Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
HALI ya tahadhari ilionekana jana katika vitongoji mbalimbali kisiwani Unguja wakati Jeshi la Polisi Zanzibar lilipomhoji Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Habari kutoka mjini Unguja zilisema maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho yalikuwa katika hali ya tahadhari kuanzia Jumatatu usiku hadi jana, huku polisi wenye silaha wakionekana wakizunguka katika maeneo mengi ya mji wa Unguja.
Baadhi ya wananchi wa Zanzibar waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa katika hali ya tahadhari wakihofia uwezekano wa kuwapo matukio ya vurugu kutoka kwa wanachama wa CUF.
“Hapa tulipo tuko katika hali ya tahadhari, tunahofia wakati wowote hawa jamaa watalipuka na kuingia mitaani,” alisema mmoja wa wanausalama aliyezungumza na MTANZANIA.
Maalim alihojiwa jana chini ya ulinzi mkali wa polisi wakimtuhumu kutoa kauli za uchochezi alipokuwa katika ziara zake kisiwani Pemba, hivi karibuni.
Maalim aliwasili Makao Mkuu ya Polisi Ziwani saa 03:05 asubuhi akiongozana na Mwanasheria wake, Awadh Salim Said na Mkurugenzi wa Sheria wa CUF, Aboubakar Khamis Bakar.
Ilipofika saa 03:15 asubuhi, mahojiano hayo yalianza huku yakiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCP), Salum Msangi na kumalizika saa 06:05 mchana.
Habari zilizopatikana zilisema, katika mahojiano hayo, Maalim alituhumiwa kutoa kauli za uchochezi ikiwamo kumuita Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuwa ni dikteta na kuitisha mikutano ya hadhara na mikusanyiko bila kibali.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Wakili wa Maalim, Awadh alisema Maalim alituhumiwa kuwataka wananchi kutomtambua, Dk. Shein kuwa ni Rais halali wa Zanzibar.
Awadh alisema Maalim pia alihojiwa akituhumiwa kutoa kauli kwamba Dk. Shein hataweza kumaliza muda wake wa miaka mitano ya uongozi.
“Kwa swali hilo, Maalim aliwajibu kuwa hakusema Rais Shein hatamaliza muda wake wa uongozi wa miaka mitano bali alisema Shein hatamaliza muda wake wa uongozi.
“Alimuita Shein na si Rais Shein kwa sababu CUF hakimtambui kuwa Rais kwa sababu amekaa katika nafasi hiyo isivyo halali,” alisema.
Wakili huyo alisema Maalim aliwaeleza kwamba CUF itatumia njia za harakati za siasa kuhakikisha inafanikisha Shein hamalizi muda wake huo wa uongozi na wala si kwa kumdhuru.
Alisema mbali na swali hilo, polisi pia walimtaka Maalim Seif atoe ufafanuzi kuhusu kauli aliyoitoa ya kumuita Dk. Shein ni dikteta.
“Mwenyewe aliwaeleza kuwa anamchukulia kiongozi huyo kuwa ni dikteta kwa sababu ameingia kwa njia zisizo halali kwenye nafasi hiyo ya urais.
“Kuhusu mikusanyiko, walimuwekea video zinazoonyesha mikutano aliyoifanya kule Pemba, Maalim aliwajibu wananchi ndiyo waulizwe kwa sababu waliguswa na kuwapo kwake kisiwani Pemba na kumlaki kila anapojitokeza katika hadhara,” alisema Awadh.
Kwa mujibu wa Awadh polisi walimuachia Maalim kwa dhamana kwa sharti kwamba iwapo watamhitaji watamuita tena kwa mahojiano, na aliendelea na ziara zake katika Jimbo la Mfenesini mjini Unguja.
Maalim alidhaminiwa Wakili wake Awadh na Aboubakar Khamis.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCP), Salum Msangi alithibitisha kufanyika mahojiano hayo.
“Ni kweli tumemuhoji Maalim katika muda huo. Mahojiano hayo yalijikita katika matamko yake mbalimbali aliyoyatoa hivi karibuni kwenye mikutano yake ya siasa,” alisema.
Msangi alisema polisi watamuita tena Maalim kwa mahojiano iwapo maelezo aliyowapa hawataridhishwa nayo.
“Tunayapitia kwanza haya aliyotueleza na iwapo tutaona hayajaturidhisha tutamuita tena kwa mahojiano zaidi,” alisema Kamanda Msangi.
Mahojiano ya Maalim Seif na polisi Zanzibar yalipangwa kufanyika Mei 27, mwaka huu lakini yaliahirishwa baadaye kwa kile kilichodaiw ana jeshi hilo ni kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.