28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

UENYEKITI WA MBATIA NCCR-MAGEUZI WATIKISWA

mbatia

Na PATRICIA KIMELEMETA – dar es salaam

ALIYEKUA Mkuu wa Idara ya Kampeni ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura, ameanzisha fukuto kwa kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia kujiuzulu nafasi yake kwa madai kuwa ameshindwa kukiongoza chama hicho tangu alipoingia madarakani.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Sungura alisema bila kufanya hivyo, atashirikiana na wanachama wengine kumwondoa, kwa sababu amekisahau chama na kujikita katika shughuli nyingine zisizo na tija, jambo ambalo limechangia chama hicho kupata mbunge mmoja kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba, mwaka jana.

Alisema hali ilipofikia hivi sasa, chama hicho kinaweza kufa na kubaki historia ambayo haiwezi kuwasaidia wanachama wengine wanaopigania uhuru na demokrasia ndani ya nchi yao.

“Hatumwondoi Mbatia kwa sababu tunamchukia, bali tunamwondoa kwa kushindwa kuangalia masilahi ya chama na kujikita kwenye shughuli zisizo na tija, jambo ambalo limechangia kupoteza wabunge na kubaki na mbunge mmoja ambaye ndiye yeye katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

“Kwa sababu nafasi ya uenyekiti si ubatizo na wala si kiungo cha mwili wake, hata tuseme tutamuumiza, hivyo basi tunaamini vijana wenye mapenzi mema na chama wataungana na mimi kuhakikisha kuwa mwenyekiti anatoka madarakani ili tuweze kukiendesha chama,” alisema Sungura.

Aliongeza kuwa lengo lao ni kufanya siasa zenye tija, zikiwamo za kuzunguka mikoani kutafuta wanachama wapya na kuandaa viongozi ambao wataweza kukisimamia chama hadi uchaguzi ujao wa mwaka 2020.

Alisema kutokana na hali hiyo, nafasi yake itakabidhiwa kwa mwanachama mwingine kama alivyonyang’anywa mwenzake na kijiti kukabidhiwa yeye ili aweze kukiongoza chama.

Alisema kuwa Mbatia atabaki kuwa mshauri wa chama na hasa kama atakuwa amekubali kujiuzulu kwa hiari yake.

Sungura alijunga na chama hicho tangu mwaka 1992, akiwa mwanachama mwenye kadi N0. 00011763.

Alisema chama hicho kimeendelea kupoteza mvuto hali iliyosababisha baadhi ya wanachama kukihama.

Sungura alisema  ameshushwa baada ya kuona viongozi na wanachama wanaendelea au kujivua uanachama na uongozi kwa madai ya kuwa chama hakifanyi siasa, jambo ambalo unaweza kulitafsiri kama mwenyekiti ameshindwa kazi.

“Kazi ya mwenyekiti ni kushawishi watu wajiunge na chama,  wakishajiunga washawishike kubaki. Kama baadhi ya watu wanajiunga, kasha hawashawishiki kuendelea kubaki ndani, bado ni ujumbe kuwa mwenyekiti amekalia kiti kisicho chake,” alisema.

Alisema kama mwanachama au kiongozi wa chama, anaacha kupeleka malalamiko yake ndani ya vikao husika, badala yake anapeleka katika mahakama ya umma, lazima watu waungwana wajue kuna tatizo.

Hata hivyo, Ofisa Utawala wa chama hicho, Frolian Mbeo, alipoulizwa kuhusu kauli ya Sungura, alisema hadi jana mchana hakuwa na taarifa yoyote ya kuwapo malalamiko ya mwanachama huyo.

Alisema uamuzi wa Sungura, umekuja  baada ya kutolewa kwenye nafasi ya ukurugenzi wa kampeni, jambo ambalo limemfanya kuzunguka mikoani na kuanza kukisema vibaya chama.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles