30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

KABURI LA FARU JOHN LIFUKULIWE

waziri-mkuu

Na MASAYAGA MATINYI, ARUSHA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza kufukuliwa kwa kaburi la faru aliyefahamika kwa jina la John, anayedaiwa kufa katika eneo la Grumeti, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Alitoa agizo hilo jana mjini hapa wakati wa hotuba ya majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Alisema kwamba baada ya kuisoma ripoti ya awali aliyokabidhiwa Desemba 8, mwaka huu, hakuridhishwa nayo, hivyo ameagiza kitumwe kikosi kazi kwenda kuchunguza zaidi ukweli kuhusu kifo cha Faru John.

“Taarifa nilizopewa hazitoshi, tumetuma timu nyingine iende ikaone kaburi alimozikwa Faru John, kisha wafanye vipimo kubaini vinasaba vyake, kwa sababu hawa faru wana utambuzi maalumu.

“Wakimaliza kufanya hivyo, waende Ngorongoro wakalinganishe vinasaba vya John na vile vya watoto wake, lazima ukweli wote kama alikufa au vinginevyo ufahamike.

“Ripoti niliyonayo inaonyesha faru huyo alipimwa mara ya kwanza na daktari na hakukutwa na tatizo lolote lile. Hata alipopimwa kwa mara ya pili, hakukutwa pia na tatizo, lakini tunaambiwa alikufa.

“Tuna watumishi ambao wamepewa dhamana ya kulinda rasilimali zetu za wanyamapori, lakini wanakosa uaminifu na kushiriki katika kuzimaliza, hili kamwe halikubaliki,” alisema huku akishangiliwa.

Desemba 6, mwaka 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu Majaliwa aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha Faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizopo wilayani Ngorongoro, na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafugaji, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

Saa saba usiku wa Desemba 9, Waziri Mkuu alipokea taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru huyo kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko Hifadhi ya Grumeti.

Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu alisema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Profesa Maghembe alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati Faru John anahamishwa, alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwapo ndani ya kreta.

“Kati ya faru 37 waliokuwapo ndani ya kreta, watoto wake walikuwa 26, sawa na asilimia 70.2.

“Uamuzi wa kumwondoa Faru John ulikuwa ni muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Profesa Maghembe.

Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru huyo ilianza kudorora na alikufa Agosti 18, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru.

Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande, alisema pembe kubwa ya Faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.

Mbali ya Waziri Mkuu kupokea ripoti na pembe za faru huyo, siku tatu baada ya agizo hilo, maofisa watano wa NCAA wanaotuhumiwa kushiriki kumwondoa Faru John kutoka katika kreta hiyo, walikamatwa kwa mahojiano kujua ukweli kuhusu mazingira ya kupotea kwake.

Pia, Waziri Mkuu aliituhumu menejimenti na wafanyakazi wa NCAA, kuwa imejaa vitendo vya rushwa na wizi na asingeweza kuvumilia sakata la faru huyo ambaye alisema kuwa aliuzwa kwa Sh milioni 200 kwenye Hoteli ya Grumet iliyo Hifadhi ya Serengeti na kuwa walipokea fedha za awali Sh milioni 100.

Alisisitiza pia kwamba ikibainika kuna ambao wamekiuka taratibu na kusababisha kifo cha faru huyo, watawajibika.

Maofisa waliokamatwa na kuhojiwa ni pamoja na Israel Naman ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhifadhi wakati faru huyo akiondolewa, Cuthbert Lemanya, ambaye alikuwa Mkuu wa Kanda ya Creta na Dk. Athanas Nyaki, ambaye anadaiwa kumdunga sindano ya usingizi ili aweze kubebwa.

Maofisa wengine waliokamatwa ni aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Mamlaka ya Ngorongoro, Kuya Sayaleli na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Ikolojia, Patrice Mattey.

 

MBUNGE NASSARI

Wakati huo huo, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), amesema msimu wa siasa umepita, na sasa ni wakati wa kuwatumikia wananchi.

“Unajua kwetu Wameru anapokuja Mangi kukutembelea kwenye boma, ni lazima apokewe na Mangi mwenzake, sasa nilikuwa London, lakini nikasema lazima niende jimboni kwangu kushiriki ziara ya Waziri Mkuu.

“Ingawa sikuwahi, nimefurahi kupata fursa ya kuzungumza na Waziri Mkuu leo asubuhi aliponialika kunywa naye chai. Mahusiano ni jambo zuri katika kuwaletea wananchi maendeleo.

“Pamoja na ukweli kuwa majimbo yote isipokuwa moja katika Mkoa wa Arusha yanawakilishwa na wapinzani, ni lazima tufanye kazi pamoja na Serikali ya awamu ya tano kwa ajili ya wananchi wetu.

“Uchaguzi umepita, tuliochaguliwa tumechaguliwa, sasa siasa za ushindani kama wakati wa uchaguzi si wakati wake sasa, tusubiri uchaguzi mwingine 2020.

“Sasa tufanye kazi kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi wetu bila kujali itikadi zetu,” alisema Nassari ambaye amekuwa mbunge tangu 2012.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles