30 C
Dar es Salaam
Saturday, December 4, 2021

Faida hii ya mabenki, mikakati sasa iwe endelevu

Mwandishi Wetu

MOJA ya kati ya habari ambazo tunaweza kusema ni nzuri katika eneo la uchumi ni takwimu mpya kuonyesha faida kupanda kwa mabenki ya biashara nchini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo ambazo zimeashiria kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini, benki 11 kati ya 12  za kibiashara zimeripotiwa kuongeza faida kubwa.

Benki hizo ni NMB, CRDB, Standard Charterd, NBC, Stanbic, Diamond Trust Bank, TPB, KCB, Azania, Exim na Barclays (Absa) ambazo zimetengeneza  faida ya zaidi ya Sh bilioni 429 kwa mwaka unaoishia Desemba 2019 ukilinganisha na Sh bilioni zaidi ya 262 za mwaka 2018.

Benki ya kwanza inayoongoza kwa kutengeneza faida kubwa ni NMB ambayo imefika Sh bilioni 148.6 mwaka 2019 kutoka bilioni  97.7 mwaka 2018.

Benki ya CRDB inafuatia ikiwa imetengeneza faida ya Sh bilioni 122.4 kutoka bilioni 69.6, wakati Standard Charterd imeshika nafasi ya tatu ikiwa na Sh bilioni 34 kutoka Sh biioni 20.

Nafasi ya nne imeshikwa na NBC ambayo imetengeneza Sh bilioni 22.7 kutoka bilioni 10.3 na Stanbic inafuatia kwa kuwa na Sh biioni 21.3 kutoka bilioni 16.2, DTB imeongeza Sh bilioni 17.4 kutoka bilioni 15.4.

Benki ya KCB yenyewe imepanda hadi kufikia Sh bilioni 14.168 kutoka Sh bilioni 9.56 wakati kwa upande wa Azania wana bilioni 12.7 kutoka bilioni 5.9 na Exim ambao walishuhudia hasara huko nyuma nayo imepanda hadi kutengeneza faida ya bilioni 9.8 kwa mwaka 2019.

Benki ya TPB nayo faida yake imeongezeka na kufikia Sh bilioni 16.9 Barclays ikiwa na bilioni 9.6.

Hatua ya benki hizo kuongeza faida  pamoja na mambo mengine sisi tunaona ni dalili njema baada ya miaka mitatu iliyopita taasisi hizo kupita katika hali ngumu kiasi cha wakati fulani Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuamua kujitokeza hadharani na kuionya Tanzania kuhusu mzunguko wa fedha. .

Mwaka 2017 wakati huo IMF likiionya Tanzania dhidi ya sera zake za kubana matumizi likisema hatua hiyo ilikuwa inapunguza mzunguko wa fedha na kuathiri uwekezaji, ndio wakati ambao benki  nyingi zilionekana kupitia hali ngumu zaidi.

Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema) alilifikisha suala hilo bungeni na kuhoji sababu za mzunguko mdogo wa fedha katika soko.

Ndio wakati huo Serikali ilijitokeza na kutangaza kuwa ilikuwa imeanza kuchukua hatua ya kukabiliana na  tatizo la mzunguko mdogo wa fedha katika soko ikiwemo kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alikaririwa Aprili 3, 2019 bungeni mjini Dodoma akisema kuwa katika kutatua changamoto ya kupungua kwa mzunguko wa fedha katika soko, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua  mbalimbali za kuongeza ukwasi kwenye uchumi ikiwemo kushusha riba inayotumika kuzikopesha benki za biashara nchini (discount rate) kutoka asilimia 16 Machi, 2017 hadi asilimia 7, Agosti 2018.

Pengine pamoja na hatua kama hizo katika robo ya mwisho ya mwaka 2019 hali imeonekana kuwa tofauti kabisa  hasa baada ya faida kubwa kuanza kuonekana kwenye benki hizo za biashara.

Tunapotizama hayo yote  na pengine kupongeza hatua zilizochukuliwa ni vyema pia Serikali kupitia Benki Kuu ikaendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kusimamia mzunguko wa fedha unaoendana na mahitaji halisi ya uchumi kwa lengo la kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei na hivyo kuweka mazingira mazuri ya ukuaji wa uchumi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,968FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles