MOJA ya mambo ambayo Rais John Pombe Magufuli aliyasisitiza wakati wa kutangaza baraza lake la mawaziri lilikuwa ni kuwaasa kufanya sherehe kwa ajili ya uteuzi huo na kwamba kama wakifanya hivyo wajue pia siku ya kutenguliwa uteuzi wao wafanye sherehe pia.
Maudhui ya kauli hiyo ya Rais ni kwamba uteuzi huo ulikuwa ni wa kufanya kazi kulingana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” kwa kuwatumikia Watanzania na sio kwamba wajione wameukata.
Aidha maudhui mengine yanaweza kuwa uteuzi wao ulilenga kuwafanya wawe watumishi wa watu na sio watu wa kutumikia bali wawe ni watu wa kuwatumikia watu kwenye maeneo yao kwa kuzisimamia vyema rasilimali za umma zilizopo.
Kwa maneno mengine ni kwamba wateule hao walitakiwa kuibeba misalaba inayowaelemea wavuja jasho ili kuwaletea unafuu wa maisha pamoja na kuziba pengo lililopo kati ya wanyonge hao na wavuna jasho.
Mwangwi wa kile alichokisema hivi sasa umeanza kujionesha wazi baada ya kutenguliwa na ukuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa mteule wake, Anne Kilango Malecela katika kile ambacho kimeonekana kuwa ni kusema uongo kuhusu kutokuwapo kwa watumishi hewa mkoani humo.
Hata hivyo ilibainika baada ya uchunguzi kuwapo kwa wafanyakazi hewa zaidi ya 40 hali ambayo imemgharimu Kilango kwa uteuzi wake pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo kutenguliwa.
Kimsingi ni kwamba baadhi ya watendaji kwenye nafasi mbalimbali inaonesha kuwa walisahau ile kanuni ya Mwana TANU na baadaye CCM ambayo inasema “Nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko”.
Kukithiri kwa udanganyifu miongoni mwa watendaji kunaashiria kile ambacho Rais Magufuli alichokisema ni utendaji wa mazoea.
Kuwapo kwa idadi kubwa ya watumishi hewa kunaashiria ni jinsi gani baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia mamlaka wanayopewa kuvuna jasho la wavuja jasho bila kuona aibu.
Matukio kama hayo ndio yameleta athari kubwa kwa jamii na kuidhoofisha ile dhana ya utawala bora pamoja na uwezo wa Serikali kutambua haki za binadamu na kuipatia jamii maendeleo kwa uwiano na kwa uendelevu.
Kwa maana hiyo dhana kwamba utawala bora unatolewa kupitia uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji pamoja na mwitiko kwa mahitaji ya wavuja jasho, walioko pembezoni na walio na uwakilishi mdogo imekuwa ikipindishwa na wavuna jasho wachache .
Katika mazingira hayo tafsiri inayoweza kupatikana kuhusu uhusiano kati ya ubora wa Serikali na ufanisi mkubwa kwenye maendeleo kwamba kila kimoja kinachangia kukiboresha kingine nao ulipindishwa.
Hali hiyo ikiwa na maana kwamba badala yake maendeleo yameonekana kwa wavuna jasho ambao wamekuwa wakitumbua jasho la wavuja jasho bila chembe ya huruma.
Katika mazingira yote hayo ni dhahiri kuwa ubabaishaji umekuwa ukilelewa na kwa kutumia mwamvuli wa utawala bora mambo mengi yakawa yanafanyika kwa mazoea.
Katika nchi ambayo inadaiwa kuwa na rasilimali nyingi na za thamani ukiachilia mbali rasilimali watu iliyonayo bado imekuwa inaonekana kuwa na kipato cha chini na hali hiyo inatokana na kukithiri kwa ubadhirifu, wizi, matumizi mabaya ya madaraka ambavyo vyote vinahitimishwa na kutamalaki kwa ufisadi.
Mambo yote hayo yamekuwa tofauti na dhana iliyojengeka kwamba katika nchi ambayo ina kipato cha chini inatakiwa kupambana ili kuwa na Serikali yenye ufanisi na usimamizi mzuri ulio bora na utawala wa sheria na udhibiti mkubwa wa rushwa.
Kwa mfano inatakiwa kujiepusha na migogoro, kuzingatia haki za binadamu na kutoa huduma muhimu za umma. Hapa inamaanisha kuwa katika jamii ambayo inakumbana na kadhia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa pengo kati ya wavuna jasho na wavuja jasho, kuibuka migogoro ni jambo lililo dhahiri na hali kadhalika unaweza kuwapo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na inakuwa ni vigumu kutoa huduma muhimu kwa umma.
Ili nchi iweze kuingia kwenye orodha ya nchi zilizo na kipato kikubwa inatakiwa kuboresha utawala bora kwa kuzingatia na kuheshimu ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji wa serikali.
Hapa ni dhahiri kuwa nchi inatakiwa kuanza upya kwa kuwa mitazamo, fikra na vitendo vya viongozi na umma kwa jumla vilishakuwa sio vya kuielekeza jamii kwenye maendeleo kutokana na kukithiri kwa utendaji wa mazoea ambao uliyapa mahitaji ya jamii kisogo.
Hata hivyo ni nani wa kuwatetea wavuja jasho kama sio wabunge ambao ni wawakilishi wao? Lakini katika kile kinachoonekana kuwa mdudu rushwa anatambaa kila mahali nao ambapo wapo wabunge ambao wametuhumiwa kwa rushwa pia.
Hali hiyo inaonesha dhahiri kuwa wawakilishi wa aina hiyo huwavunjisha moyo watu wao wanaowawakilisha na hata kuona utukufu wa Bunge lenyewe kudhalilika.
Hali hiyo inasababisha kile alichowahi kusema Pius Msekwa, akiwa ni Mtanzania mweusi wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu wa Bunge mwaka 1962, katika kitabu chake “Towards Party Supremacy” (1977), akikiri kwamba “Bunge la uhuru liliheshimika kwa watawala na kwa wananchi kwa ujumla, sio tu kama chombo cha kutunga sheria, bali pia kama taasisi ambayo watu, kupitia wawakilishi wao, walitumia haki yao ya kutoa mawazo na uamuzi uliyogusa maisha yao na uongozi wa nchi”.
Sasa kama wapo wabunge wanaotuhumiwa kupokea rushwa ni mpiga kura gani atakayekuwa na imani na watunga sheria hao?
Hapa inatakiwa kurejea kile alichowahi kusema Martin Luther King Mwanaharakati wa Haki za Binadamu aliposema, “Maisha yetu huanza kuonekana hayana maana pale tunapokuwa kimya wakati mambo yasiyofaa yanaendelea kufanyika mbele yetu,”
Hapa kuna ukweli kwamba mambo ambayo yamekuwa yakifanyika ya utendaji wa mazoea pamoja na kadhi nyingine nyingi sio kwamba yamekuwa hayaonekani bali yamekuwa yanaonekana lakini ukawepo ukimya dhidi ya mambo hayo kwa kuyalea na kupoteza thamani ya maisha ya wavuja jasho.