NA CHRISTOPHER MSEKENA,
WANASEMA kama una bandama basi huwezi kujizuia kucheka popote pale ulipo, hata kama ni kwenye eneo ambao hutakiwi uonyeshe tabasamu.
Kama ni hivyo basi huwezi kushangaa pale ambapo mkongwe katika filamu za Kibongo, Abdallah Mkumbila ‘Muhogo Mchungu’ alipovunjwa mbavu na mmoja ya waumini ndani ya msikiti wakati ibada ikiendelea katika kile kipengele cha kutoa sadaka.
Akibonga na Juma3tata, Muhogo Mchungu anasema kila inapokaribia sikukuu kubwa huwa kuna sadaka inatolewa kwa waumini mbalimbali katika msikiti huo, ili kuwasaidia ambao wapo vibaya kiuchumi waweze kufurahia sikukuu kama watu wengine.
“Kuna sadaka huwa inatolewa kila inapokaribia sikukuu na safari hii kila muumini alipewa shilingi laki moja, sasa mimi nilijikuta naachia kicheko pale nilipomuona muumini mmoja ambaye alikuwa kwenye swala akiivuta ile hela aliyowekewa pembeni yake kwa hofu ya jirani yake kumwibia.
“Unajua mtu akiwa kwenye swala, huwezi kumkatisha hivyo yule aliyekuwa anazigawa zile laki moja moja baada ya kuona jamaa yupo kwenye swala akaamua kumuwekea pembeni ili atakapomaliza kuswali aichukue. Kweli pesa ni hatari, mtu hadi anafikia kuacha swala kwanza achukue pesa? Ilinishangaza sana kwakweli,” anasema Muhogo Mchungu.
Muhogo Mchungu aliongeza: “Nilijiuliza, inamaana huyu jamaa hakufumba macho? Hata kama yalikuwa wazi, aliwezaje kuona kilichokuwa kikiendelea na kuachana na swala kisha akazisogeza zile fedha kwanza? Kila nikikumbuka kwakweli nachoka kabisa.”