28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi Muhimbili walazimika kuchangia damu

TUNU NASSOR NA MWANTUMU SAADI,
DAR ES SALAAM
KUTOKANA na uhaba wa damu ulioikumba Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wafanyakazi wa hospitali hiyo na ndugu wa wagonjwa, wamelazimika kuchangia damu kunusuru maisha ya wagonjwa .

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminieli Aligaesha, alisema wamelazimika kutumia wafanyakazi wa hospitali hiyo na ndugu wa wagonjwa kama chanzo cha ndani na kwa siku ya jana wamewezesha kuchangia chupa 62 za damu.

“Kiasi cha damu kilichopatikana kutoka kwenye chanzo cha ndani bado hakitoshelezi kutokana na mahitaji ya hospitali kwa siku kuwa chupa 70 hadi 100. Ni vema wananchi na taasisi wajitokeze kuokoa maisha ya wagonjwa,” alisema Aligaesha.

Alisema hadi jana chupa 129 za damu zilikuwa zimekusanywa kutoka vyanzo vya nje kwa benki ya damu Dodoma kuchangia chupa 50, Tumbi Red Cross chupa 30 na Hospitali ya Lugalo chupa 13.
Nyingine ni Benki ya Damu Morogoro chupa 10, Mpango wa Damu Salama Kanda ya Mashariki chupa 20 na Mpango wa Damu Salama makao makuu chupa sita.

Alisema hospitali ina wataalamu wa kutosha waliojipanga kuhakikisha hatua ya ukusanyaji damu inafanyika vema hivyo watu wajitokeze kuchangia damu kuokoa maisha ya wagonjwa.

Alisema hospitali inahudumia wagonjwa 1,200 hadi 1,500 kwa siku hali inayowalazimu kuwa na damu ya kutosha wakati wote.

Wakati huohuo, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) nayo imetangaza kukabiliwa na upungufu wa damu kutokana na kupokea wagonjwa wengi wa dharura hasa waliopatwa na ajali mbalimbali.

Akizungumza na MTANZANIA, Meneja Ustawi na Uhusiano wa taasisi hiyo, Almas Jumaa, alisema mahitaji ya damu ya taasisi hiyo ni makubwa kutokana na huduma za upasuaji zinazoendelea kutolewa.

“Kuanzia kesho (leo) tutakuwa na huduma za matibabu na upasuaji za uti wa mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu zitakazotolewa na wataalamu kutoka katika taasisi hii kwa kushirikiana na Chuo cha Tiba cha Weil Cornell kutoka Marekani hivyo tutahitaji damu ya kutosha,” alisema Jumaa.

Jana uongozi wa MNH ulitoa taarifa ya dharura kwa serikali, watu binafsi, mashirika ya umma na makampuni kusaidia kuchangia damu kuokoa maisha ya wagonjwa hospitalini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles