28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

ALI KIBA KURUDISHIWA TUZO ALIYOSTAHILI TUMEJIFUNZA NINI?

NA CHRISTOPHER MSEKENA

NOVEMBA mwaka jana ni mwezi ambao hauwezi kusahaulika katika historia ya muziki wa Bongo Fleva kupenya kimataifa. Hii ndiyo ile siku ambayo uongozi wa tuzo za MTV EURO ulitangaza kutoa kimakosa tuzo katika kipengele cha Msanii Bora Afrika.

Usiku wa utolewaji wa tuzo hizo ndani ya mji wa Rotterdam nchini Holland katika kipengele hicho, alipewa staa wa muziki kutoka Nigeria ingawa kwenye vikokotoo vya kura mpaka dakika za mwisho msanii, Ali Kiba alikuwa anaongoza kwa kura nyingi kuliko msanii yeyote.

Kelele za mashabiki wa Tanzania kwenye mitandao ya kijamii ziliushtua uongozi wa tuzo hizo kwamba kuna kosa limefanyika na baada ya kujiridhisha wakakiri kufanya kosa na wakatangaza kuirudisha tuzo hiyo ambayo tayari ilikuwa mikononi mwa Wizkid.

Matukio kama haya ni adimu mno kutokea  kwenye ulimwengu wa burudani. Inawezekana yapo na yanatokea mara nyingi ila huwa yanafanywa siri kufuatia mwenendo wa upigaji kura huwa hayawekwi hadharani.

Kwa hiyo inawezekana tuzo nyingi zimeenda kwa wasanii wasiostahili. Kuna uwezekano wasanii wengi wa Tanzania wamedhulumiwa tuzo zao na pia inawezekana kuna Watanzania wameshawahi kushinda tuzo wasizostahili.

Maana kila tuzo huwa zinakuwa na mifumo yake ambayo ni wanakamati pekee ndiyo wanayoifahamu ambayo ndiyo hutoa matokeo ya nani amekuwa mshindi kwenye kipengele kipi mbele ya jukwaa mubashara kabisa kwa mashabiki.

Siku ya jana Ali Kiba alikonga tena nyoyo za wapenda maendeleo kunako Bongo Fleva, baada ya kukabidhiwa tuzo yake rasmi huko Johannesburg, Afrika Kusini. Ni furaha iliyoje kuona Tanzania tumeweza kuonyesha uwezo na ushirikiano mpaka tuzo imerudi nchini.

Unaweza kujifunza mambo mengi kwenye jambo hili lililotokea kufuatia kosa la kiutendaji ndani ya kamati ya MTV EURO. Kikubwa ni namna umoja wetu unavyoweza kutuletea matokeo chanya kwenye tasnia ya burudani.

Tukiamua kupigania kitu bila kuingiza utimu tunaweza kufika mbali na tukawa msaada mkubwa kwa watu wetu maarufu pale wanapowania tuzo au nafasi flani wakishindanishwa na watu wa mataifa mengine.

 “Hii ni tuzo yetu, tumeipigania na tumeipata…. asanteni sana kwa kunipigia kura, namshukuru Mungu pia kwa baraka zake, familia yangu, managementi yangu na mashabiki,”  alishukuru Ali Kiba punde alipokabidhiwa tuzo hiyo yenye umaarufu wa aina yake barani Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles