21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Flyover na dira yetu ya maendeleo

FlyoverKATIKA makala hii ninayoinukuu katika mjadala wangu wa leo Social science as imperialism, Mwanahistoria maarufu, Claude Ake anazungumzia dhana kuu mbili za maendeleo ambazo tumerithishwa na fikra za wageni.

Dhana ya kwanza ni ile ya kusema kuwa jamii huenda kwa hatua na hatua ya mwisho ni ile ya kufikia hatua fulani ya juu ya maendeleo na hatua hizi ni zile tu ambazo zimepitiwa na Wazungu. Katika mtazamo huu, hatua za maendeleo zinazopitiwa na jamii nyingine na hasa za kwetu Afrika, hazionekani zinafaa na kuwa tunalazimishwa kufuata hatua zile ambazo Wazungu wamefikia.

Na dhana ya pili ni ile kuwa ulaya ndio jamii pekee ya mfano wa maendeleo, The Ideal Society na kama hatujawa kama ulaya basi hatujaendelea. Kwa ufupi ni kuwa maendeleo maana yake ni kufika ulaya na maisha maana yake ni kuishi kama ulaya.

Ninavyoangalia mfumo wa ujenzi wa majumba, mfumo wa mipango ya ujenzi wa barabara na uwekezaji unafadhiliwa na wazungu, wachina au Japan, ni katika kutekeleza hiki ambacho Claude Ake anaita ubeberu wa kifikra kupitia tafsiri ya maendeleo.

Ndio najiuliza kama ambavyo Ana Mgwira, Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, kama kweli kujenga Flyover, ni jambo la tija katika mazingira ambapo reli zote zimedorora na maendeleo vijijini ni kitendawili? Je, ni kweli Flyover itatatua tatizo la foleni jijini Dar es Salaam? Na Je, ni kweli tatizo la foleni linatokana na barabara zisizopitisha magari mengi kwa wakati mmoja au kuna chanzo kingine?

SIdhani kama naweza kujibu maswali yote! Flyover inajengwa na hili ni jambo la kunifikirisha, mahali ambapo kuna kituo cha Reli ya TAZARA ambayo kwa miaka kadhaa sasa utendaji wake hauridhishi na imekumbwa na kashfa mbalimbali na kushindwa kulipa mishahara na stahiki zingine, lakini pia ni reli ambayo kwa kweli inachechehemea kutokana na kushindwa kufanya biashara na sababu moja ni kufumba macho kwa Serikali juu ya wanaoamua kusafirisha mizigo mizito kwa magari na kuharibu barabara zetu.

Lakini tunasahau kuwa, kufunguka kwa reli na kama kungekwenda sambamba na uimarishaji wa shughuli za uchumi kando kando ya reli yenyewe, tungeweza kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapatia nyenzo ya kusafirisha bidhaa, kuimarisha mawasiliano na kuwarahisishia wananchi wanaokaa huko vichochoroni kufika maeneo yenye huduma za afya, biashara, masoko ya mazao yao ya kilimo na kadhalika, kwa urahisi zaidi.
TAZARA, sasa imekuwa ni tembo mweupe, yaani kinyago cha urembo tu kinachoweza kuwekwa makumbusho.

Tanzania, kama ilivyo nchi nyingi za Afrika imekumbwa na sifa mbaya ya kushuhudia miradi ya maendeleo iliyoanzishwa miaka ya 1970 na kufaidisha wengi, ikirudi nyuma, ikifa, ikiharibika na huku tukiendelea kuangalia ikichakaa bila kufanya lolote na kwa upande mwingine miradi mipya ya mfano huo huo inaanzishwa.

Nichepuke kidogo, najiuliza kama kweli shida yetu kimaendeleo ni kutofika kule ulaya walikofika. Naambiwa kuwa kamera nne za ulinzi za pale daraja la Kigamboni zimeshapotea, kama ambavyo bomba za maji zilivyopotea muda mfupi baada ya Uwanja wa Taifa ulipofunguliwa.

