28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Hekima ya matumizi ilivyonufaisha jamii ya Norway

*JOSEPH HIZA

NCHI ya Norway inajivunia kuwa na Mfuko mkubwa zaidi duniani wa Utajiri wa Dola au Sovereign Wealth Funds (SWF), shukrani zikiendea miaka mingi ya ukubwa wa bei ya mafuta na gesi katika soko la dunia.

Kutuna kwa mfuko wake huo, kiasi cha kuziacha mbali nchi nyingi zenye mifuko kama hiyo duniani, kumewafanya Wanorway wote nchini humo kuwa mamilionea.

Kutokana na kuhakikiwa ustawi wa maisha katika kila nyanja, kwa miongo kadhaa sasa, Wanorway ni miongoni mwa jamii zenye viwango vya juu vya ustawi wa kijamii duniani.

Na kwa sababu hiyo ni miongoni mwa jamii zenye viwango vya juu vya furaha zaidi duniani.

Taifa hilo la Nordic limethibitisha kuwa na usimamizi wa fedha wa kipekee, ikizitumia kwa hekima kipindi ambacho mataifa mengine yanahaha kujinasua kutoka mlima wa madeni.

Nchi nyingi duniani zikiwamo za Afrika zimeanzisha SWF kwa ajili ya uwekezaji unaotokana na sekta zinazohusiana na mapato kutokana na rasilimali zilizobarikiwa katika ardhi zao kwa manufaa na maendeleo ya mataifa husika.

Kwa maneno mengine SWF ni mifuko ya uwekezaji inayomilikiwa na serikali za mataifa husika kwa minajiri ya kuwekeza katika mali halisi au fedha kama vile hisa, dhamana za serikali, mali zisizohamishika, madini ili kunufaisha jamii zao.

Hali kadhalika inaweza kuwa katika uwekezaji mbadala kama vile mfuko wa mitaji binafsi na au mfuko wa akiba kwa ajili ya sekta ya nishati. Mara nyingi zaidi uwekezaji wa SWF huvuka mipaka kwa maana ya kwenda kuwekeza katika nchi nyingine.

Lengo la kufanya hivyo ni kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza nyumbani ikiwamo mfumuko wa bei au kushuka kwa uchumi iwapo uwekezaji utajikita ndani tu.

Sehemu kubwa ya SWF huendeshwa na mapato kutokana na mauzo ya bidhaa nje au kutoka akiba ya fedha za kigeni zilizopo Benki Kuu.

Wakati mwingine SWF huweza kudhibitiwa na benki kuu ambayo inakusanya fedha wakati ikisimamia mfumo wa kibenki wa serikali kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na mtiririko wa fedha kwa mwaka.

SWF ya Norway ukiwa umeanzishwa mwaka 1990, unamiliki karibu asilimia moja ya soko la hisa duniani, pamoja na dhamana za serikali na mali zisizohamishika zilizotapakaa kuanzia London, Uingereza hadi Boston nchini Marekani.

Norway inatengeneza fedha kwa ajili ya mfuko huo kutokana na kodi zinazotokana na mafuta na gesi, umiliki wa visima vya mafuta na mgao kutoka asilimia 67 ya hisa katika kampuni kubwa kabisa ya nishati ya nchi hiyo, Statoil ASA (STL).

Mapato ya ziada hukusanywa na Mfuko wa Kimataifa wa Akiba wa Serikali.

Kwa mujibu wa takwimu za awali katika tovuti ya benki kuu, ambayo inasimamia mfuko huo, ulifikisha kroner trilioni 5.11 sawa na dola bilioni 828.66.

Hiyo inakokotolewa zaidi ya mara milioni moja ya takwimu rasmi za idadi ya watu nchini Norway, ambayo inasimama katika watu 5,096,300.

Kiwango hicho ni sawa na pauni 100,000 za Uingereza au Sh milioni 250 za Tanzania kwa kila Mnorway.

Imekuwa mara ya kwanza kwa mtu mmoja nchini humo kumiliki kroner milioni moja, msemaji wa Benki Kuu ya Norway, Thomas Sevang alisema.

Hata hivyo, haina maana Wanorway watagawiwa fedha hizo au kuzitumia bali zitahifadhiwa kwa manufaa yao ya baadaye na kwa vizazi vijavyo.

Norway imefanikiwa kukabiliana na changamoto zinazotokana na ugunduzi wa nishati ya mafuta tangu mwaka 1969 katika Bahari ya Kaskazini.

Waziri wa Fedha, Siv Jensen aliliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba mfuko huo uitwao Mfuko wa Akiba wa Serikali, umesaidia kukabiliana na changamoto zisizotabirika za bei ya mafuta na gesi.

Norway ni muuzaji namba saba wa mafuta duniani.

‘Nchi nyingi zimeanzisha mapato ya muda kutokana na rasilimali zilizopo kutengeneza ustawi unaokaa kwa muda mfupi, ambao hufuatiwa na vipindi vigumu, anasema.

Mfuko huo ambao ni sawa  na asilimia 183 ya pato la taifa la Norway (GDP) la mwaka 2013, unatarajia kufikisha asilimia 220 mwaka 2030.

‘Mfuko umefanikiwa kutokana na ukweli kwamba Bunge limeweza kutenga fedha kwa ajili ya wakati ujao. Kuna mifano mingi ya nchi ambazo hazijaweza kufikia lengo kama hili, alisema Oeystein Doerum, mchumi mkuu katika masoko ya Benki ya Uwekezaji ya Norway (DNB).

Norway ilikuwa imechukua tahadhari ya kuepuka makosa ya baadhi ya nchi ambazo hushuhudia kipindi cha neema kabla ya kuvurugika kutokeapo matatizo ya kiuchumi  kwa kuwekeza nje ya nchi badala ya nyumbani.

Serikali huweza kutumia asilimia nne ya mfuko huo kila mwaka nchini humo, ikiwa ni zaidi kidogo ya mapato ya mwaka ya uwekezaji.

Pamoja na utajiri wake wa mafuta, Norway imesita kufanya mageuzi au kupunguza ruzuku zisizoweza kufikiriwa popote pale duniani.

Miongoni mwa ruzuku zinazotolewa ni pamoja na ile kwa ajili ya sekta ya uzalishaji maziwa, ambapo hulenga kusaidia kuwaweka katika hali ya joto ng’ombe wa maziwa katika eneo hilo lenye baridi kali la Aktiki.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaonya kwamba ustawi unaoshuhudiwa kiasi cha kuwadekeza wananchi, unaweza kuwafanya Wanorway wasite kufanya kazi.

‘Mmoja kati ya watu watano mwenye umri wa kufanya kazi nchini humo hupokea aina fulani ya bima ya jamii badala ya kufanya kazi,’ Doerum alisema pamoja na kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kinasimama katika asilimia 3.3.

Lakini pia pamoja na neema hiyo maisha ya Norway bado ni ghali mno.

Mjini Oslo, ambako glasi ya bia inauzwa kwa pauni tano sawa na Sh 12,500 ni ghali zaidi duniani kwa mujibu wa jarida la uchumi, The Economist.

Aidha chakula cha usiku kwa watu wawili katika migahawa ya wastani kwa bei ya chini ni pauni 200 za Uingereza sawa na Sh 500,000.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles