27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, December 14, 2024

Contact us: [email protected]

Tendwa aficha siri ya mgogoro CUF

tendwaNA RACHEL MRISHO

MSAJILI mstaafu wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amesema siku atakayozungumzia mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) atamuudhi mtu.

Amesema ingawa anayo mengi ya kuzungumza kuhusu mgogoro huo, ameamua kukaa kimya kwa sababu akijitokeza kuzungumza kile anachokijua kuhusu sakata hilo wapo watakaoichukulia kauli yake kuwa ya kuchonganisha.

Tendwa aliyasema hayo mapema wiki hii katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumamosi lililomuuliza pamoja na mambo mengine mtizamo wake kuhusu mgogoro huo na jinsi alivyokifahamu chama hicho katika kipindi cha miaka 13 alichokuwa msajili wa vyama vya siasa.

Akijibu swali hilo bila kutaja jina la mtu, Tendwa alisema ameamua kukaa kimya tangu mgogoro huo ulipoibuka kuepuka kumuudhi mtu na pia kutokuwa katika kundi la watu wachonganishi ndani ya CUF.

“Kwa sasa siwezi kuongea chochote kwa sababu naweza kumuudhi mtu. Nimeamua kukaa kimya kwa muda mrefu bila kuzungumzia jambo lolote la kisiasa na hasa hili sakata linaloendelea ndani ya chama hicho ili kuepuka kuwa katika kundi la wachonganishi ndani ya CUF.

Msajili huyo ambaye alistaafu Agosti 2013 na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Mutungi alisema: “Kwa sababu nimeamua kukaa kimya acha niendelee kukaa kimya, nafanya hivi ili niwe mtazamaji, siwezi kuwa sehemu ya kuwachonganisha watu.

“Najua kiu yako unataka kuniuliza kuhusu yanayoendelea ndani ya CUF, ninayo ya kusema ila nikisema italeta shida maana nitamgusa mtu nami sipendi kumuudhi mtu.

“Nikizungumza sasa baadhi ya watu watahoji nazungumza kama nani wakati nilikwishaondoka ofisini. Ila Serikali ikinihitaji nami nitaenda kutoa mawazo yangu, hivi sasa nisingependa kuzungumzia lolote kwa waandishi wa habari,” alisema Tendwa.

Kauli hii ya Tendwa imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Bodi ya Wadhamini ya CUF kumfungulia kesi Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 12 waliokuwa wamefukuzwa.

Katika kesi hiyo bodi inaiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kumzuia msajili asifanye kazi nje ya mamlaka yake pamoja na kutambua maamuzi ya kikao kilichobatilishwa na Jaji Mutungi ambacho kilimpoka Prof. Lipumba na wenzake uanachama wao.

Miongoni mwa wanachama waliokuwa wamefukuzwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya, Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma, Wajumbe wa Baraza Kuu, Masudi Omari Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa na Kapasha Kapasha.

Baada ya kufunguliwa kwa shauri hilo, Wakili wa CUF, Juma Nassoro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa msingi wake ni kutoridhishwa na mwenendo wa msajili, Jaji Mutungi.

“Tunaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia msajili kufanya kazi nje ya mamlaka aliyonayo kwa sababu Mahakama Kuu ya Tanzania ilishawahi kutoa hukumu kuwa msajili hana mamlaka ya kuingilia mambo yanayoendelea ndani ya vyama vya siasa.

“Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya vyama ni kuharibu demokrasia,” alikaririwa akisema Wakili Nassoro.

Awali katika barua yake iliyobatilisha kunyang’anywa madaraka kwa Prof. Lipumba aliyokiandikia CUF, Jaji Mutungi alitoa hoja 11 za kuubatilisha baada ya kusikiliza pande mbili zinazogombania madaraka.

Barua hiyo ya Jaji Mutungi ilisomeka kuwa uamuzi wake umezingatia mamlaka na wajibu wa msajili wa kushughulikia migogoro ya vyama vya siasa.

Wakati huo huo, Ofisi ya Msajili imesisitiza msimamo wake wa kumtambua Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF na Maalim Seif Shariff Hamad kuwa ndiye Katibu Mkuu.

Barua ya ofisi hiyo ya Oktoba 4, mwaka huu iliyoelekezwa kwa makatibu wakuu wa vyama vya siasa ambayo gazeti hili imeiona ilikuwa na orodha ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu ambavyo ni 22 pamoja na viongozi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles