23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya Mengi kutoka ufukara hadi bilionea

Mwandishi Wetu –Dar es Salaam

DK. Reginald Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro mwaka 1944, akiwa ni mmoja wa watoto saba wa Abraham Mengi na Ndeekyo Mengi.

Alianza safari yake kielimu katika Shule ya Msingi Kisereny Village Bush, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School na baadaye Sekondari ya Old Moshi.

Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU), Dk. Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.

Dk. Mengi ni mmoja kati ya Watanzania wa mwanzo kusoma nchini humo na kufanikiwa kuwa mhasibu anayetambulika na Taasisi ya Wahasibu ya Uingereza na Wales.

Baada ya kumaliza masomo ughaibuni, alirudi nchini mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania (sasa Prince Water House Cooper) hadi mwaka 1989 alipoamua kujikita katika ujasiriamali.

Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited na baadae kufahamika zaidi kama IPP Limited.

Kupitia IPP Limited alianzisha kampuni mbalimbali na kufanya biashara kadhaa kuanzia uzalishaji wa sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio.

Kituo chake cha runinga – ITV pamoja na kituo cha redio – Redio One ni moja ya vituo vikubwa vya utangazaji huku magazeti yake ya Guardian na Nipashe yakiwa miongoni mwa magazeti makubwa nchini.

Hadi umauti unamfika, Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Mwaka 2014, jarida la Fobes lilimuorodhesha MOAT Mengi akiwa nafasi ya 45 kati ya matajiri 50 zaidi barani Afrika, akiwa na utajiri wa Dola za Marekani milioni 560 sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.2.

Wakati wa uhai wake, pia alipewa tuzo mbalimbali kitaifa, kikanda na kimataifa akitambulika zaidi kwa kazi yake ya kujitolea kwa watu.

Alipewa tuzo ya ‘The Order of the United Republic of Tanzania’ mwaka 1994 na ‘The Order of The Arusha Declaration of the First Class’ zilizotolewa na Serikali mwaka 1995.

Aidha alipewa tuzo ya ‘The Martin Luther King Jr. Drum Major for Justice’ iliyotolewa na Marekani mwaka 2008.

Tuzo zingine ni ‘The International Order of the Lions Club’ iliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa ya Lions Club mwaka 2014 na ‘The 2012 Business For Peace Award’ iliyotolewa na Taasisi ya Business for Peace Foundation ya Oslo, Sweden baada ya kupendekezwa na kamati inayotoa tuzo za Nobel.

Kwa kutambua juhudi zake za kupambana na rushwa na ufisadi nchini mwaka 2008, Serikali ya Marekani ilimpatia tuzo ya ‘Martin Luther King Jr. Drum Major Award’.

Mwaka 2014 Rais Jakaya Kikwete alimpa Dk. Mengi tuzo ya taifa katika mambo ya kuisaida na kuiwezesha jamii, hasa katika ujasiriamali wa kijamii – ‘The National Philanthropy Award’ katika sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

URITHI WA KITABU

“Nimezaliwa katika umasikini wa kutupwa, lakini jambo hilo hata siku moja halikunikatisha tamaa,” ni moja ya kauli ambazo Mengi alikuwa hachoki kuzisema kila alipopata wasaa wa kuzungumzia alipotokea.

Mwaka 2018 Dk. Mengi alichapisha kitabu cha maisha yake kiitwachoI can, I must, I will’ (Ninaweza, Lazima nifanye, Nitafanikisha) kinachoangazia historia ya maisha yake toka alipozaliwa hadi kufanikiwa kibiashara.

Akiwa mmoja wa watoto saba wa mzee Abraham na mkewe Ndeekyo, katika kitabu hicho ameeleza wasifu wake, ikiwamo safari yake ya maisha ya dhiki akiwa mtoto hadi kuwa msomi mkubwa fani ya uhasibu na kisha tajiri wa kupigiwa mfano.

Anaelezea maisha ya kubangaiza waliyokuwa wakiishi wazazi wake katika vibanda vya udongo katika Kijiji cha Nkuu kilichopo Machame mkoani Kilimanjaro.

 “Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki si zaidi ya ekari moja, tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe wachache na kuku.

“Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma, ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile.”

Hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Mengi ambaye ugumu wa maisha tangu utotoni ndio uliomsukuma kaka yake Elitira kuanza kufanya biashara ya kuuza mayai wakati huo akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mbinu za Elitira katika ujasiriamali zikamvutia mdogo wake, ambaye katika kitabu anasema zilimvutia sana.  Anasema Elitira alipewa kipawa cha kugundua fursa na kuzigeuza kuwa biashara.

Baadaye Mengi naye alianza kujenga himaya ya biashara baada ya kugundua kuwapo kwa uhaba wa kalamu za wino ambazo miaka ya 1983 ilikuwa ni bidhaa iliyoagizwa kutoka nje.

Huo ulikuwa mwanzo wa kuingia katika ulimwengu wa biashara akianza na utengenezaji wa kalamu alizozipa jina la ‘Epica’. 

Anasema alianza biashara hiyo kwa kuagiza vifaa kutoka Mombasa akiwa hana senti mfukoni bali kwa makubaliano ya kulipa baada ya mauzo.

Kutoka kukusanya vifaa vya kutengeneza kalamu, Mengi alizidi kutanua wigo wa biashara kadiri siku zilivyokwenda.

Hadi anaaga dunia, Mengi anatajwa kama mmoja wa matajiri wakubwa nchini na ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na himaya ya biashara ya vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.

Mwishoni mwa mwaka jana Mengi alifiwa na aliyekuwa mke wake wa kwanza, Mercy Mengi.

Ameacha mjane Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wanne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles