Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika maendeleo,” alisema Jaji Warioba.

KUHUSU KATIBA

Jaji Warioba pia alizungumzia suala la katiba akisema ya kwanza ilikuwa mwaka 1961 mara baada ya uhuru ambayo ilikuwa ya Muingereza kwani ni kawaida akiwapa uhuru lazima atunge katiba.

Alisema kuna katiba ilitakiwa itungwe mwaka 1966, lakini haikutungwa hadi mwaka 1977.

“Katiba ya mwaka 1977 ilikuwa ni shinikizo la Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere ambapo alitaka iwe ni mwisho wa kugombea, lakini alitoa hotuba na kuzungumza mengi ikiwa ni pamoja na kusema kuwa nchi ni ya chama kimoja, na kama ni ya chama kimoja ni vizuri kufikiria na kuwa na chama kimoja.

“Pia ni lazima kuendeleza demokrasia, wakati huo eneo la uongozi wa chini kulikuwa na utaratibu wa kubadilishana viongozi, lakini eneo la juu huku hawakutaka kumbadilisha, kila zikipigwa kura alikuwa anatakiwa kuchaguliwa yeye tu,” alisema Jaji Warioba.

Alisema aliona ni muhimu kung’atuka, lakini 1976 waliamua kuunganisha vyama vya Afro Shiraz Party na Tanu huku mwaka 1977 mwezi kama huu ndio kikazaliwa Chama Cha Mapinduzi.

“Baada ya kuunganishwa vyama ikaonekana wakati umefika wa kutengeneza katiba mpya na mwezi Machi mwaka 1977 ikapelekwa mapendekezo mapya na ndio katiba inayotumika mpaka sasa,” alisema Jaji Warioba.

Alisema katiba ilianza kuunganisha muungano, Shaban Mloo alikuja Bara kufanya kazi ndani ya CCM na Benjamin Mkapa alikwenda Zanzibar kufanya kazi.

Jaji Warioba alisema vita ya Uganda pia ilirudisha nyuma kupitia mapendekezo ya pili ya Katiba mwaka 1979, hivyo haikujadiliwa.

Alisema Nyerere mwaka 1980 aligoma tena kugombea, ingawa watu wake walimlazimisha.

Jaji Warioba alisema mwaka 1980 aliendelea kuomba kubaki kutokana na hali ya nchi kuwa mbaya kwa wakati huo kutokana na kutoka kwenye vita, alitakiwa pia kubaki katika nafasi hiyo ili watengeneze utaratibu wa kuchagua kiongozi katika ngazi hiyo ya juu.

“Hata hivyo aliagiza afanyiwe utafiti kuhusu taratibu za kukabidhiana madaraka duniani inakuwaje, tulifanya utafiti ule na kumpelekea, lakini akawa kimya mpaka Septemba mwaka 1980 wakati mkutano mkuu unafanyika kumteua mgombea wakamteua tena kuwa rais.

“Baba Nyerere alikubali, lakini alizungumzia suala la uchumi na pia alisema ni vizuri kuwepo na utaratibu wa kupokezana uongozi na pia kuwepo vipindi vya uongozi wa urais kwa vipindi viwili,” alisema Jaji Warioba.

Alisema pia alipochaguliwa alisisitiza kudumisha muungano zaidi, lakini alisisitiza suala la kugawa madaraka kwa kuwa alisema endapo akifanya kazi yeye atakuwa dikteta.

Historia yake kwa ufupi

Jaji Warioba alisema alipokuwa mwanafunzi aliingia katika siasa katika uongozi wa shule katika vyama vya wanafunzi, kisha alipomaliza shule alifanikiwa kuwa mtumishi wa umma na kuachana na mambo ya siasa.

Alijiunga na ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa kufanya kazi kisheria na kisha kupanda vyeo hadi kuwa mwanasheria mkuu.

“Kwa kuwa mwanasheria mkuu ndicho kilichonifanya kuingia kwenye siasa tena, nikawa Waziri wa Sheria na kisha kuwa Waziri Mkuu hivi ndivyo nilivyoingia katika siasa,” alisema Jaji Warioba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles