Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma inawashikilia wanafunzi 13 wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) cha jijini hapa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani.
Imedaiwa kwamba wanafunzi hao kwa  kutumia rushwa waliweza kurudia kufanya mtihani nje ya chumba cha mtihani na baadae walijaribu kuingiza karatasi za kujibia mtihani kwenye mfumo rasmi ambapo alidai Chuo kiliwabaini na kutoa taarifa Takukuru.
Hayo yameelezwa leo Januari 16 mwaka huu na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo, wakati akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari juu  ya utendaji wa Takukuru Mkoa wa Dodoma kwa robo ya Oktoba hadi Desemba mwaka 2020.
Kibwengo amesema wanawashikilia wanafunzi hao wa mwaka wa tatu kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa na udanganyifu wakati wa kufanya mtihani marudio ( supplementary examination) wa somo la Applied Statistics II uliofanyika Novemba mwaka jana chuoni hapo.
Amesema uchunguzi wa awali umeonesha kwamba wanafunzi hao kwa kutumia rushwa waliweza kurudia kufanya mtihani huo nje ya chumba cha mtihani na baadae walijaribu kuingiza karatasi za kujibia mtihani kwenye mfumo rasmi ambapo alidai Chuo kiliwabaini na kutoa taarifa Takukuru.
Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Dodoma amewataka waliokuwa wanafunzi wa Chuo hicho, Evarist Nyaki na Lameck Kawinga kuripoti mara moja kwenye ofisi za Takukuru Mkoani Dodoma kwa ajili ya kusaidia uchunguzi huo.