31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

JPM asema hatochoka kufanya mabadiliko

Mwandishi Wetu, Dar

RAIS Dk. John Magufuli, ameonyesha kukerwa na malumbano ya viongozi wa ngazi mbalimbali na kuwaonya kuwa hatasita kuwachukulia hatua.

Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana wakati wa kuapisha viongozi mbalimbali, Rais Dk. Magufuli alisema amekuwa akifuatilia na kusoma ujumbe mfupi wa maneno wa baadhi ya watendaji wake akiwemo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za (Tamisemi). Dk. Zainabu Chaula (ujenzi wa hospitali) wanavyojibizana ndipo alipochukua uamuzi wa kuwaunganisha katika wizara moja.

Alisema katika kufuatilia kwake, alijaribu kuangalia yule anayeshambuliwa sana na aliona yule anayeshindiliwa maneno zaidi ndiye anayefaa kuwekwa naye katika wizara moja, hivyo aliamua kumchukua  Dk. Zainabu  aliyesimamia ujenzi wa vituo 300 kwa kushirikiana na Tamisemi na kumpeleka kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.

Alisema wakati wa mvutano huo, msimamizi wa fedha alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambaye ndiye anayesimamia fedha na kwa kuwa kulikuwa na mvutano baina ya naibu katibu mkuu na waziri aliamua kuwaweka pamoja ili aweze kusimamia ugawaji wa fedha hizo katika maeneo yote ya nchi.

Alisema katika ufuatiliaji wake, anajua kuwa kuna halmashauri ambazo viongozi wake wanaongoza kwa kugombana, huku akitaja Halmashauri ya Nyasa ambapo mkuu wa wilaya na mkurugenzi hawaelewani, akisema kuwa hao amewaweka kiporo.

Alisema ugomvi mwingine ni wa mkuu wa wilaya na mbunge ambaye amefikia hatua ya kumtukana mkuu wa wilaya ambaye ni mke wa mtu bila kujali kuwa kuna kamati za nidhamu za chama ambazo zinaweza kumchukulia hatua na anaweza kupoteza hata ubunge wake, huku akimtaka mbunge huyo kwenda kuomba msamaha.

“Pale Dodoma Mkurugenzi wa Jiji na mkuu wa wilaya walikuwa wanagombana, nikatuma ujumbe endeleeni kugombana mtagombania vijijini siku moja, sasa hivi naona yameisha,” alisema.

Aliwataka watendaji katika wizara kutochukua wizara kama mali zao bali wazichukue kama mali za Watanzania wakijua wana jukumu la kwenda kufanya kazi.

Upungufu balozi

Rais Magufuli alisema ameona pia kuna upungufu mkubwa katika balozi nje ya nchi na kuamua kufanya  uamuzi wa kuziimarisha kwa kumchukua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya ambaye aliona ni miongoni mwa makatibu wakuu waliotembea sana nje hivyo ni vyema aende akakae nje ili akaiwakilishe vyema nchi.

Alisema katika kuangalia kwake, Wizara ya Afya imekuwa na mikutano mingi sana ya nje na amekuwa akipewa vibali vingi na Katibu Mkuu Kiongozi, akifafanua kuwa hata hivyo amefanya kazi yake vizuri sana katika kipindi chote cha utumishi wake.

Aliwataka watendaji na wote walioapishwa kusimamia masuala ya kitaifa ili kuifikisha nchi sehemu nzuri, pia wasiogope kufanya maamuzi na hakuna atakayehukumiwa kwa kufanya maamuzi yote hata kama ni mabaya lakini kwa nia njema.

Agomea ombi la likizo

Rais Magufuli pia alikataa ombi la Spika wa Bunge, Job Ndugai la kutaka mawaziri mmoja mmoja wapatiwe likizo ili waweze kupumzika.

Spika wa Bunge, Ndugai aliwaombea mawaziri likizo hizo jana wakati aliposimama kuzungumza baada ya kuapishwa kwa viongozi wapya wa Serikali walioteuliwa na Rais juzi.

Ndugai ambaye alisema ana matumaini kuwa Bunge la mwaka huu litakuwa la mafanikio na litashirikiana na watakaotaka kuwasiliana nalo, alisema mawaziri wanaonekana kuwa wamechoka.

“Serikali ya awamu ya Tano, ina kasi ya kipekee ambayo hatukuwahi kuiona huko nyuma kwa hiyo ninapowapongeza hawa ndugu zangu, niwape pole kidogo, mvute soksi”.

“Maana Rais, wakati zoezi la kuapisha linaendelea nilikuwa ninaangaliana na mawaziri naona wamechoka. Nikajiuliza hivi mawaziri huwa mna likizo? Nawaombea likizo mheshimiwa Rais.

“Mmojammoja angalau mwezi kidogo, lakini umewapa wasaidizi na mimi kwakuwa nafanya nao kazi kwa karibu mawaziri kule bungeni kwa kweli nashuhudia wanachapa kazi ambayo haijawahi kuonekana,” alisema Ndugai.

Baada ya kueleza hayo, Rais Magufuli alisema anafahamu majukumu makubwa waliyonayo lakini hata yeye hajachukua likizo.

 “Kwa makatibu wakuu na wizara, najua mna majukumu makubwa na ndio maana Spika anazungumza hapa hamjachukua likizo  hata mimi sijachukua likizo.

“Hapa nilipo niko hoi kweli, lakini utaichukua likizo wakati wananchi unaowaongoza hawana likizo? Kwa sababu ukiangalia wakulima, wafanyakazi, wavuvi, wafugaji,  katika sekta mbalimbali Watanzania hao wote milioni 55 hawana likizo katika shughuli zao.

‘Kwa hiyo saa zingine inatuwia vigumu kuchukua likizo wakati waliotuchagua hawana likizo. Wanataka maendeleo yale ambayo tuliwaahidi,” alisema  Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema hata wakati wa kuapisha huko alichelewa takribani dakika kumi kwa usiku alikuwa akifanya mawasiliano na watu wanaoileta ndege mpya nyingine aina ya Air bus.

“Usiku ni kama sikulala kwasababu nilikuwa na communicate (nawasiliana) na waliofata ndege ya Air Bus nyingine ambayo inawezekana ikaondoka leo (jana). Sasa ni lazima tufanye negotiation (majadiliano).

“Kule wakawa wananipa taarifa, Je, mmechukua taili zote za spea? Je, mmkiondoka mtatua wapi? Mtafika saa ngapi hapa? Hayo yote lazima wakueleze, Je, mmei-test (jaribu) ndege? Wamesema sasa hivi tumekaa angani zaidi ya saa nne tumezunguka.

“Je, iko sawa sawa? Hayo yote ni usiku, ukichukua likizo hayatafanyika. Nawaomba mawaziri na watendaji Serikalini, angalau hii miaka mitano tuteseke kwa ajili ya Watanzania, katika mingine inayokuja” alisema Rais Magufuli.

Alisema kama ambavyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alizungumza awali, anatambua kuwa watendaji wengi serikalini wanafanya kazi vyema  hivyo wanawajibu wa kuendelea ili kupata matokeo mazuri zaidi.

Aliwapongeza Spika na Jaji Mkuu namna Bunge na Mahakama zinavyofanya kazi ambako alisema mihimili hiyo miwili inaisaidia Serikali.

Alisema viongozi walioteuliwa kazi yao ni nzito na kubwa hususani suala linalohusu watumishi wa umma.

Alisema Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Steven Mbwana pamoja na makamishna ni wale ambao walifanya kazi ya utumishi na wamepambana na mambo mbalimbali.

“Yambesi (George Yambesi –Kamishna Tume ya Utumishi wa Umma) amekuwa Katibu Mkuu wa Utumishi leo (jana) ndio Kamshna wa kuwasemea. Kila mmoja ana uzoefu wake. Naamini mtatekeleza wajibu wenu katika kulinda maslahi ya watumishi lakini kulinda pia maslahi ya Serikali. Ili Serikali isionewe na watumishi wasionewe,” alisema Rais Magufuli,. 

Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majali ambaye naye alikuwapo wakati wa kuapishwa viongozi hao baada ya kusafiri kwa siku tisa katika mikoa ya Dodoma, Ruvuma, Lindi pamoja na Mjini Magharibi- Zanzibar alisema huko alipewa salamu kufikisha kwa Rais Magufuli.

Alisema Dk. Ali Mohamed Shein  pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walimtuma afikishe salamu zao kwake za mwaka mpya.

 “Tulikuwa jana (juzi) kwenye wiki mbili za sherehe za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambazo zinatumika kuweka mawe ya msingi, kuzindua miradi mbalimbali ikiwa ni mwelekeo wa Januari 12, ya mapinduzi ya Zanzibar. 

Alisema viongozi walioapishwa ni dalili kuwa Rais anawaamini kuwa wataungana na watendaji wenzao ndani ya Serikali kwenye nafasi hizo mpya walizoteuliwa ili kuendeleza jukumu la maendeleo.

“Serikali ya awamua ya Tano ambayo inatekeleza Ilani ya CCM kwa miaka mitano, tumeshakamilisha miaka mitatu , sasa tuna miaka miwili, uteuzi wenu ni ishara tosha kuwa Rais ana imani kubwa kuwa mtaongeza nguvu ndani ya Serikali ili kuhakikisha tunafikia malengo yaliyowekwa na Ilani ya CCM kufikia 2020,” alisema.

 Alisema shughuli za maendeleo zinaendelea na watendaji wa Serikali wako tayari kuyapokea na kutekeleza yale aliyoyaahidi.

Akizungumza awali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alisema pamoja na kuwapongeza walioapishwa lakini hafla hiyo ilikumbusha viongozi wote viapo vyao walivyoapa pamoja na kujua majukumu yao.

Aliwaasa viongozi hao kuwa pamoja na kutumia sherioa lakini hawana budi kuangalia dunia inayowazunguka kwa kuwa inakwenda kasi.

“Ninyi ni viongozi na kazi kubwa ya kiongozi ni kututoa sisi wananchi ambao tunawategemea tulipo na kutufikisha sehemu ambayo tunatarajia.

“Pamoja na kutumia sheria na Katiba, hamna budi kuangalia dunia inayotuzunguka kwa sababu tunashindana na dunia inayoenda kasi.

“Tumewapa dhamana ya kuhakikisha kwamba tutakuwa katika hali bora zaidi kuliko wale ambao wanatuzunguka. Nawahakikishia muhimili wa mahakama utaendelea kutoa ushirikiano kwa mujibu wa sheria,” alisema Jaji Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles