24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Spika Ndugai amtisha CAG

RAMADHAN HASSAN Na ANDREW MSECHU-DODOMA/DAR

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai,  amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge kwa hiari yake ili akahojiwe vinginevyo atafikishwa mbele ya kamati hiyo kwa pingu.

Amesema Profesa Assad anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 21, mwaka huu kutokana na kauli yake inayodaiwa kuwa amelidhalilisha Bunge.

Licha ya CAG pia Spika Ndugai, amesema Mbunge wa Kawe (Chadema),  Halima Mdee naye anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Januari 22, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana,  Spika Ndugai, alisema kuwa Profesa Assad amelidhalilisha Bunge.

Alisema CAG Assad, akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili Redio ya Umoja wa Mataifa (UN), alisema Bunge la Tanzania ni dhaifu.

“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji,  huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi,  na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema kitendo hicho kimemkasirisha kwani hakutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Desemba mwaka jana Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

Katika majibu yake CAG alisema. “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge, kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“…Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika, ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa,” alisema CAG Assad

Katika majibu yake kwa swali hilo aliendelea kusema kuwa “Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua,” alisema Prof. Assad.

Hata hivyo mwaka jana lilipoibuka suala la upotevu wa Sh1.5 trilioni kwenye hesabu za Serikali mwaka wa fedha 2016-2017, Assad aliulizwa kuhusu nini kifanyike, akataka Bunge liulizwe kwani ndilo lenye kutakiwa kuibana Serikali kuhusu kutoonekana kwa fedha hizo.

Kutokana na mahojiano hayo Spika Ndugai, alisema kuwa kama CAG anasema Bunge ni dhaifu basi mpotoshaji mkubwa atakuwa CAG na wafanyakazi wake.

“Kwa hiyo sasa na kwa mujibu wa kinga madaraka na haki za Bunge kwa sheria za Tanzania. Na Kwa mujibu wa mamlaka niliyonayo kama Spika, Kifungu cha 4, kifungu kidogo cha kwanza (a) cha nyongeza ya nane ya kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari mwaka 2016.

“Suala hili nalipeleka kwenye kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge, ili waweze kulifanyia kazi. Kwa hiyo CAG Profesa Assad anapaswa kufika kwenye kamati Januria 21 mwezi huu nakazia wito huu atokee tarehe 21 na ajitokeze kwenye kamati na kuthibitisha maneno yake ya huko Marekani.

“Na mnafahamu pamoja na hatuna polisi, lakini tuna uwezo wa kumleta mtu kwa pingu kwa hiyo natumaini wito huu, atauzingatia kwa sababu nataka kumhakikishia sisi si dhaifu,” alisema Spika Ndugai.

Licha ya hilo Spika Ndugai alitoa wito maalumu kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kufika mbele ya kamati hiyo kujibu maneno aliyosema hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii akiunga mkono kauli ya Prof. Assad kwamba Bunge ni dhaifu.

“Lakini pia tunatoa wito maalum kwa Mbunge wa Kawe Halima Mdee, kufika mbele ye kamati hiyo tarehe  22, Januari kwa maneneo aliyoyasema hivi karibuni kupitia mitandao.

“Roho ya mwenendo nchi inategemea uimara wa Bunge, sasa CAG amesema Bunge ni dhaifu, ni kweli mimi kama mbunge wa vipindi vitatu nathibitisha hilo, na yeye naye badala ya kusema vichochoroni aje aseme hadharani.

“Na mkumbuke tumeshampa adhabu kadhaa kwa kushindwa kutawala mdomo na ulimi wake na namuhakikishia hatuja choka na yeye atokee kwenye kamati apate haki yake ya kusikilizwa,” alisema Spika Ndugai.

Mbali na wito huo, Spika Ndugai, alimtaka CAG ajitathimini dhidi ya kauli hiyo na kwamba Bunge liko imara na kamwe halitokubali kudharauliwa.

“Bunge tumepokea kwa masikitiko kuhusu kauli ya CAG, aliyoitoa Marekani, kauli hiyo imelenga kutoa picha kwamba ripoti zake hazifanyiwi kazi au akishazifikisha bungeni kazi inakuwa imekwisha, jambo ambalo si kweli.

“CAG na maofisa wake wanaingia kwenye Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC).

Spika alisema kuwa ripoti hizo zikifika kwenye kamati hizo ambazo zinaongozwa na upinzani, muda wote maofisa wa CAG wanakuwepo kueleza mapungufu waliyoyabaini na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, imekuwa ikipambana dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma na hatua zimekuwa zikichukuliwa.

Spika Ndugai alisema mabadiliko makubwa kwenye usimamizi wa fedha za umma yamefanyika kwa ushauri wa Bunge na CAG, hivyo alishangazwa na hatua zipi ambazo CAG alitaka zichukuliwe.

“Alitaka hatua gani zichukuliwe?. Napeleka tahadhari kwa maofisa wa serikali na wananchi kutojaribu kulidhalilisha Bunge.Tunasikitika zaidi matamko haya ya dharau kutoka kwa CAG kuliita dhaifu tena akiwa nje ya nchi.

“Ni ustaarabu kutoisema nchi yako vibaya ukiwa nje ya nchi kama vile wewe ni mkimbizi. Hata wageni wanaotutembelea hapa bungeni hawazisemi vibaya nchi zao unafikiri huko ni peponi.

“Na ieleweke sio kwamba Bunge hatuna uvumilivu wa kukosolewa tunachokikaataa hapa ni dharau. Bunge la 11 hili la sasa hivi ndio limesheheni wasomi kuliko Bunge lolote, Watanzania wamekuwa wakichagua watu wenye elimu,tukumbuke tunaposema Bunge….

“Mule ndani lipo Baraza lote la Mawaziri isipokuwa Rais, mule wapo manaibu mawaziri wapo wabunge yupo Waziri Mkuu halafu mtu mmoja anakwenda Marekani anasema  lina watu madhaifu.

“Wapo watakaosema CAG ana uhuru kikatiba, lakini kwenye katiba hakuna aliyehuru bila kuwa na uwajibikaji,” alisema Spika Ndugai

Alisema wapo watakaojitokeza kwamba Ofisi ya CAG ni huru na analindwa kiajira lakini aliwakumbusha kwamba kwenye katiba hakuna ambaye yupo huru bila kuwa na sehemu ya kuwajibika.

“Kwa mfano yeye CAG nitatumia maneno ya Kiingereza maana nimejaribu kutafuta nimepata taabu kidogo CAG  ni ‘Responsibal’ na ‘Countable’ kwa Bunge, katika nchi za wenzetu huko CAG ni mmojawapo ya sehemu ya Bunge.

“Ili apate uhuru wa kufanyakazi kama nchi yake ambavyo wameona hivyo ndio maana ripoti zake zote analeta hapa,hivi unapopeleka ripoti si ndio kwa mabosi wako,” alisema

ZITTO APINGA

Baada ya agizo hilo la Spika Ndugai, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliandika katika mtandao wa kijamii kwamba hakubaliani na hatua hiyo ya spika na kudai kwamba hana mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria.

“Wito alioutoa Spika Ndugai kwa CAG Prof Assad ni dharau kubwa kwa Taasisi za Uwajibikaji katika nchi yetu na ni dalili za kulewa madaraka. Watanzania tusikubali CAG (mlinzi wa fedha zetu) kudhalilishwa. Tunajua hizi ni mbinu za kumkatisha tamaa Prof. Assad katika utendaji wake.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania 143 (6) ikisomwa kwa muktadha wa pamoja na sheria ya ukaguzi wa umma sheria namba 14, hakuna mamlaka yoyote nchini inayoweza kumuhoji CAG ispokuwa kwa mashtaka mahakamani. Spika wa Bunge hana mamlaka ya kisheria kumwita CAG Kamati ya Maadili # Nasimama Na CAG,” aliandika Zitto Kabwe kwenye mtandao wake wa Twitter.

FATMA KARUME

Akizungumzia suala hilo Mwanasheria, Fatma Karume alisema Kanuni za Bunge zinampa mamlaka Spika kumwita mtu aliyezungumza suala linalohusu Bunge nje ya Bunge iwapo ameanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo, lakini ni kwa ajili ya kutoa tu ushahidi katika kamati.

Fatma ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), alisema kwa mujibu wa sheria inayohusu mamlaka na kinga, Bunge lina haki ya kumwita mtu yeyote kwa ajili ya kutoa ushahidi kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha sheria hiyo kinachoeleza wazi kwamba mtu yeyote atakayeitwa hatakiwi kudharau wito huo, lakini si kufanya uchunguzi kuhusu suala hilo kwa kuwa Bunge si mahakama.

“Lakini iwapo mtu akiwa nje ya Bunge, kama ni mbunge amesema maneno yanayolituhumu, kulichafua au lilidhalilisha Bunge, anaweza kuchukuliwa hatua za kijinai kwa kukamatwa, kisha kupelekwa mahakamani. Kwa suala kama hilo linapotokea nje ya Bunge hilo ni suala la jinai, lina vyombo vyake vinavyohusika,” alisema.

Kuhusu kuitwa kwa CAG, alisema Katiba ndiyo inayotoa majukumu ya CAG na kwamba inaelekeza wazi kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumtia hatiani au kumuhoji akiwa katika utekelezaji wa madaraka chini ya mamlaka anayopewa.

Alisema alichokieleza CAG Assad ni malalamiko yake kuwa Bunge halimsaidii katika shughuli zake za kuidhibiti Serikali katika mapato na matumizi yake na kwamba ieleweke kuwa kwa mujibu wa Katiba hakuna mwenye mamlaka ya kumuingilia katika utekelezaji wa majukumu yake.

MSANDO

Katika ukurasa wake wa Twitter, wakili Albert Msando aliandika: Twende taratibu Mhe. Spika taratibu kabisa. Umesema unapeleka suala hilo kwenye Kamati ya Maadili ili wakushauri na walishauri Bunge.

“Lakini hapo hapo unasema CAG aende kwenye kamati akajieleze. Asipoenda mnaweza kumtia pingu. 1. Kamati imeshakushauri wewe na Bunge kwamba CAG aitwe ajieleze? 2. Anayepaswa kufikia uamuzi na kutoa wito kumuita CAG ni wewe au kamati?

Aliendelea kuandika: “3. Unamuita CAG kwa Press Conference na kumtishia kwa pingu? 4. Marehemu babu yangu aliwahi kunionya kwamba kufanya jambo kwa haraka ni kiashiria cha udhaifu. Alichosema CAG ni kwamba kazi ya ofisi yake ikishakamilika anakabidhi Bunge lichukue hatua. Anadhani Bunge halichukui hatua kwa sababu ni dhaifu

Anaedelea: “ Unajibu kwamba siyo dhaifu kwa kumtishia pingu. Hiyo siyo kazi ya Bunge wala njia ya kuonyesha Bunge siyo dhaifu. Kwa hili ni bora uangalie upya kuhusu Mamlaka ya Bunge, Taratibu za Kumhoji CAG Kikatiba na njia bora za kiuongozi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles