33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Hatima ya bidhaa za Kenya Ulaya mikononi mwa Magufuli

Joh-Magufuli

NAIROBI, KENYA

BAADA ya Uganda kukubali kusaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (EPAs) na Umoja wa Ulaya (EPAs), hatima ya bidhaa za Kenya kutozwa au kutotozwa katika soko la Ulaya itajulikana wakati Rais wa Tanzania, John Magufuli atakapoongoza kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baadaye wiki hii.

Kikao hicho kitakachofanyika mjini Arusha, pamoja na mambo mengine kinaonekana kama juhudi za mwisho kwa Kenya kushinikiza kusainiwa kwa makubaliano hayo na mataifa wanachama EAC ili kuepuka bidhaa zake kutozwa kodi ya asilimia 24 ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu.

Kikao hicho cha kilele cha wakuu wa EAC kinafuatia hatua ya hivi karibuni ya Tanzania kujiondoa ghafla katika mpango wake wa awali, ambao ungeshuhudia kwa pamoja mataifa wanachama yakisaini EPAs na Ulaya kabla ya tarehe ya mwisho Septemba 30.

Kenya na Rwanda tayari zilisaini mkataba mjini Brussels, Ubelgiji wiki iliyopita, huku Uganda ambayo awali iliungana na Tanzania kugoma kusaini kwa kile ilichoeleza suala hilo linahitaji makubaliano ya mataifa yote, sasa imeahidi kusaini wakati wa vikao vitakavyoanza keshokutwa.

Uamuzi huo wa Uganda unaiacha Tanzania pekee kwa vile EU imeashiria haihitaji saini ya mwanachama mwingine wa EAC, Burundi, hadi itakapotatua matatizo yake ya ndani.

Sudan Kusini – mwanachama mpya wa EAC, pia hailazimiki kusaini hadi kitakapopita kipindi cha miaka miwili.

Kama mwenyekiti wa kikao cha wakuu wa jumuiya hiyo, uamuzi utakaofanywa wiki hii na Rais Magufuli utatoa picha iwapo mauzo ya Kenya katika soko la EU yatatozwa kodi kuanzia mwezi ujao.

Mataifa yote ya Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) hutakiwa kusaini makubaliano ya EPAs kuwezesha uhusiano wa kiuchumi na EU isipokuwa kwa mataifa yaliyo kundi la nchi zenye maendeleo kidogo (LDCs).

Miongoni mwa mataifa sita wanachama EAC, ni Kenya pekee ambayo ni taifa linaloendelea – ikiwa haimo kundi la LDC, na hivyo ni pekee iwapo Tanzania haitasaini itakabiliwa na kibano cha EU.

Kwa mujibu wa takwimu, biashara na EU zimenufaisha kampuni 200 za Kenya kibiashara kutokana na uwekezaji wa euro bilioni mbili, sawa na shilingi za Kenya bilioni 224.

Tanzania imekuwa ikipinga makubaliano hayo kwa kile inachoeleza yataufanya ukanda wa EAC kuwa dampo la bidhaa kutoka EU kwa asilimia 80 na hivyo kuua viwanda vya ndani kutokana na ushindani usio wa haki.

Waziri wa Viwanda na Ujasiliamali wa Kenya, Adan Mohamed ambaye alihojiwa na Kamati ya Bunge la Ulaya ya Biashara ya Kimataifa, anaamini EU haitaitoza kodi Kenya mara watakapopata ushahidi wa uwapo wa dhamira ya dhati kutoka mataifa wanachama EAC.

“Mkutano wa Arusha utatoa msukumo zaidi kwa EPAs kutokana na umuhimu wa EU kama mshirika wa biashara na maendeleo wa muda mrefu,” alisema Mohamed.

Matarajio hayo ya Kenya inayonufaika zaidi na soko la EU kuliko jirani zake, yanamuweka Rais Magufuli katika wakati mgumu, akiwa kama mwenyekiti wa kikao cha juu cha EAC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles