VERONICA ROMWALD
UTAMADUNI wa familia, ndugu, jamaa na marafiki kukaa mezani na kula chakula pamoja kilichopakuliwa katika chombo kimoja (sinia na bakuli), ni jambo la kawaida kwa miaka mingi.
Ni kweli bado utamaduni huo upo kwenye jamii lakini si kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa zamani.
Watu tulizunguka meza tukila chakula pamoja kwa furaha, kila mmoja alishukuru na kunyanyuka baada ya kuridhika kwamba ametosheka.
Lakini hali haikuwa hivyo katika familia ya Ahmad Salum (85), Mkazi wa Kijiji cha Kigugu, Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro.
Salum hakuwa na furaha kila alipoketi na ndugu zake kula pamoja mezani, hali hiyo ni kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimkabili.
“Ndugu zangu tuliozaliwa tumbo la mama, baba mmoja walikuwa wananiogopa kwa hali niliyokuwa nayo wakati huo, tulipokaa mezani kula chakula, tulikuwa tunapakuliwa kwenye chombo kimoja.
“Kwa mfano kama tunakula ugali, tunaizunguka ile meza, mwanzo tunakula kwa amani kabisa, lakini wakifika mahala wanaona wamekaribia kufika pale ninapokula mimi, kila mmoja unaona kanyanyuka na kusema ameshiba.
“Lakini kwa sababu mimi nilikuwa mkubwa zaidi kwao, nilielewa wazi walikuwa wananiogopa kunigusa wakihofia kwamba nitawaambukiza.
“Baba yangu alikuwa ana akili, akamweleza mama suala lile, wakakubaliana niwe natengewa chakula changu peke yangu.
“Nikawa sikai tena mezani na ndugu zangu kula pamoja, japo hilo lilikusudia kuepusha wasiniogope kuwaambikiza lakini nilikuwa najisikia huzuni mno,”anabainisha.
Anasema bado haikuwa imejulikana kinachomsumbua, alikuwa hajapelekwa hospitalini kwa uchunguzi kwani baba yake hakuwa na fedha za kutosha.
“Niliendelea kukaa nyumbani, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi ya awali, baba aliendelea kujitahidi kutafuta fedha kwa ajili yangu,” anasema.
SAFARI YA MATIBABU
“Niliendelea kuugulia maumivu makali, nakumbuka Juni, 1969…mguu wangu wa kushoto ulipoanza kuuma kwenye kidole gumba.
“Kilivimba mno hadi ikafika hatua uvimbe ule ukapasuka, macho nayo yalikuwa yanawasha kama vile yamepakwa pilipili hasa jicho la kulia.
“Nashukuru baba alikuwa amepata fedha kiasi, tukasafiri kuja huku Kijiji cha Chazi kwa uchunguzi, wakati ule tulimkuta daktari wa kigeni (mzungu), alinipokea kwa upendo, nikaanza matibabu.
“Ikaonekana kwamba kidole changu kilikuwa kimeathirika mno, hivyo kikatwe kama sehemu ya matibabu, nilikubali, baada ya matibabu hali yangu ilipoimarika niliruhusiwa kurudi nyumbani,” anasema.
Anasema hata hivyo ilipofika 1970 alianza kuhisi tena maumivu katika eneo lile (kidole gumba kilichokatwa).
“Macho nayo yalizidi kuuma, ikabidi nirudishwe tena hospitalini, nakumbuka ilikuwa 1975, nikakuta kuna daktari mwingine mzungu, yule aliyenitibu mwanzo alikuwa amerejea kwao.
“Nilifanyiwa vipimo na akanieleza amebaini mguu wangu nao ulipaswa kukatwa kulingana na jinsi kidonda kilivyokuwa, sikuwa na jinsi, ilibidi nikubaliane na matokeo hayo.
“Wazee wangu waliniombea dua, nikakatwa mguu wangu, baada ya matibabu, 1980 walitufanyia utaratibu na wenzangu kadhaa, tukasafirishwa hadi mkoani Tabora, huko tulikwenda kutengenezewa miguu ya bandia.
“Tulikwenda Hospitali ya Kitete, wenyeji wetu walitupokea vizuri, kulikuwa na wauguzi walitupokea vizuri mno, kwa kweli tulienda kishujaa, tulisafiri hadi huko na basi lilikuwa linaitwa ‘Sebene bus’.
“Tulijiona wenye bahati kubwa, baada ya kutengenezewa miguu yetu bandia, tulikuwa tumepatiwa usafiri wa kuturudisha kambini Chazi,”anasimulia.
MAISHA YA NDOA
“Nimejaliwa kupata watoto wanne kwa mke wangu wa kwanza ambaye nilikuwa naishi naye kule Kijijini Kigugu, lakini niliomba kuachana naye kutokana na maradhi haya.
“Kabla sijaanza matibabu, nilimshauri mke wangu tuachane kwa sababu, sikujua nitarejea lini kutoka Chazi, sikujua kwa hali niliyokuwa nayo matibabu yangu yangekamilika lini ili niweze kurudi nyumbani.
“Niliona angeteseka bure kunisubiri, alikubali, nikampa talaka yake, nilipoondoka huko nyuma aliolewa na mwanamume mwingine na walibahatika kupata watoto wengine.
“Jambo ambalo nashukuru yule mwanamume aliishi vizuri na wanangu, hivi sasa wote ni marehemu, nawaomba kheri huko walipo, Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi,”anasema.
SIMANZI
Anasema baada ya miaka mitano tangu alipopatiwa mguu ule wa bandia, ulianza kuchoka hatimaye ukaisha kabisa, haukufaa kwa matumizi.
“Mambo yalianza kuwa magumu kwangu, sikuwa tena na mguu mwingine wa kuniwezesha kutembea,”anasimulia.
Anasema alielekezwa kuwa kuna mtu ambaye angeweza kumsaidia kupata mguu mwingine.
“Jamaa huyo kweli alijitolea kunisaidia, alinitengenezea mguu wa bandia kwa kutumia mti (akimuonesha mwandishi), ni zaidi ya miaka kumi sasa nimekuwa nikiutumia.
“Kwa kweli ni mzito mno kuliko ule niliotengenezewa Tabora, lakini umenisaidia kwani nimeweza kuutumia kutembea kwenda popote ninapotaka kama binadamu wengine wasio na ulemavu.
“Naishi vizuri tu, naenda sokoni, mimi ni mkulima nina hekari tatu, kwa kutumia mguu huu, huwa nakwenda shambani kwangu kukagua mazao.
“Kweli siwezi kulima, huwa nalimisha, navuna, nauza napata fedha zangu za kujikimu, baba yangu ndiye ambaye aliniambia ‘nipige jembe’.
“Aliniambia haya maisha, watu wanaopiga jembe ndiyo wanapendwa na kila mtu, alinitaka niwe mkulima ikiwa nataka kuishi maisha mazuri hapa duniani,”anasema.
Anasimulia; “Naishi maisha ya kawaida, nina furaha na amani tele, ila huwa najisikia unyonge pale mtu anaponisimanga juu ya hali yangu.
“Kwa mfano nikiwa hapa kambini, nilipata mwanamke nikakubaliana kuishi naye, lakini niliona mwenzangu hatuelewani, nikampa talaka yake.
“Nikabaki naishi kwa amani na furaha kama unavyoniona, Nashukuru Mungu wanangu sasa wamekua huwa wanakuja pia kuniona hapa kambini, wananisaidia pia.
FARAJA MPYA
Mzee Salum ni miongoni mwa waathirika wa ukoma ambao hivi karibuni walikabidhiwa miguu ya bandia na Shirika lisilo la Kiserikali la nchini Ujemarumani, linashughulika na mapambano dhidi ya kifua kikuu na ukoma (GLRA).
Shirika hilo linashirikiana kwa ukaribu na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) ambao upo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kukabili magonjwa hayo nchini.
Mtaalamu wa Viungo Sanifu Bandia NTLP, Paul Shunda anasema waliona vema kumpatia mguu mwingine Salum kwani aliokuwa akiutumia ulikuwa mzito mno.
“Kwa kitaalamu huwa hairuhusiwi kumpatia mguu wa bandia mtu aliyevuka zaidi ya miaka 60, kwa sababu uwezo wake wa kuona huwa umepungua pia.
“Lakini kwa hali ya mzee huyu na kwa kuzingatia kwamba tayari ana uzoefu wa kutembelea mguu wa aina hii na kwa kuwa mguu aliotengenezewa (wa mti) ulikuwa mzito kiasi cha karibu kilo tatu.
“Tuliona vema kumtengenezea mguu huu tuliompatia, tunaamini utamsaidia zaidi kuliko ule wa mti aliokuwa akiutumia,”anasema.
Mzee huyo anashukuru GLRA na NTLP kumpatia mguu huo mpya kwani anaona ni sawa na wamemtua mzigo uliokuwa umemuelemea.
“Hakika ni mwepesi kuliko ule wa mti, siku zote siwezi kuacha kumshukuru Mungu, wazazi na walezi wangu hawa wanaonitunza hapa kambini.
“Siwezi pia kuacha kumshukuru jamaa yule ambaye alinitengenezea mguu huu wa mti kwani umenisaidia mno katika maisha yangu,” anasema.
Anaongeza “Lakini bado ni muhimu elimu kuhusu ugonjwa huu kuendelea kutolewa kwa jamii, hasa vijijini wengi hawajui, kusema ukweli ni vigumu mno kuishi kijijini na hali kama yangu.
“Huku watu wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu tatizo, ndiyo maana wanaishia kututenga, kutunyanyapaa, wakielimika nina uhakika watabadilika na kuacha,”anashauri.
ZAIDI YA 2,000 WANUFAIKA
Mwakilishi wa GLRA-Tanzania, Buchard Rwamtoga anasema kwa mara ya kwanza lilipata usajili 1977 na kuanza kushirikiana na NTLP kupambana dhidi ya TB na Ukoma.
Anasema tangu kipindi hicho shirika hilo kwa kushirikiana na NTLP wamewezesha watu wenye ulemavu utokanao na ukoma kupatiwa huduma za marekebisho ya kiafya ikiwa ni pamoja na kupewa nyenzo za kijimudu.
“Watu 1,650 wamefanyiwa upasuaji, 450 wamepewa miguu bandia, 500 magongo na viti-mwendo 55, tumewapatia viatu maalumu pea 94,500 vyenye gharama ya Sh milioni 897.75 ambavyo vimetolewa kwa waathirika wa ukoma 47,250 ili kuzuia wasipate ulemavu zaidi,” anabainisha.
Anasema sambamba na hilo wamekabidhi magari 270 yenye gharama ya Sh bilioni 9.4 kwa waratibu wa TB na Ukoma kwa mikoa ya Bara na visiwani, pikipiki 675 zenye gharama ya Sh bilioni 2.77 kwa waratibu wa wilaya, vipuli vya magari na pikipiki.
“Tumewezesha mafunzo kwa watumishi wa afya 750 na maofisa ustawi 12, ya kuzuia ulemavu utokanao na ukoma na marekebisho kwa watu wenye ulemavu.
“Tumeweza uanzishwaji na usajili wa vikundi 50 vya ujasiriamali vya walemavu wa ukoma vyenye wanachama 677 na kuvisajili kama asasi za kijamii na tumefadhili watoto wao 3,765 kupata elimu,”anabainisha.
Rwamtoga anasema pamoja na hayo wamejenga shule nne katika kijiji cha Nandanga (Ruangwa), Makundechi (Pemba), Nyabange (Musoma) na Mkaseka (Masasi) ili kuwezesha watoto wa familia za waathirika wa ukoma kupata haki ya elimu ya awali.
“Tumeweza kuzijengea nyumba bora familia 120 zenye walemavu 739 hivyo kuweza kuwachangamanisha na wanajamii wengine,” anabainisha.