Sikushangaa kuona hilo kwa sababu kwangu ni ishara ya maisha duni ya wananchi na maisha ya kubabia yanawafanya kuchakura mitaani na wakiona chochote wanachoweza kukiuza kujipatia kipato, watakiiba, watakichomoa, wapate namna ya kujikimu.

Unapojenga kitu kikubwa kama daraja na kama barabara kwa mabilioni ya dola lakini wananchi wanabaki pembeni kama watazamaji kwenye mpira, hawawezi kuingilia kati na kusema refa ulikosea, nadhani ni kujenga fikra ambazo hazina uhakika nini hasa wananchi wanataka. Tunaweza kuwa na uwezo wa kuamua nini wananchi wapewe lakini inaweza kuwa sio kipaumbele chao.

Tena ninafurahi kuwa barabara hii inajengwa na Wajapan. Huko kuna mtaalamu mmoja Dk. Kauro Ishakawa ambaye alijenga mfumo wa uchambuzi wa matatizo katika uongozi, fishbone diagram, ambao unasaidia kutambua tatizo halisi linalokumba jamii, taifa au mahala pa kazi.

Najua wao waliamua kutusaidia kadri tulivyoomba, kuwa watu wetu wakienda Uwanja wa Ndege wanachelewa, kwa hiyo mtusaidie kujenga barabara.

Na wao wanasema sawa, lakini hawa WanaIshakawa wanajua kuwa tatizo halisi, ‘real cause or the effective cause’ la maendeleo ya nchi yetu ni kukosekana kwa mpango madhubuti wa kufufua uchumi na kuendelea kuwapo kwa kundi kubwa la wananchi wakiishi nje ya mfumo rasmi wa kipato na wengine hawajui hata watakula nini kesho kutokana na kukosekana ajira, kuzorota kwa kilimo na kutokuwapo na viwanda.

Lakini kwetu limekuwa ni jambo la sifa kuwa na daraja kubwa, na sasa kuwa na Flyover na tunataka na sisi tuonekana kama ulaya, kama alivyowahi kusema mmoja wa marais wetu waliotangulia. Ni daraja la aina yake Afrika Mashariki! Ni Flyover ya kwanza na tuache viongozi waliobuni wazo hili kupewa sifa! Na kadhalika.

Lakini katika jiji hili mafuriko katika barabara na makazi ya watu ni jambo la kawaida, wananchi wanatumia mifuko ya rambo kutupa kinyesi, wananchi hawajui watalala wapi kwa kuongezeka idadi ya watu wanaokimbia vijijini kuja kuishi mijini na shule na hospitali zikishindwa kufanya kazi yake ipasavyo… barabara nzuri nzuri, ndiyo; tunaihitaji! Je, ni kipaumbele kwa sasa?

Niliwahi kuandika miaka kama ishirini iliyopita kuwa tatizo la Dar es Salaam ni mipango miji na hilo ni tatizo kila mahali unapokwenda… mipango miji haina uyakinifu katika kufikiriwa kwake, tunapanga kwa mazoea na kwa sababu ufisadi nao ulichukua nafasi yake, basi hakuna kitu kilichopangwa kwa kufikiria kesho, bali kwa kufikiria leo, sasa!

Na ukiona matatizo ya mipango miji katika maeneo, majiji mapya, unaona makosa yakijirudia na huenda nako tutafikiria kujenga Flyover. Kama tutaendelea kufanya mipango miji kwa mtindo wa sasa, tutafikiria kujenga Flyover hata Chalinze, Singida na Sumbawanga… kwa sababu hakuna fikra zinazokwenda mbele, ni fikra za kufanya kazi kwa mazoea. Nina imani kuwa ni Flyover, daraja, lililotokana na kufikiri kwa mazoea na sio mahitaji halisi ya nchi!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles