24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru ampongeza Kamanda Shanna


PETER FABIAN-MWANZA

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna na kumtaka kuongeza nguvu ya maarifa katika jukumu la kulinda rasilimali za madini nchini ikiwemo kudhibiti matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani.

Dk. Bashiru alitoa pongezi hizo juzi mkoani hapa wakati akizungumza na viongozi wa taasisi za Serikali waliohudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoani hapa.

Alisema Kamanda Shanna ameonesha ushupavu kutokana na kufanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha rasilimali ya madini ya dhahabu hivi karibuni.

“Nikupongeze na timu yako kwa kutekeleza majukumu yenu na maagizo ya Rais ya ulinzi wa rasilimali za taifa zilizokuwa zikiibwa na watu wachache na mara nyingine kutolipiwa kodi hali iliyokuwa imezoeleka huko nyuma na kulifanya taifa kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo na kupelekea wananchi kuichukia Serikali,” alisema.

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinao wajibu wa kulinda rasilimali mbalimbali ikiwemo madini ya aina zote, kudhibiti uvuvi haramu ambao umekuwa janga linalokwamisha uvuvi endelevu na kusababisha rasilimali hiyo kuanza kutoweka kwenye baadhi ya maeneo ya Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika.

“Kamanda kama umepungukiwa nguvu sema tukuombee kwa viongozi wakuongezee vitendea kazi na askari kupambana na uhalifu wa kila aina na kuwakamata hata wanasiasa, ikiwamo viongozi wa chama, wabunge na madiwani ambao watabainika watashiriki kwenye uvuvi haramu na kusaidia utoroshwaji wa madini na kuikosesha Serikali kodi na mapato,” alisisitiza.

Alisema taifa kwa sasa chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli liko katika mapambano na vita ya kujenga uchumi ili kulifikisha taifa kwenye uchumi wa kati, ni wajibu wa kila kiongozi, mwananchi na wanachama wote kwa pamoja kumuunga mkono rais ili kufikia azma ya uchumi wa kati.

Bashiru alisema katika kujenga taifa lenye uchumi imara ni lazima kuwahimiza wananchi kulipa kodi na mapato ili Serikali iweze kupata fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, mradi wa umeme wa uhakika wa maji na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kufanikisha upatikanaji wa huduma muhimu katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo, usafiri na usafirishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles