24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yakusanya trilioni 7.9/-

MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya jumla ya Sh trilioni 7.9 kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2018/19 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana.

Kiwango hicho ni kikubwa kikilinganishwa na Sh trilioni 7.8 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha 2017/18.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema makusanyo ya Desemba 2018 yaliongezeka kuzidi makusanyo ya miezi yote iliyopita kwa mwaka huu ambayo yalikuwa Sh trilioni 1.63.

“Mbali na makusanyo hayo ya mwezi Desemba, katika Novemba 2018 TRA ilikusanya jumla ya shilingi trilioni 1.21 na Oktoba 2018 zilikusanywa jumla ya shilingi trilioni 1.29. Nachukua fursa hii kuwashukuru walipakodi wote kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati,” alisema Kayombo.

Alisema katika kutatua kero na malalamiko mbalimbali ya walipakodi, uongozi wa TRA umeamua kwamba kila siku ya Alhamisi itakuwa ni siku maalumu kwa mameneja wa mikoa na wilaya nchini kuwasikiliza na kutatua changamoto za walipakodi.

“Pamoja na kutenga siku hiyo maalumu, tumeanzisha Kituo cha Ushauri kwa Walipakodi kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho kipo katika jengo la NHC kwenye makutano ya Mtaa wa Samora na Bridge kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwa karibu na walipakodi.

“Tumeanza kwa Dar es Salaam, lakini vituo hivi vitaendelea kufunguliwa katika mikoa mingine nchini,” alieleza Kayombo

Pia Kayombo aliwakumbusha wamiliki wa majengo kote nchini kulipia kodi ya majengo ambayo viwango vyake ni Sh 10,000 kwa nyumba za kawaida, Sh 50,000  kwa kila sakafu ya ghorofa na Sh 20,000 kwa ghorofa za wilayani na vijijini.

“Sambamba na kuwakumbusha wamiliki wa majengo kulipia kodi ya majengo, napenda kuchukua fursa hii kuwasisitiza wafanyabiashara wadogo wadogo kuchangamkia vitambulisho vya wamachinga ambavyo vinapatikana nchi nzima katika ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya kwa shilingi 20,000. Vitambulisho hivyo ni maalumu kwa wale tu ambao mauzo yao ghafi hayazidi shilingi milioni nne kwa mwaka,” alisisitiza.

Kayombo ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari huku TRA ikiwa imeanza kampeni rasmi ya usajili wa walipakodi wapya nchini kwa kuwapatia namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) bure katika maeneo wanayofanyia biashara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles