ILI si tatizo jipya ambalo baadhi ya vyombo vya habari nchini vimekuwa vikiligusia mara kwa mara. Kama kuna tatizo linalowakera wakazi wengi wa Wilaya ya Kilombero na sehemu nyingine nchini, hasa wakulima na wanamazingira, basi ni tabia ya wafugaji kulisha ovyo mifugo yao.
Tabia hii si kwamba inaharibu uoto wa asili na vyanzo vya maji, bali pia imejenga chuki kubwa kati ya wakulima na wafugaji hao kiasi cha mara kwa mara pande hizi mbili kujikuta zikipigana.
Wafugaji hulisha ng’ombe wao katika mashamba ya wakulima, na hivyo kuharibu mazao yao.
Aidha, uchafuzi wa maji na uharibifu wa vyanzo vya maji umesababisha upungufu mkubwa wa samaki katika Bonde la Mto Kilombero.
Tatizo la wafugaji wilayani Kilombero, na hata Kilosa mkoani Morogoro, ni la siku nyingi, na athari zake kwa jamii zinajulikana, lakini mamlaka husika zinakosa utashi wa kisiasa wa kutatua tatizo hili moja kwa moja.
Viongozi kadhaa, wakiwamo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, mawaziri wakuu wa zamani, wakuu wa Mkoa wa Morogoro kwa nyakati tofauti; na wakuu wa Wilaya ya Kilombero kwa nyakati mabalimbali pia wamekuwa wakitoa ahadi za kuwaondoa wafugaji kutoka katika maeneo nyeti ya Bonde hili, lakini ahadi hizo zimekuwa zikiishia hewani.
Jitihada za wataalamu wa ikolojia na wanamazingira kuwashawishi viongozi na mamlaka husika kutenda zimeendelea kugonga mwamba.
Kimya hiki huko nyuma kiliwahi kuisukuma Kamati Tendaji ya Baraza la Biashara la Wilaya ya Kilombero kumpatia Kikwete risala maalumu ambayo si tu ilimkumbusha kuwa ahadi yake aliyokuwa ameitoa Novemba, 2008 haikutekelezwa, bali pia iliweka bayana hali ya kutisha ya uharibifu wa mazingira ambao bado unaendelea katika wilaya hiyo ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na ufugaji holela.
Kwamba sensa ya mifugo iliyofanywa na Idara ya Mifugo mwaka 2010 katika vijiji 23 ilibaini kuwapo kwa jumla ya ng’ombe 38,451 wakati eneo la malisho lilikuwa hekta 120,000 tu!
Kwa kuliona tatizo hili, Serikali huko nyuma ilifanya jitihada mbalimbali kutatua tatizo hili, likiwamo agizo la Kikwete ambalo halikutekelezwa!
Tunadhani huu ulikuwa ni utani, tena utani mbaya kwa sababu historia inaonyesha kuwa kulikuwa na mito 78 iliyokuwa inatiririsha maji kwa msimu wote wa mwaka katika Bonde la Mto Rufiji, lakini sasa mito inayotiririsha maji kwa msimu wote ni chini ya 25.
Hali hii inahatarisha uhai na uwepo wa Bonde la Mto Kilombero na uhai wa Bonde la Mto Rufiji ambalo theluthi mbili ya maji yake hutoka katika Bonde la Mto Kilombero.
Tunathubutu kusema kuwa wakati wa kuliokoa Bonde la Mto Kilombero ni sasa, vingivevyo tusahau mafanikio ya sera ya Kilimo Kwanza ya Serikali, kwani Bonde hili hutoa asilimia 30 ya mpunga nchini, ukiachia mbali ya vyanzo vya maji ambavyo huchangia maji ya kuzaliha umeme huko Mtera na Kidatu.
Tunasema Awamu ya Tano ithubutu na itatue tatizo hili lililoshindikana kwa muda mrefu.