ZURICH, USWISI
BARAZA la Umoja wa Ulaya kuhusu uhuru wa vyombo vya habari limeripoti kuwa mwaka 2018 ulikuwa mbaya zaidi kwa waandishi wa habari barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita baridi.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2019 ya baraza hilo iliyopewa kichwa cha habari ‘Demokrasia hatarini’, uhuru wa vyombo vya habari katika nchi wanachama uko katika hali mbaya tangu kumalizika kwa vita baridi.
Ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano na Jukwaa la Ulinzi na Usalama wa Waandishi wa Habari, inasema mashambulizi dhidi ya wanataaluma wa habari yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka michache iliyopita.
Katika ripoti hiyo inaelezwa kuwa waandishi wa habari wawili waliuawa mwaka 2018 kuhusiana na kazi zao, akiwemo Jan Kuciak wa Slovakia na Jamal Khashoggi ambaye kifo chake katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul bado kinachunguzwa.
Jukwaa hilo lilidaia kuwa mbali na vifo hivyo, lilipokea taarifa za mashambulizi mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na mabomu ya kwenye magari, shambulio la visu, uchomaji wa mali na uvamizi wa ofisi za magazeti.
Lakini mashambulizi hayo si tu yalikuwa ya kimwili, bali ripoti inaeleza kuwa mwaka 2018 ulionekana kuelekea zaidi kwenye mashambulizi ya maneno na unyanyapaa wa umma dhidi ya vyombo vya habari na waandishi habari binafsi katika nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
“Mfano wa mashambulizi hayo ni kauli zilizotolewa na viongozi wa siasa zikiwemo za wale waliosema wanasikitika kwamba bado waandishi wa habari hawajatoweka kabisa duniani na hata kutoa orodha ya wandishi wa habari ambao walidiriki kukosoa Serikali na kuwaita wasaliti,” ilieleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waandishi wa habari 130 bado walikuwa kizuizini hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, wengi nchini Uturuki ambayo imesalia kuwa taifa lenye idadi kubwa duniani lenye waandishi wa habari walioko gerezani, ambako zaidi ya waandishi 200 walikamatwa tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi mwaka 2016.
Aidha, ripoti hiyo imekosoa utamaduni wa kushindwa kwa mamlaka za Serikali katika kuwatambua, kuwashtaki na kuwaadhibu wale wote wanaohusika na uhalifu wa vurugu dhidi ya waandishi.
Ilieleza kuwa nchi 47 wanachama wa baraza hilo waliahidi kuchukua hatua za kukomesha kinga mwaka 2016, lakini hakuna hatua iliyopigwa. Ripoti inapendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya mashambulizi hayo.