28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Mafuriko yaua watano Iringa

Francis Godwin – Iringa

MVUA zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha maafa makubwa mkoani Iringa ambako vimeshuhudiwa vifo vya watu watano katika Tarafa ya Idodi na Isimani.

Pamoja na vifo hivyo miundombinu ya barabara ya  kwenda Hifadhi ya taifa ya Ruaha imekatika.

Miongoni mwa watu waliopoteza wapendwa wao ni Hadija Nungwa ambaye licha ya kuokoa watoto wake wawili, wengine wawili aliwapoteza baada ya kusombwa na maji.

Hadija ambaye kwa sasa amelazwa Kituo  cha Afya Idodi akisimulia mkasa huo baada ya kutembelewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa  waliofika  kumpa pole na kutoa msaada kwa  wahanga wa mafuriko hayo  alisema; akiwa  ndani ya  nyumba yake  asubuhi  saa 12 alisikia mlio wa  vyombo vikigongana.

Alisema kitendo hicho kilimfanya amwamuru mtoto kutoka nje kuangalia kulikoni na aliporejea alimweleza kuwa maji yamezingira nyumba yao .

Alisema alilazimika kutoka nje  akiwa na watoto  wake  wanne akijaribu  kuwaokoa na wakati anavuka maji watoto  wawili   walimponyoka na  kusombwa na maji.

Kwamba yeye na watoto  wawili waliweza  kunusurika baada ya  kuung’ang’ania mti uliokuwepo  eneo hilo .

“Baada ya kuona tumezidiwa na maji na kuna uwezekano wa  kusombwa  wote wale wakubwa nikawaacha sababu matumaini ya kuwaokoa yalipotea kutokana na kasi kubwa ya maji, waliwasombwa nami nikaona nife na huyu mdogo mwenye umri wa miaka 3 na huyu wa miezi 2 ambao  niliwakumbatia “

Alitaja watoto waliofariki dunia  kuwa ni Bosco Kayese (8 ) na  Stevin Suga ( 5) huku walionusurika ni  Neema Suga (3) na  Salome Suga(2).

Akikabidhi msaada  wa  chakula na kutoa  pole kwa  wahanga wa mafuriko hayo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa, Dk.  Abel Nyamahanga  ambaye  alikuwa amembatana na viongozi wa CCM wilaya ya Iringa vijijini na mkoa, aliwataka wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo kuendelea  kuchukua tahadhari ikiwamo kuhama hasa wale wanaoishi katika maeneo hatarishi .

Aliyataja maeneo hatarishi  na yaliyoathirika zaidi  kuwa ni Kitisi, Mapogoro na Idodi ambako watu wanne wamefariki dunia na Tarafa ya  Isimani mtu  mmoja.

Alisema mbali ya kupoteza  wananchi  watano  pia hali ya miundombinu katika  Kijiji cha Tungamalenga  na  Kitongoji cha Darajani  kuelekea  katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni mbaya  kutokana  na kuharibika kwa daraja kubwa  eneo hilo .

Akitoa  taarifa ya maafa  hayo  Katibu  Tarafa wa Idodi,  Jacob Kiwanga  alisema  nyumba  15  zimefikiwa na mafuriko na  zilizoanguka ni 171 pia mazao yote yamesombwa.

Pia alisema madaraja  mbali mbali yamevunjika na kusombwa na mafuriko  hayo hivyo hakuna  usafiri na kufika  kijiji kwa  kijiji  na hivyo kuwa kama  kisiwa .

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles