Francis Godwin – Iringa
MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha maafa makubwa mkoani Iringa ambako vimeshuhudiwa vifo vya watu watano katika Tarafa ya Idodi na Isimani.
Pamoja na vifo hivyo miundombinu ya barabara ya kwenda Hifadhi ya taifa ya Ruaha imekatika.
Miongoni mwa watu waliopoteza wapendwa wao ni Hadija Nungwa ambaye licha ya kuokoa watoto wake wawili, wengine wawili aliwapoteza baada ya kusombwa na maji.
Hadija ambaye kwa sasa amelazwa Kituo cha Afya Idodi akisimulia mkasa huo baada ya kutembelewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa waliofika kumpa pole na kutoa msaada kwa wahanga wa mafuriko hayo alisema; akiwa ndani ya nyumba yake asubuhi saa 12 alisikia mlio wa vyombo vikigongana.
Alisema kitendo hicho kilimfanya amwamuru mtoto kutoka nje kuangalia kulikoni na aliporejea alimweleza kuwa maji yamezingira nyumba yao .
Alisema alilazimika kutoka nje akiwa na watoto wake wanne akijaribu kuwaokoa na wakati anavuka maji watoto wawili walimponyoka na kusombwa na maji.
Kwamba yeye na watoto wawili waliweza kunusurika baada ya kuung’ang’ania mti uliokuwepo eneo hilo .
“Baada ya kuona tumezidiwa na maji na kuna uwezekano wa kusombwa wote wale wakubwa nikawaacha sababu matumaini ya kuwaokoa yalipotea kutokana na kasi kubwa ya maji, waliwasombwa nami nikaona nife na huyu mdogo mwenye umri wa miaka 3 na huyu wa miezi 2 ambao niliwakumbatia “
Alitaja watoto waliofariki dunia kuwa ni Bosco Kayese (8 ) na Stevin Suga ( 5) huku walionusurika ni Neema Suga (3) na Salome Suga(2).
Akikabidhi msaada wa chakula na kutoa pole kwa wahanga wa mafuriko hayo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Dk. Abel Nyamahanga ambaye alikuwa amembatana na viongozi wa CCM wilaya ya Iringa vijijini na mkoa, aliwataka wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo kuendelea kuchukua tahadhari ikiwamo kuhama hasa wale wanaoishi katika maeneo hatarishi .
Aliyataja maeneo hatarishi na yaliyoathirika zaidi kuwa ni Kitisi, Mapogoro na Idodi ambako watu wanne wamefariki dunia na Tarafa ya Isimani mtu mmoja.
Alisema mbali ya kupoteza wananchi watano pia hali ya miundombinu katika Kijiji cha Tungamalenga na Kitongoji cha Darajani kuelekea katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni mbaya kutokana na kuharibika kwa daraja kubwa eneo hilo .
Akitoa taarifa ya maafa hayo Katibu Tarafa wa Idodi, Jacob Kiwanga alisema nyumba 15 zimefikiwa na mafuriko na zilizoanguka ni 171 pia mazao yote yamesombwa.
Pia alisema madaraja mbali mbali yamevunjika na kusombwa na mafuriko hayo hivyo hakuna usafiri na kufika kijiji kwa kijiji na hivyo kuwa kama kisiwa .