23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Muungano wetu na kumbukizi ya Taifa la China kutimiza miaka 55

Na Judith Mhina-MAELEZO

MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar ambao sasa unatimiza miaka 55 na ndio chanzo cha ushirikiano wa kiplomasia na Jamhuri ya Watu wa China chini ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Shekhe Abeid Amani Karume kwa kushirikiana na  Mwenyekiti Mao Ze Dong  na Waziri Mkuu  Chou en Lai wa China ambao sasa unatimiza miaka 55.

Alama ya Tanzania kwa Taifa la Watu wa China ilisimikwa na  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, rais wa kwanza wa Tanzania aliposhauri  na kupigania Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China (The People Republic of China) kujiunga na Umoja wa Mataifa (UN).

Tanzania iliyopambana na Marekani  mwaka 1973 kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Rais wa Marekani wakati huo, George W Bush, alipokuwa Balozi wa Marekani  katika Umoja wa Mataifa na Dk. Salim Ahmed Salim ambaye alikuwa  mwakilishi  wa kudumu wa Tanzania katika umoja huo.

Mwana diplomasia huyo aliwezesha nchi ya China kuchukua kiti chake halali cha UN ambacho kilikaliwa isivyo halali na Taiwan, Taifa ambalo lilikuwa jimbo lililoasi la China kutoka Chama cha Kikomunisti cha China na kujiita  Kuomitang chini ya Kibaraka Kai Shekh kuanzia 1947.

Wakati wa kampeni hizo, ujumbe wa Tanzania ukiongozwa    na  Chifu Patrick Kunambi, ulihakikisha China inaingizwa UN na kuigaragaza Marekani ambayo ilianza kununua kura za wajumbe kwa kutoa rushwa  waziwazi kwa fedha ambazo Bush alisema anatoa papo  kwa papo. Njama hizo hazikufua dafu kwa diplomasia ya Tanzania, mwishowe China iliingia UN kwa kishindo.

Tanzania ikiwa na mtaji wa nchi zisizofungamana na upande wowote-Non Aligned Countries zilishinda kwa umoja na uwingi wao, kwani Baraza Kuu kura  za turufu-Veto hazitumiki.  

Hii ilikuwa faraja sana kwa China ambayo ilianza kukata tamaa wakati ule wa vita baridi, ambapo pamoja kuwa mwanachama mwanzilishi, aliwekewa vikwazo  na Marekani  kwa kuwa  aliunga  mkono Taiwan.

Nyakati hizo historia inatuambia siasa za ulimwengu zilikuwa makundi mawili ya Magharibi ikiongozwa na Marekani, Mashariki ikiongozwa  na Urusi na hivyo kuanzisha uhasama ambao Marekani alilipiza kwa kura ya Veto mara mbili pale Balozi  Dk. Salim  Ahmed alipowania Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kukataliwa na Marekani.

Wakati wa kuingiza China UN  Marekani kwa kutamba kwake,  ikaanzisha  na kuzusha  msemo wa ‘banana republics’ wa George Bush akiamaanisha nchi ndogondogo  zenye uchumi dhaifu ambapo kwa kauli kamili ilikuwa: “The United States cannot be humiliated by the banana republics  that it can buy its votes,”.  Lakini ikashindwa vibaya pamoja na kumwaga fedha nyingi kwani siku zote palipo na ukweli  uongo hujitenga na  ukweli siku zote hushinda.

Kwa kuzingatia hayo, China na Tanzania ni marafiki wa damu hivyo hufaana kwa dhiki na faraja.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere mwana falsafa na mbobezi katika masuala mbalimbali duniani ikiwemo historia, alitambua mapema kasoro iliyokuwepo ya  Taifa la Watu wa China kuwakilishwa katika Umoja wa Mataifa  na taifa dogo  la kisiwa cha  Taiwan. Hii ilitokana na Jamhuri ya Watu wa China Bara ilikuwa na jumla ya watu milioni 800 na kisiwa cha Taiwan ambacho kilikuwa kinawakilisha China katika Umoja wa Mataifa kikiwa na jumla ya watu milioni 18.

Kutokana na Muungano wetu kuwa na watu mahiri na wanadiplomasia wabobezi, Mwalimu alimwagiza Balozi wetu wakati huo, UN Dk. Salim Ahmed Salim kuwa ahakikishe China inaingia na kuwa mwanachama wa umoja huo, historia hii imeandikwa mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Dk. Salim Ahmed Salim alitoa pendekezo  hilo  UN na kuwauliza kwanini Taiwan ikiwa na idadi ndogo ya watu inaiwakilisha China Mainland kwenye Umoja huo badala ya China Mainland kuiwakilisha Taiwan yenye idadi ndogo ya watu na eneo dogo la kijiografia.

UN ikachukua hatua stahiki kwa kukaa kikao na kujadili mapendekezo hayo ya Serikali ya Tanzania juu ya Jamhuri ya Watu wa China kuwa miongoni mwa nchi wawakilishi katika Umoja huo na takribani nchi 33 zilipiga kura ili kumpata mwakilishi halali kati ya Bara la China na Kisiwa cha Taiwan, matokeo yake Bara la China ilishinda hapo ndipo ilipoanza kujulikana kimataifa.

Akihojiwa kwa nyakati tofauti na Idara ya Habari Maelezo, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Wang Ke, anasema undugu wa watu wa China na Tanzania ni wa damu  na ni wa muda mrefu.

Kwa Tanzania nchi ya China ni wenzetu na historia inajieleza ambapo katika miaka ya 1960, nchi nyingi za Bara la Afrika zilikuwa katika vuguvugu la kutafuta uhuru, Tanzania ikiwemo. Wakati huo China ilikuwa katika vita baridi na Marekani na kiuchumi ilikuwa ni nchi masikini.

Hata hivyo, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, walikwenda nchi za Magharibi kusema kwamba wahahitaji reli kati ya Tanzania na Zambia kwa sababu reli zilizokuwepo Afrika ya Kusini, Zimbabwe na Msumbiji zilikuwa zikiendeshwa kwa ubaguzi, nchi za magharibi hazikukubali ombi hilo. Lakini walipokwenda China kuomba msaada huo wa ujenzi, waliambiwa reli hiyo itajengwa kwa ushirikiano.

Wachina wakashiriki katika ukombozi wa  Afrika-Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo walijenga Reli ya TAZARA inayojulikana kama Reli ya Uhuru. Mwenyekiti Mao Ze Dong  na Waziri Mkuu, Chou en Lai wa China walikuwa marafiki wa Mwalimu Nyerere na urafiki huo umedumishwa hadi leo.

China imeimarika na kuwa mshirika mkubwa wa Afrika kiuchumi. Fedha zinazotoka China kuelekea Afrika zimekuwa zikiongezeka tofauti na zamani. China imekuwa ikitoa misaada na kuwa mfadhili mkuu katika kutekeleza miradi mingi na miundombinu ambayo inashuhudiwa barani Afrika na Tanzania kwa ujumla katika miaka ya hivi karibuni. Hakuna nchi inayoweza kulingana na kiwango chake cha ushirika.

Kutokana   na hilo, biashara imeinuka kwa asilimia 20kila mwaka katika kipindi chamwongo mmoja uliopita.  Zipo kampuni nyingi za China zinazofanya kazi barani Afrika, hiyo ikiwa ni mara nne zaidi ya makadirio ya awali. Inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya kampuni hizo ni zile za binafsi katika sekta tofauti huku theluthi moja zikijikita katika viwanda.

Kampuni hizo zinachangia kwa mitaji ya uwekezaji, maendeleo ya usimamizi na ujasiriamali katika sekta mbalimbali barani Afrika. Kwa kufanya hivyo, zinasaidia kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika.  

“Tunaamini kuna nafasi ya kuendelea zaidi.

Mbali na viwanda, robo ya kampuni za China zimejikita katika utoaji huduma kwenye biashara na ujenzi. Tayari asilimia 12 za mapato ya viwanda vya Afrika hutokana na kampuni za China, hiyo ikikadiriwa kuwa ni jumla ya dola bilioni 500 kwa mwaka.

China imechukua asilimia 50 ya soko la Afrika kuhusu uhandisi, ununuzi na ujenzi. Kampuni za China zinapata faida nzuri na kurejesha fedha zao za mtaji kwa muda wa mwaka mmoja au chini ya muda huo. Kampuni hizo zinalenga zaidi matakwa ya masoko ya Afrika yanayokuwa kwa kasi kuliko kulenga kwenye bidhaa za kuuza au kusafirisha nje ya Afrika. Uwekezaji wao unaashiria ushirikiano wa kudumu kwa Afrika. Kampuni za China zina matumaini ya mustakabali mzuri wa Afrika.

Uwekezaji na biashara barani Afrika unaofanywa na China uneleta faida kuu za kiuchumi kama vile kubuni nafasi za ajira na taaluma, kubadilishana ujuzi na teknolojia na pia ni ufadhili na maendeleo ya miundombinu.

Imani na alama aliyoiweka Mwalimu Nyerere na shujaa wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano, ndio inayotufanya tutembee kifua mbele na kuthaminiwa kwa kiasi kikubwa  na Jamhuri ya Watu wa China ambao Aprili 26, mwaka huu ya kumbukizi ya  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wao wanaadhimisha siku ya kumbukumbu ya Ushirikiano wa Kidiplomasia  wa Tanzania na China kutimiza miaka 55.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles