WAANDISHI WETU-MWANZA
JESHI la Polisi mkoani Mwanza linadaiwa kuwachunguza askari polisi saba waliohusika katika kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa na dhahabu kilo 323.6.
Mbali ya dhahabu hiyo, watuhumiwa walikutwa na Sh milioni 305 ambazo hazikuelezwa mara moja zilikuwa zinapelekwa wapi.
Taarifa za uchunguzi zinasema hadi jana jioni polisi hao walikuwa chini ya ulinzi. Inadaiwa askari baada ya kuwakamata watuhumiwa walifanya nao majadiliano ambayo mpaka sasa hayajawekwa wazi.
Inadaiwa siku ya tukio, mpango wa mazungumzo na polisi na watuhumiwa hao ulisababisha wachelewe kupelekwa sehemu husika, baada ya mmoja wa watuhumiwa kudaiwa kwenda benki kuchukua fedha ambazo zilionekana kuvuka Sh milioni 50 kitendo ambacho kiliwafanya watumishi wa benki kutoa taarifa kwa uongozi wa mkoa na vyombo vya usalama kwa ajili ufuatiliaji zaidi.
Taarifa zilizozifikia gazeti hili kutoka nyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinadai miongoni mwa askari waliowekwa chini ya ulinzi, yumo aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo na askari wengine sita.
Askari hao wanashikiliwa kituo kikuu na wengine wako vituo vya wilaya za Ilemela na Nyamagana wakiendelea kuhojiwa.
RPC, RC warushiana mpira
Hata hivyo, MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna ili kuzungumza kinachoendelea katika ukamataji wa dhahabu hiyo, ambapo alisema suala hilo lipo mikononi mwa Mkuu wa Mkoa, John Mongela na hawezi kusema chochote mpaka apate kibali kutoka kwake.
“Suala lile lilianzia ofisi za mkoa hivyo mwenye mamlaka ya kulisemea ni mkuu wa mkoa, naomba umtafute atakupatia taarifa maana yeye ni bosi wangu hapa lakini akinipa kibali cha kuzungumza nitasema kile atakachinielekeza,”alisema.
Alipoulizwa taarifa za askari waliohusika katika ukamataji wa dhahabu hiyo kuwekwa mahabusu , alikana na kudai hakuna kitu kama hicho.
MTANZANIA kwa mara ya kwanza, lilimtafuta Mongela ambapo alisema mpaka jana watuhumiwa waliokamatwa ni watatu na hakuna aliyeongezeka, huku uchunguzi ukiendelea na kuahidi kutoa taarifa leo.
“Tangu tuwakamate watuhumiwa wale watatu hakuna aliyeongezeka, ispokuwa uchunguzi wa sakata hilo unaendelea, leo kama mkuu wa mkoa nikishirikiana na wakuu wa wilaya tunashughulika na mambo ya kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaanza masomo.
“Ila nakuahidi kwamba kesho (leo) nikipata nafasi ya kukutana na RPC Shana tutapeana mwendelezo wa uchunguzi unaoendelea, wale watuhumiwa watafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika,”alisema.
Hata hivyo baadaya taarifa kupatikana kwamba askari saba waliohusika nao wamewekwa chini ya ulinzi kwa uchunguzi zaidi, gazeti hili liliwasiliana tena na RC Mongela ili kupata uhakika lakini alidai kutokuwa na taarifa huku akihoji nani aliyetoa taarifa hizo.
Alipojibiwa kuna taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi, RC Mongela alisema ni vema kuwanukuu hao hao waliotoa taarifa, alipotajiwa miongoni mwa askari mwenye cheo cha SSP ambaye alikuwa naye siku ya tukio aliomba kupewa muda ili afuatilie na kujiridhisha.
Hata hivyo, baada ya saa mbili alipotafutwa tena Mongela, alisema hakupata nafasi ya kujiridhisha kwa sababu alikuwa na kikao ofisini kwake.
“Nimetoka kikaoni na nipo safarini kwenda kumpokea Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally anaingia mkoani kwangu kuanza ziara.
“Ndugu mwandishi, naomba niseme sijafuatilia suala hilo tangu muda ule ulivyoniambia kwa sababu nilikuwa na kikao… kikao chenyewe sijamaliza vizuri nimetoka nipo barabrani nakwenda Misungwi kumpokea Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi kwa leo (jana) sina cha kuzungumza.
Vigogo watua Mwanza
Taarifa zinasema Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boazi amewasili jijini hapa kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.
Wengine ambao walitarajia kuwasili ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulagwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dotto Biteko.
Meneja TRA
Alipotafutwa Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Ernest Dundee ili kujua kama viongozi hao wamewasili, alisema ana taarifa zisizo rasmi baadhi ya viongozi kuwepo mkoani hapa.
“Taarifa rasmi sina ya mabosi wangu kuja Mwanza, ingawa tetesi zipo ila nakuomba kesho (leo), nitafute nitakuwa na fursa ya kuzungumza kwa uwazi zaidi maana hili sakata la kukamatwa dhahabu ni kubwa, naweza kukuambia fulani hayupo kumbe yupo,kesho tutafutene utapata taarifa nzuri,”alisema Dundee.
Kukamatwa fedha
Inaelezwa mmoja wa watuhumiwa aliyekutwa na Sh milioni 305, alishindwa kutoa maelezo ya kina kwa maofisa wa benki juu ya matumizi ya fedha hizo.
Kutokana na maelezo yake kusuasua, hali iliwafanya maofisa wa benki kumtilia shaka na kuamua kutoa kutoa taarifa kwa mkuu wa mkoa.
Inadaiwa maofisa wa benki walipomhoji mteja wao sababu za kuchukua fedha nyingi bila kuwa na barua, alidai anakwenda kununulia dhahabu na walimtaka kufuata taratibu alidai ana dharura.
Hata hivyo ilielezwa kuwa kabla ya kukabidhiwa kiasi hicho chs Sh milioni 305, tayari taarifa kwa mkuu wa mkoa na vyombo vingine ilikuwa imefikishwa na ufuatiliaji ulikuwa unaendelea hadi walipokamatwa eneo la Kivuko cha Busisi wilayani Sengerema.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya tukio kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ofisa Mwandamizi wa Polisi mkoani hapa, Advera Bulimba alisema jeshi la polisi lilipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema kwamba kuna watu wana kiasi kikubwa cha madini na wanakisafirisha ndipo walipoanza kufuatilia.
Kikosi kilichokuwa kinafuatilia kiliongozwa na ofisa operesheni wa mkoa kufuatilia na kuweka mitego iliyofanikiwa kuwanasa.