25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA YAIENGUA SIMBA KILELENI

yanga

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, timu ya Yanga, wameanza vema mzunguko wa pili wa ligi hiyo baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 3-0, jana katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kukalia usukani wa ligi hiyo.

Yanga wameishusha Simba kileleni, waliokuwa wakiongoza ligi hiyo baada ya kumalizika mzunguko wa kwanza wakiwa na pointi 35.

Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Elly Sasii kutoka Dar es Salaam, Yanga walionekana kucheza kwa kujiamini, huku wakifanya mashambulizi mengi, ambapo katika dakika ya tisa, mshambuliaji Amis Tambwe alikosa bao baada ya kupiga mpira wa kichwa ulioruka juu ya goli na kutoka nje.

JKT Ruvu nao walikuja juu na kufanya shambulizi katika dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji wake, Atupele Green, aliyewatoka mabeki wa Yanga na kupiga mpira mrefu ulioishia mikononi mwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.

Katika dakika ya 18, JKT Ruvu walishindwa kutumia nafasi vema baada ya Green kupiga shuti kwa mguu wa kushoto na kutoka nje, huku katika dakika ya 31 Yanga wakikosa bao baada ya Simon Msuva akiwa peke yake kupiga mpira uliopaa katika lango la maafande hao.

Yanga walianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 38, lililofungwa na Deus Kaseke, baada ya kumalizia pasi aliyopewa na Simon Msuva.

Kuingia kwa bao hilo kuliwashtua JKT Ruvu, ambao nao waliliandama lango la Yanga katika dakika ya 42 ambapo Ally Bilal alipiga mpira uliotoka juu ya lango na hivyo hadi mapumziko Yanga kuwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili JKT walifanya mabadiliko kwa kumtoa Yussuf Chuma na nafasi yake kuchukuliwa na Naftal Nashon, ambapo katika dakika ya 51 Yanga walikosa bao baada ya Ngoma kupiga shuti hafifu na kutoka nje.

Yanga nao walifanya mabadiliko katika dakika ya 55 kwa kumtoa Tambwe na kuingia Juma Makapu na katika dakika ya 57, Msuva aliipatia Yanga bao la pili kwa kichwa baada ya kupokea krosi ya Kaseke.

Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya JKT kuchanganyikiwa na katika dakika ya 63 nusura wajifunge, kutokana na Yussuf Chuwa kuwa katika harakati za kuokoa mpira, lakini kipa wao, Hamisi Seif aliokoa.

JKT Ruvu walifanya tena mabadiliko katika dakika ya 64 kwa kumtoa Ally Bilal na kuingia Mussa Juma na katika dakika 78 walifanya tena mabadiliko kwa kumtoa Atupele Green na kuingia Saady Kipanga, huku dakika ya 84 Yanga wakimtoa Thaban Kamusoko na kuingia Geofrey Mwashiuya.

Yanga walipata bao la tatu katika dakika 88 kupitia kwa Msuva, baada ya kipa wa JKT Ruvu, Hamisi Seif kudaka mpira lakini ulimshinda na kujaa wavuni.

Katika dakika ya 89 Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Donald Ngoma na kuingia Obrey Chirwa, na hadi dakika 90 zinamalizika Yanga walitoka kifua mbele kwa ushindi wa mabao 3-0.

Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Mwadui FC iliifunga Toto Africans bao 1-0 huku Mbeya City na Kagera Sugar zikitoka uwanjani bila kufungana na wakati Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zikitoka sare ya kufungana bao 1-1.

 JKT Ruvu:

Hamis Seif, Edward Charles, Michael Aidan, Yusup Chima/Naftal Nashon, Kelvin Nashon, Rahim Juma, Ally Bilali/Mussa Juma, Hassan Dilunga, Najim Magumu, Atulepe Green/Saady Kipanga, Edward Joseph.

Yanga:

Deogratius Munishi, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Thabani Kamusoko, Saimoni Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma/Obrey Chirwa, Amisi Tambwe/Juma Makapu, Deus Kaseke

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles