28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Kisena wa Mwendokasi aenda gerezani

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM    

MKURUGENZI wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo  Haraka Dar es Salaam (UDART), Rober Kisena na wenzake watatu wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka 19 yakiwamo ya kutakatisha zaidi ya Sh bilioni mbili, kuiba zaidi ya Sh bilioni moja na kusababisha hasara ya Sh bilioni 2.4 kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART).

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Geoge Barasa.

Barasa aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Kulwa Kisena, Charles Newe na Chen Shi.

Alidai shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote, wanaodaiwa kati ya Januari mosi 2011 na Mei 31, mwaka 2018 katika maeneo yasiyofahamika Dar es Salaam kwa nia ovu walipanga kutenda kosa.

Shtaka la pili na la tatu linamkabili Kisena na Kulwa ambao wanadaiwa kati ya Januari mwaka 2015 na Desemba 31, 2017 maeneo ya Jangwani wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Zenon kwa pamoja walijenga kituo cha mafuta bila kibali cha Ewura.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujiingiza katika biashara ya kuuza mafuta katika yadi ya mabasi yaendayo haraka iliyopo Jangwani.

Barasa alidai shtaka la nne linamkabili Kisena na Kulwa wakiwa wakurugenzi wa UDART na mshtakiwa Nawe akiwa mhasibu wa kampuni hiyo waliiba mafuta ya petroli yenye thamani ya Sh 1,216,145,374.10.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kutakatisha fedha na wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 Dar es Salaam.

Kwa nyakati tofauti washtakiwa wanadaiwa kutakatisha jumla ya Sh 2,432,290,748.20 huku wakijua mafuta hayo ya petroli na fedha ni zao la wizi.

Mshtakiwa Kisena na Shi wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kughushi na mawili ya kuwasilisha nyaraka za uongo.

Inadaiwa Oktoba 20 mwaka 2012 walighushi nyaraka ya uamuzi wa bodi kwa lengo la kuonesha kwamba Kampuni ya uhandisi ya Longway inafungua akaunti katika benki ya KCB wakati wakijua si kweli na wanadaiwa kutoa nyaraka hizo KCB.

Pia wanadaiwa kughushi idadi ya wanahisa kwa lengo la kuonesha kwamba watu hao ndio wanahisa wa Kampuni ya Uhandisi ya Longway, wameidhinisha kufungua akaunti wakati wanajua si kweli na wakawasilisha nyaraka hiyo KCB.

“Shtaka la 11 linamkabili Kisena, anadaiwa Aprili 6 mwaka 2016, NMB benki alijaza fomu ya kuhamisha fedha Sh 594,925,000 akionyesha fedha hizo ni malipo ya Kampuni ya Longway kwa ajili ya matengenezo ya makabati, vifaa na kazi za ujenzi huku akijua si kweli na aliwasilisha fomu hiyo NMB bank.

“Shtaka la 13 linamkabili Kisena na Shi. Wanadaiwa Juni 8,2016 Benki ya NMB Tawi la Bank House walijipatia Sh 594,925,000 kwa njia ya udanganyifu,” alidai Barasa.

Alidai shtaka la 14 linamkabili Kisena na Shi akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Longway, Mei 30 katika Benki ya NMB walitakatisha Sh 594,925,000  huku wakijua ni zao la kosa la kughushi.

Barasa alidai shtaka la 15 linamkabili Kisena na Shi ambao wanadaiwa Mei 26, mwaka 2016 walijaza fomu ya kuhamisha fedha Benki ya NMB, Sh 750,000,000 walionyesha ni malipo ya Kampuni ya Longway kwa ajili ya kujenga uzio katika vituo vya mabasi yaendayo haraka Kimara, Feri, Ubungo na Morocco wakati si kweli.

Washtakiwa wanadaiwa kuwasilisha nyaraka hiyo benki na kujipatia Sh 603,255,886.58 kutoka DART kwa njia ya udanganyifu.

Shtaka la 18 linamkabili Kisena na Shi, ambao wanadaiwa kutakatisha Sh 603,255,886.58 huku wakijua ni zao la kosa la kughushi.

Barasa alidai shtaka la mwisho linawakabili washtakiwa wote ambao wanadaiwa katika kipindi hicho walisababisha DART kupata hasara ya Sh 2,414,326,260.70.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, upelelezi haujakamilika na kesi itatajwa Februari 25, mwaka huu.

Wakili wa utetezi, Majura Magafu aliomba upelelezi ukamilike haraka kwa sababu washtakiwa wamekuwa wakiripoti Takukuru karibu mwaka mzima. Washtakiwa wameenda Segerea.

MTANZANIA ILIVYOFICHUA

Hatua ya kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao ilitokana na ripoti maalumu iliyotolewa na gazeti hili kuhusu madudu ya usafiri wa mwendokasi, ikiwamo baadhi ya viongozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa vituoni kukwapua mamilioni ya shilingi kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo ilieleza hatua ya kushuka kwa kasi kwa mapato hasa katika Kituo cha Kimara.

Kwamba zilikuwa zikikusanywa Sh milioni 20 hadi 25 kwa siku wakati ulipokuwa ukitumika kupitia mfumo wa ukusanyaji wa kieletroniki na kushuka hadi kufikia hadi Sh milioni 10 kwa siku.

Kutokana na hali hiyo DART kwa kushirikiana na vyombo vya dola, walifanya uchunguzi na kubaini mtandao huo wa wizi huku kigogo wa juu wa UDART akibainika kuhusika jambo lililosababisha kukamatwa.

Inadaiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi (majina yanahifadhiwa kwa sasa kwa sababu za kiuchunguzi), waliunda mtandao maalumu wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha.

Mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000 na kwa kila safari hulazimika kulipa Sh 650 ukijumlisha kwa idadi hiyo mapato kwa siku yaliyokuwa yanakusanywa hufikia Sh milioni 130 ingawa kwa sasa yameshuka.

Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki, pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi za Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikingia katika mifuko ya wajanja.

Aprili 24 na Mei 16, mwaka huu makusanyo yalianza kuhujumiwa baada ya UDART kuingilia kati na kutaka kukusanya wao fedha huku wakipinga uwepo wa tiketi za kieletroniki chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles