23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

RIYAMA: MTUACHE TULALE!

Riyama (1)

Na KYALAA SEHEYE,

STAA wa filamu za Kibongo, Riyama Ally amewafunga midomo wote waliokuwa wakibeza uhusiano wake na msanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva, Haji Mwalimu Mzee ‘Leo Mysterio’, baada ya kufunga naye ndoa hivi karibuni.

Minong’ono ilikuwa mingi mitaani na kwenye mitandao ya kijamii kuwa Riyama yupo kwenye uhusiano na Serengeti Boy kwa vile kijana huyo ni mdogo wake kiumri kwa miaka saba zaidi.

Akiondoa utata na Juma3tata, Riyama alisema wanaojua kusugua midomo waendelee lakini wao tayari wameshakuwa mwili mmoja, yeye akiwa mali halali ya Leo Mysterio.

“Wamesema sana, lakini sasa limewashuka shuuu! Wengine walisema sijui tunatafuta kiki, mara ooh! Sijui nimemzidi umri… inawahusu nini? Tayari tumeshafunga ndoa, sasa watuache tulale. Kama vilimilimi tushawakata,” anasema Riyama.

Mysterio ana umri wa miaka 26 huku Riyama akiwa na miaka 33, miaka saba zaidi ya mume wake huyo anayetamba kupendana mpaka kifo kitakapowatenganisha.

Riyama anasema: “Mimi najiheshimu sana, ndiyo maana huwezi kunikuta kwenye skendo yoyote. Hata mavazi yangu siku zote huwa ya heshima. Najitambua sana.

“Sasa kama kupenda au kupendwa na mtu mliyezidiana umri ni skendo, nipo tayari kwa hiyo. Mimi nilichoangalia ni mapenzi ya kweli, siyo umri. Mume wangu tumeelewana na naona kila mmoja anakidhi haja za mwenzake, sasa tatizo nini?

“Nampenda na nitamheshimu mume wangu hadi kifo kitakapotutenganisha, wanaosema na waseme, sisi tumeziba masikio yetu. Wala hatufikirii kuachana. Sisi ni wa maisha.

NDOA

BARAKA ZA WAZAZI

“Watu wengi wanaongelea ndoa hii vibaya wakiwa hawajui kuwa sisi Waislamu mkiridhiana wenyewe na wazazi wakatoa baraka zao, basi hakuna shida.

“Yote hayo tunayo. Kwanza tumeridhiana na wazazi wetu pande zote mbili wamekubali. Hatuna wasiwasi kwa hilo na ninafurahia ndoa yangu. Hao wanaotaka wanaume wenye mali na kuwazidi umri basi nawaambia watasubiri sana, mimi nimeshaolewa na mwanaume ambaye ndiye chaguo la moyo wangu.”

ALITUMIA VIGEZO GANI KUMPATA?

“Nilichoangalia kwanza mapenzi ya kweli na siyo kwa sababu nina jina. Kingine ni hofu ya Mungu, mume wangu anamheshimu sana Mungu, hilo najivunia lakini mwisho ni mchapa kazi.

“Hivi ninavyozungumza tayari yeye ndiye meneja wangu, ndiye atakayesimamia kazi zangu zote. Hivyo basi, natangaza rasmi ukitaka kufanya kazi na mimi hakikisha umepata ruksa kutoka kwa mume wangu.

“Kutana naye na muwekane sawa kuhusu namna ya kufanya kazi na Riyama. Kupitia yeye naamini sasa tutafanya kazi kitaalamu zaidi na pesa ya kipaji changu itaonekana.”

ISHU YA UMRI VIPI?

“Haini shida hata kidogo. Jamii ndiyo inayoongea na mimi siangalii watu wanasema nini. Lakini nikuambie tu kwamba, kuhusu umri wa mwanaume na mwanamke waliopendana na wanataka kuingia kwenye ndoa siyo ishu kabisa.

“Ninachojua mimi Mungu amempa daraja kubwa mwanaume na hata uwe na umri mkubwa kiasi gani, kwa kuwa umri ni namba kinachoangaliwa ni mapenzi ya kweli na unapata kile unachokitaka, basi. Hayo mengine maneno tu.”

ANA NENO KWA MASTAA

“Ninachowaambia wasanii wenzangu, ustaa una mwisho hivyo wajitahidi kujisitiri ili kuweza kulinda heshima ya mahusiano yao. Jamani tujitahidi kuvaa mavazi ya heshima, siyo kujiweka wazi ili wazazi wa upande wa pili waweze kukukubali.

“Nazungumza hasa na wasanii wenzangu wa kike. Hata kama hujaolewa, unaweza kuwa unajicheleweshea bahati kutokana na mavazi yako ya ovyo na tabia zisizofaa. Wasanii tubadilike, tunapewa majina mengi sana.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles