KUFUATIA Serikali kukaa kimya juu ya bajeti ya safari kwa ajili ya Olimpiki, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limesema halihusiki na halijui chochote kuhusiana na bajeti hiyo.
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imewasilisha serikalini bajeti ya Sh milioni 80 kwa ajili ya safari ya kwenda jijini Rio de Jeneiro, Brazil kushiriki katika michezo hiyo ambapo hadi sasa Serikali haijatoa msimamo wake.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu BMT, Mohamed Kiganja, alisema wao kama baraza hawana taarifa yoyote na kudai kuwa suala hilo linashughulikiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Sisi hatuna taarifa yoyote kuhusiana na hiyo bajeti, sasa hatuwezi kuiongelea, lakini taarifa za wanamichezo wetu kwenda Brazil tunazo,” alisema Kiganja.
TOC imewasilisha bajeti hiyo kwa Serikali itakayowawezesha wanamichezo 12 watakaoiwakilisha Tanzania katika michezo hiyo ambao wataondoka nchini kwa mafungu kuanzia Agosti 2.