33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ASKARI ATOA USHAHIDI KESI YA MALKIA WA MENO YA TEMBO

Na MANENO SELANYIKA

DAR ES SALAAM

ASKARI kutoka Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kitengo cha Kupambana na Ujangili, Sajenti Beatus, ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyochukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa Manase Philemon kwa kujihusisha na ujangili na biashara ya meno ya tembo na kuyathibitisha kwa kutia saini yake.

Manase, mwenzake raia wa China anayejulikana kwa jina la Malkia wa Meno ya Tembo, Yang Feng Glan (66) na Salvius Matembo wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya nyara za Serikali yenye thamani ya Sh bilioni 13 iliyotokea kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi, kutoa ushahidi jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, Beatus, alidai kuwa Aprili 20, 2014 katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama alichukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa Manase.

Alidai kuwa kabla ya kuchukua maelezo hayo alimpa haki Manase kwa  kujitambulisha mbele yake, kumfahamisha tuhuma zinazomkabili na kumpa haki ya kuwa na ndugu jamaa ama rafiki wakati akichukuliwa maelezo yake ya onyo.

Alidai kuwa maelezo hayo anayoyatoa yanaweza kutumika mahakamani kama kielelezo cha ushahidi na kwamba Manase alimwambia amefahamu haki alizopewa na yupo tayari kutoa maelezo yake akiwa peke yake.

Akiendelea kutoa ushahidi, Beatus, alidai kuwa alichukua maelezo ya onyo ya Manase kati ya saa 10:05 jioni na saa 11:28 jioni na kwamba baada ya kumaliza mshtakiwa huyo alipewa ayasome na akathibitisha kuwa yapo sawa, akasaini na kuweka dole gumba na akaomba ayatoe mahakamani hapo kama sehemu ya kielelezo cha ushahidi.

Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya, alipinga akiomba mahakama isiyapokee maelezo hayo ya onyo ya Manase aliyoyatoa polisi kwa sababu yalichukuliwa nje ya muda na alipigwa na kunyanyaswa.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Shahidi, aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na Machi 14 hadi 15, mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ili kuthibitisha kama maelezo hayo ya onyo yalichukuliwa nje ya muda na mshtakiwa alipigwa na kunyanyaswa ama la.

Washtakiwa wanatetewa na Wakili Masumbuko Lamwai, Jeremiah Mtobesya na Hassan Kihangio.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014  walijihusisha na biashara  ya nyara za Serikali. Katika kipindi hicho washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889 yenye thamani ya Sh bilioni  5.6 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles