Na Sheila Katikula, Mwanza
Kinara wa usafirishaji wa wahamiaji haramu, David Kapangala (31) na wenzake watatu wamekamatwa mkoani Mwanza na Idara ya Uhamiaji kwa kosa la kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji haramu kutoka nchi mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Kamishina wa Idara ya Uhamija Mkoa wa Mwanza, Bahati Mwaifuge, amesema wanawashikilia watuhumiwa hao kwa kosa la kuwahifadhi, kuwasafirisha wahamiaji haramu 54 wakiwamo Warundi 13 ambao ni wanawake, Mkenya mmoja na Waethiopia 11 na watanzania wanne ambao wamekamatwa kwa nyakati tofauti.
Amesema idara hiyo imewatia nguvuni wahusika warioshiriki kuwahifadhi kwenye nyumbani hiyo iliyopo mtaa wa Majengo Mapya Kata ya Mkolani kwa kuwatunza wahamiaji hao.
“Tulikuwa tukimtafuta tangu siku nyingi David, tulienda hapo alipopanga kwa lengo la kumkamata tulipofika baada ya kufanya ukaguzi tukagundua kuna watu juu ya dari tulipowaambia washuke walitoka watu 11,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, amewataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya kutunza na kusafirisha wahamiaji hao kwani kufanya hivyo ni kosa na sheria zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo amelipongeza jeshi hilo kwa jitihada zao za kufanya kazi usiku na mchana na kupelekea kuwakamata wahamiaji hao jijini hapa.
“Nawaomba wananchi wajishughulishe na kazi za kilimo kwani mvua zinaendelea kunyesha  waache kufanya kazi ambazo siyo za halali,” amesema Mongela.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Mapya iliyopo Kata ya Mkolani, Ramadhan Musabi, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili kuepusha vitendo hivyo,kwani mtuhumiwa huyo mara ya kwanza waliwakamata wahamiaji kwenye eneo la nyumba ya David wakiwa kwenye gari likiwa limepaki kwenye shama la mahindi.
“Viongozi wa mitaa washirikiane na wananchi ili waendelee kubaini vitendo vya uharifu na wasikubali kudanganyika na rushwa ndogo ndogo bali waendeleze uzalendo wa nchi,”amesema Musabi.