27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Askari Polisi waliokamata dhahabu wachunguzwa

WAANDISHI WETU-MWANZA

JESHI la Polisi mkoani Mwanza linadaiwa kuwachunguza askari polisi saba waliohusika katika kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa na  dhahabu kilo 323.6.

Mbali ya dhahabu hiyo, watuhumiwa walikutwa na Sh milioni 305 ambazo hazikuelezwa mara moja zilikuwa zinapelekwa wapi.

Taarifa za uchunguzi zinasema hadi jana jioni polisi hao walikuwa chini ya ulinzi. Inadaiwa askari baada ya kuwakamata watuhumiwa walifanya nao majadiliano ambayo mpaka sasa hayajawekwa wazi.

Inadaiwa siku ya tukio, mpango wa mazungumzo na polisi na  watuhumiwa hao ulisababisha wachelewe kupelekwa sehemu husika, baada ya mmoja wa  watuhumiwa kudaiwa kwenda benki kuchukua fedha ambazo zilionekana kuvuka  Sh milioni 50 kitendo ambacho kiliwafanya watumishi wa benki  kutoa taarifa  kwa uongozi wa mkoa na vyombo vya usalama kwa ajili ufuatiliaji zaidi.

Taarifa zilizozifikia gazeti hili kutoka nyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, zinadai   miongoni mwa askari waliowekwa chini ya ulinzi, yumo aliyekuwa kiongozi wa operesheni hiyo na askari wengine sita.

Askari hao wanashikiliwa  kituo kikuu na wengine wako vituo vya wilaya za Ilemela na Nyamagana wakiendelea kuhojiwa.

RPC, RC warushiana mpira

Hata hivyo, MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna ili  kuzungumza   kinachoendelea katika ukamataji wa dhahabu hiyo, ambapo alisema  suala hilo lipo mikononi mwa Mkuu wa Mkoa, John Mongela na hawezi kusema chochote mpaka apate kibali kutoka kwake.

“Suala lile lilianzia ofisi za mkoa hivyo mwenye mamlaka ya kulisemea ni mkuu wa mkoa, naomba umtafute atakupatia taarifa maana yeye ni bosi wangu hapa lakini akinipa kibali cha kuzungumza nitasema kile atakachinielekeza,”alisema.

Alipoulizwa taarifa za askari waliohusika katika ukamataji wa dhahabu hiyo kuwekwa mahabusu , alikana na kudai hakuna kitu kama hicho.

MTANZANIA  kwa mara ya kwanza, lilimtafuta Mongela ambapo alisema mpaka jana  watuhumiwa waliokamatwa ni watatu na hakuna aliyeongezeka, huku uchunguzi ukiendelea na  kuahidi kutoa taarifa leo.

“Tangu  tuwakamate watuhumiwa wale watatu hakuna aliyeongezeka, ispokuwa uchunguzi wa sakata hilo unaendelea, leo kama mkuu wa mkoa nikishirikiana na wakuu wa wilaya tunashughulika na mambo ya kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaanza masomo.

“Ila nakuahidi kwamba  kesho (leo) nikipata nafasi ya kukutana na RPC Shana tutapeana mwendelezo wa uchunguzi unaoendelea, wale watuhumiwa watafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika,”alisema.

Hata hivyo  baadaya taarifa kupatikana kwamba askari saba waliohusika nao wamewekwa chini ya ulinzi kwa uchunguzi zaidi, gazeti hili liliwasiliana tena na RC  Mongela ili kupata uhakika lakini alidai kutokuwa na taarifa huku akihoji nani aliyetoa taarifa hizo.

Alipojibiwa  kuna taarifa  kutoka ndani ya jeshi la polisi, RC Mongela alisema ni vema kuwanukuu hao hao waliotoa taarifa, alipotajiwa miongoni mwa askari  mwenye cheo cha SSP  ambaye alikuwa naye siku ya tukio aliomba kupewa muda ili afuatilie na kujiridhisha.

Hata hivyo, baada ya saa mbili alipotafutwa tena Mongela, alisema hakupata nafasi ya kujiridhisha kwa sababu alikuwa na kikao ofisini kwake.

“Nimetoka kikaoni na nipo  safarini kwenda kumpokea Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally anaingia mkoani kwangu kuanza ziara.

 “Ndugu mwandishi, naomba niseme sijafuatilia suala hilo tangu muda ule ulivyoniambia kwa sababu nilikuwa na kikao… kikao chenyewe sijamaliza vizuri nimetoka nipo barabrani nakwenda Misungwi kumpokea  Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi  kwa leo (jana) sina cha kuzungumza.

Vigogo watua Mwanza

Taarifa zinasema Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boazi amewasili  jijini hapa kwa ajili ya kufuatilia suala hilo.

Wengine ambao walitarajia kuwasili ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulagwa  na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dotto Biteko.

Meneja TRA

Alipotafutwa Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza, Ernest Dundee ili kujua kama viongozi hao wamewasili, alisema ana taarifa zisizo rasmi baadhi ya viongozi kuwepo mkoani hapa.

“Taarifa rasmi sina ya  mabosi wangu  kuja Mwanza, ingawa tetesi zipo ila nakuomba kesho (leo), nitafute nitakuwa na fursa ya kuzungumza kwa uwazi zaidi maana hili sakata la kukamatwa dhahabu ni kubwa, naweza kukuambia fulani hayupo kumbe yupo,kesho tutafutene utapata taarifa nzuri,”alisema Dundee.

Kukamatwa fedha

Inaelezwa mmoja wa watuhumiwa aliyekutwa na Sh milioni 305, alishindwa kutoa  maelezo ya kina kwa maofisa wa benki juu ya matumizi ya fedha hizo.

Kutokana na maelezo yake kusuasua, hali iliwafanya maofisa wa benki kumtilia shaka na kuamua kutoa kutoa taarifa kwa mkuu wa mkoa.

Inadaiwa maofisa wa benki walipomhoji  mteja wao sababu za kuchukua fedha nyingi bila kuwa na barua, alidai anakwenda kununulia dhahabu  na walimtaka kufuata taratibu alidai ana dharura.

Hata hivyo ilielezwa kuwa kabla ya kukabidhiwa kiasi hicho chs Sh milioni 305, tayari taarifa kwa mkuu wa mkoa na vyombo vingine ilikuwa imefikishwa na ufuatiliaji ulikuwa unaendelea hadi walipokamatwa  eneo la Kivuko cha Busisi wilayani Sengerema.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya tukio kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,  Ofisa Mwandamizi wa Polisi mkoani hapa, Advera Bulimba alisema  jeshi la polisi lilipata taarifa za siri kutoka kwa raia wema kwamba kuna watu wana kiasi kikubwa cha madini na wanakisafirisha ndipo  walipoanza kufuatilia.

Kikosi kilichokuwa kinafuatilia kiliongozwa na  ofisa operesheni wa mkoa kufuatilia na kuweka mitego iliyofanikiwa kuwanasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles