30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DC Uvinza aishi kwenye kontena, Jafo aagiza wahusika wakamatwe

Na Editha Karlo, Uvinza

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(TAMISEMI), Seleman Jafo ameamuru kukamatwa na kuwekwa ndani kwa viongozi na wasimamizi wa miradi wa wakala wa majengo nchini (TBA) Mkoa Kigoma kwa kushindwa kukamilisha miradi ya ujenzi waliyopewa huku wakichukua kiasi kikubwa cha pesa.

Jengo la Utawala la halmashauri ya wilaya Uvinza ambalo limekwama huku TBA wakiwa wamepokea milioni 900

Jafo ametoa agizo hilo leo Jumamosi Januari 16, kwenye ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma

Akiwa kwenye ziara ya kukagua majengo ya Utawala ya viongozi na watumishi walio chini ya wizara hiyo wilayani Uvinza Jafo amekerwa na taarifa ya ujenzi wa majengo hayo.

Waziri Jafo ameeleza kukerwa na taarifa ya TBA kupewa kiasi cha Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya Uvinza miaka mitano iliyopita ambapo hadi sasa nyumba hiyo imefikia usawa wa msingi.

Aidha, Jafo ameonyesha kukerwa kutokana na kukwama jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Uvinza ambapo kiasi cha Sh milioni 900 kimetolewa lakini mradi umekwama kwa miaka zaidi ya mitatu na kwa sasa ujenzi upo usawa wa madirisha.

Awali, akitoa taarifa kwa Waziri, Meneja wa miradi ya ujenzi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Masawika Kachenje amesema miradi hiyo ilianza mwaka 2013 na ilipaswa kukamilika mwaka 2018 na waliomba pesa kwenye miradi hiyo kama malipo ya awali.

Jengo la nyumba ya Mkuu wa Wilaya Uvinza ambalo limekwama tangu mwaka 2013 licha ya watekelezaji wa mradi wakala wa majengo (TBA) kupokea milioni 500 kwa ajili ya ujenzi huo

Kachenje amesema pesa kwenye miradi hiyo zimeingizwa kwenye akaunti ya TBA makao makuu lakini taarifa zinaonyesha kuwa pesa hizo hazipelekwi kwenye miradi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko amemweleza Waziri Jafo kuwa analazimika kuishi kwenye kontena zilizoachwa na mradi wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami wa Kidahwe hadi Uvinza kutokana na kukwama kwa ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa wilaya.

Mrindoko amesema kuwa wamefanya jitihada kuhakikisha TBA wanarejesha fedha lakini hakuna jitihada iliyofanyika.

Kutokana na hali hiyo Jafo ameagiza kuorodheshwa kwa miradi yote iliyokwama kwa mkoa wa Kigoma ambayo ilikuwa inatekelezwa na TBA, kueleza thamani ya kazi iliyofanyika na kiasi cha pesa kilichopelekwa na taarifa hiyo iwasilishwe ofisini kwake aweze kuifanyia kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles