23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Profesa Muhongo aagiza maji yapimwe tena

Profesa Sospeter Muhongo
Profesa Sospeter Muhongo

NA TERESIA MHAGAMA,

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameagiza maji yanayotoka katika vyanzo vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa Acacia North Mara, yapimwe tena ili kujiridhisha kama hayana athari kwa binadamu, mifugo na mazingira.

Profesa Muhongo alitoa agizo hilo juzi wilayani Tarime, Mkoa wa Mara  wakati  akizungumza na wananchi wa vijiji vya Matongo, Nyabichune, Mrwambe na Nyakungulu vinavyozunguka mgodi huo.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Muhongo alitoa agizo hilo baada ya kamati iliyokuwa ikitathmini migogoro kati ya mgodi na wananchi, kueleza matokeo ya vipimo vya maabara vinaonyesha kuwa maji hayo yana viwango vinavyokubalika kwa matumizi ya binadamu, mifugo na mazingira.

“Viwango vinavyopaswa kutumika katika upimaji wa maji haya lazima viwe vya Shirika la Afya Duniani (WHO). Hivyo basi, zichukuliwe tena sampuli za maji wakati wa kiangazi na wakati wa mvua na zipimwe tena.

“Sampuli hizo zigawiwe kwa makundi mbalimbali ikiwamo wananchi, mkuu wa wilaya, kamati iliyofanya tathmini na mimi mwenyewe ili kila kundi lipeleke katika maabara inayoaminika na baadaye kuwasilisha majibu ya uchunguzi.

“Sampuli za maji nitakayopatiwa mimi nitazipeleka kwenye nchi  mbalimbali duniani ikiwamo Ujerumani na Ubelgiji ambako kuna maabara za kisasa na zinazoaminika duniani.

“Nasisitiza uchunguzi wa kina ufanyike kwa sababu vyanzo vya maji katika sehemu nyingi zenye uchimbaji mkubwa na mdogo duniani, vimekuwa vikiathiriwa na shughuli za  migodi.

“Pamoja na hayo, katika suala hili nitawasiliana na mamlaka zinazosimamia sekta ya maji pamoja na mgodi ili kupata chanzo mbadala cha maji ili kuondoa malalamiko ya wananchi,”  alisema Profesa Muhongo.

Aliwaagiza pia wataalamu wa wizara yake kuhakikisha kila baada ya miezi mitatu, wachukue sampuli za maji  katika vyanzo vinavyozunguka mgodi na kuzipima ili kujiridhisha kuwa maji hayo hayana madhara kwa binadamu, mifugo na mazingira.

Pia, Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuwaasa wachimbaji wadogo wajiunge katika makundi yatakayowawezesha kufaidika na masuala mbalimbali  ikiwamo ruzuku  inayotolewa na Serikali.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, mwaka huu Dola za Marekani milioni 400 zitatumika kuwaendeleza wachimbaji wadogo kupitia ruzuku hiyo.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alimshukuru Profesa Muhongo kwa kuamua kuishughulikia changamoto hiyo ya maji kwa kuagiza upimaji wa maji hayo uwe endelevu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles