25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Kubenea aibua tuhuma mpya

kubenea-620x307Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), amemtuhumu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli, kupanga njama za kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa umeya wa Manispaa ya Kinondoni ili kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kishinde.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Kubenea alimtuhumu Kagurumjuli kuwa na nia ya kukwamisha halmashauri hiyo kuwa na baraza la madiwani kwa muda mrefu kwa sababu mipango yake haitakubaliwa na Chadema.

Alizitaja njama hizo kuwa ni pamoja na Kagurumjuli kuvunja baraza la madiwani kinyemela kwa kutumia kikao cha kawaida bila kuwemo kwa ajenda.

Alisema kikao cha kugawa halmashauri kinatakiwa kuwa kikao maalumu chenye ajenda badala ya kuwa na kikao cha kawaida kama kilichofanywa na Kagurumjuli.

“Katika kikao cha baraza la madiwani niliwahi kutoa hoja kuwa hatuwezi kugawa halmashauri bila kufanya mgawanyo wa madiwani kujua nani anaenda wapi na mkurugenzi alikubaliana na hoja hiyo mbele ya baraza.

“Jambo la kushangaza mkurugenzi huyo alisubiri tukiwa bungeni, Septemba 16 mwaka huu akavunja/kugawa halmashauri kinyemela katika kikao ambacho hakikuwa na ajenda hiyo. Na kikao cha kugawa halmashauri kinakuwa kikao maalumu wala hakiwezi kuwa kikao cha kawaida cha kujadili ajenda nyingine.

“Kwa hiyo yeye alihitisha kikao cha kawaida akaibuka na ajenda yake ya kugawa halmashauri,” alisema Kubenea.

Mbunge huyo alisema hilo limesababisha halmashauri hiyo iendelee kuwepo bila baraza la madiwani wala kamati za kudumu ambazo hushughulikia masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Kubenea alitaja njama nyingine ya Mkurugenzi huyo kuwa ni Chadema imwondoe diwani mmoja wa viti maalumu ili wabaki 6 watakaogawanywa watatu kwa kila Halmashauri suala ambalo ni kinyume cha sheria kwa kile alichodai kuwa madiwani wote walishapitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Hakuna sheria inayotulazimisha katika kila jimbo la uchaguzi kuwa na diwani mmoja au wawili wa viti maalumu na badala yake chama kinaweza kuweka idadi ya madiwani katika majimbo kimkakati.

“Mfano Kibamba tuna madiwani sita wa kuchaguliwa lakini tunaweza kupeleka diwani mmoja wa viti maalumu au tusipeleke hata mmoja lakini Kinondoni ambayo ina madiwani 10 tukaamua kupeleka madiwani watano wa viti maalumu kimkakati.

“Hata CCM ambayo ina madiwani wawili wa kuchaguliwa jimbo la Ubungo na wakiwa hawana diwani hata mmoja Kibamba wamepeleka madiwani watatu wa viti maalumu katika Jimbo la Kibamba,” alisema Kubenea.

Katika mlolongo wa tuhuma zake mpya, Kubenea alidai kupata taarifa kuwa diwani mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF) wa Jimbo la Ubungo anataka kuhamishiwa Jimbo la Kibamba ili kupunguza kura za upinzani wakati wa uchaguzi.

“Kagurumjuli anataka kumhamisha Mbunge wa Viti Maalumu wa CUF Kinondoni, Fatuma Mwasi, kwenda Ubungo ili kupunguza kura za Ukawa kutoka 24 kuwa 21.

“Zipo taarifa za uhakika kuwa Mbunge wa kuteuliwa na rais na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, naye anataka kuhamishiwa Jimbo la Kinondoni kutoka Ilala alikosajiliwa.

“Na mpango mwingine ni kumhamisha Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa kutoka Kibamba kuja Kinondoni pia ili kuongeza kura za CCM kwenye uchaguzi wa meya,” alisema Kubenea.

Hata hivyo, alisema mipango hiyo haitafanikiwa kwa sababu Chadema kitahakikisha uchaguzi unafanyika kwa kufuata taratibu.

Majimbo ya Kinondoni na Kibamba yana jumla ya madiwani 58, kati ya hao CCM kinao 20 na Ukawa 38 na baada ya kugawanywa kwa majimbo CCM itabaki na madiwani 18 na  Ukawa 24 kwa Halmashauri ya Kinondoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles