20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Tukilea ubabaishaji tutakwenda kombo  

KASSIM MAJALIWANa Aloyce Ndeleio

MOJA ya mambo ambayo Rais John Pombe Magufuli aliyasisitiza wakati wa kutangaza baraza lake la mawaziri lilikuwa ni kuwaasa  kufanya sherehe kwa ajili ya uteuzi huo na kwamba kama wakifanya hivyo wajue pia siku ya kutenguliwa uteuzi wao wafanye sherehe pia.

Maudhui ya kauli hiyo ya Rais ni kwamba uteuzi huo ulikuwa ni wa kufanya kazi  kulingana na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” kwa kuwatumikia Watanzania na sio kwamba wajione wameukata.

Aidha maudhui mengine yanaweza kuwa uteuzi wao ulilenga  kuwafanya wawe watumishi wa watu na sio watu wa kutumikia bali wawe ni watu wa kuwatumikia watu  kwenye maeneo yao kwa kuzisimamia vyema rasilimali za umma zilizopo.

Kwa maneno mengine ni kwamba wateule hao walitakiwa kuibeba misalaba inayowaelemea wavuja jasho ili kuwaletea  unafuu wa maisha pamoja na kuziba pengo lililopo kati ya wanyonge hao na wavuna jasho.

Mwangwi wa kile alichokisema hivi sasa umeanza kujionesha wazi baada ya kutenguliwa na ukuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa mteule wake, Anne Kilango Malecela katika kile ambacho kimeonekana  kuwa ni kusema uongo kuhusu kutokuwapo kwa watumishi hewa mkoani humo.

Hata hivyo ilibainika baada ya uchunguzi kuwapo kwa wafanyakazi hewa  zaidi ya 40  hali ambayo imemgharimu Kilango  kwa uteuzi wake  pamoja na Katibu Tawala wa mkoa huo kutenguliwa.

Kimsingi ni kwamba baadhi ya watendaji kwenye  nafasi mbalimbali  inaonesha kuwa  walisahau ile kanuni ya Mwana TANU na baadaye CCM ambayo inasema “Nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko”.

Kukithiri kwa udanganyifu miongoni mwa watendaji  kunaashiria kile ambacho Rais Magufuli alichokisema ni utendaji wa mazoea.

Kuwapo kwa  idadi kubwa ya watumishi hewa kunaashiria  ni jinsi gani  baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia mamlaka  wanayopewa kuvuna jasho la wavuja jasho bila kuona aibu.

Matukio kama hayo ndio yameleta athari kubwa kwa jamii na kuidhoofisha ile dhana ya utawala bora pamoja na  uwezo wa Serikali kutambua haki za binadamu na kuipatia jamii maendeleo kwa uwiano na kwa uendelevu.

Kwa maana hiyo dhana kwamba utawala bora unatolewa kupitia uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji pamoja na mwitiko kwa mahitaji ya wavuja jasho, walioko pembezoni na walio na uwakilishi mdogo imekuwa ikipindishwa na wavuna jasho wachache .

Katika mazingira hayo tafsiri inayoweza kupatikana kuhusu uhusiano kati ya  ubora wa Serikali  na ufanisi mkubwa kwenye maendeleo kwamba  kila kimoja kinachangia kukiboresha kingine nao ulipindishwa.

Hali hiyo ikiwa na maana kwamba badala yake maendeleo yameonekana kwa wavuna jasho ambao wamekuwa wakitumbua jasho  la wavuja jasho bila chembe  ya huruma.

Katika mazingira yote hayo ni dhahiri kuwa ubabaishaji umekuwa ukilelewa na kwa kutumia mwamvuli wa utawala bora mambo mengi yakawa yanafanyika kwa mazoea.

Katika nchi ambayo inadaiwa kuwa na rasilimali nyingi  na za thamani ukiachilia mbali rasilimali watu  iliyonayo bado imekuwa  inaonekana kuwa na kipato cha chini na hali  hiyo inatokana na kukithiri kwa ubadhirifu, wizi, matumizi mabaya ya madaraka  ambavyo vyote vinahitimishwa na kutamalaki kwa ufisadi.

Mambo yote hayo yamekuwa tofauti na  dhana iliyojengeka kwamba katika nchi ambayo ina kipato cha chini  inatakiwa kupambana ili kuwa na Serikali yenye ufanisi na usimamizi mzuri ulio bora na utawala wa sheria na udhibiti mkubwa wa rushwa.

Kwa mfano inatakiwa  kujiepusha na migogoro, kuzingatia haki za binadamu na kutoa huduma muhimu za umma. Hapa inamaanisha  kuwa  katika jamii ambayo inakumbana na kadhia mbalimbali  ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa pengo kati ya wavuna jasho na wavuja jasho, kuibuka migogoro ni jambo lililo dhahiri  na hali kadhalika unaweza  kuwapo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na inakuwa ni vigumu kutoa huduma  muhimu kwa umma.

Ili nchi iweze kuingia kwenye orodha ya nchi zilizo na kipato kikubwa inatakiwa kuboresha utawala bora kwa kuzingatia  na kuheshimu ushirikishwaji wa wananchi  na uwajibikaji wa serikali.

Hapa ni dhahiri kuwa nchi inatakiwa kuanza upya kwa kuwa mitazamo, fikra na vitendo vya viongozi na umma kwa jumla vilishakuwa  sio vya kuielekeza jamii kwenye maendeleo kutokana na kukithiri kwa utendaji wa mazoea ambao uliyapa mahitaji ya jamii kisogo.

Hata hivyo ni nani  wa kuwatetea wavuja jasho kama sio wabunge ambao ni wawakilishi wao? Lakini katika kile kinachoonekana kuwa mdudu rushwa anatambaa kila mahali nao ambapo wapo wabunge ambao wametuhumiwa kwa rushwa pia.

Hali hiyo inaonesha dhahiri kuwa wawakilishi wa aina hiyo huwavunjisha moyo watu wao wanaowawakilisha na hata kuona  utukufu wa Bunge lenyewe kudhalilika.

Hali hiyo  inasababisha kile alichowahi kusema Pius Msekwa, akiwa ni  Mtanzania mweusi wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu wa Bunge mwaka 1962, katika kitabu chake “Towards Party Supremacy” (1977), akikiri kwamba “Bunge la uhuru liliheshimika kwa watawala na kwa wananchi kwa ujumla, sio tu kama chombo cha kutunga sheria, bali pia kama taasisi ambayo watu, kupitia wawakilishi wao, walitumia haki yao ya kutoa mawazo na uamuzi uliyogusa maisha yao na uongozi wa nchi”.

Sasa kama  wapo wabunge wanaotuhumiwa kupokea rushwa ni mpiga kura gani atakayekuwa na imani na watunga sheria hao?

Hapa  inatakiwa kurejea kile  alichowahi kusema Martin Luther King Mwanaharakati wa Haki za Binadamu aliposema, “Maisha yetu huanza kuonekana  hayana maana pale tunapokuwa kimya wakati mambo yasiyofaa  yanaendelea  kufanyika mbele yetu,”

Hapa kuna ukweli kwamba mambo ambayo yamekuwa yakifanyika ya utendaji wa mazoea pamoja na kadhi nyingine  nyingi sio kwamba yamekuwa hayaonekani bali yamekuwa  yanaonekana lakini ukawepo ukimya  dhidi ya mambo hayo  kwa kuyalea na kupoteza thamani ya maisha ya wavuja jasho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles