28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili kesi ya dhahabu walalamika

PETER FABIAN-MWANZA

MAWAKILI wa washtakiwa 12 wa kesi namba 1/2019 ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha iliyohusu utoroshaji dhahabu yenye uzito wa kilogram 323.6 yenye thamani ya Sh bilioni 27, wameilalamikia mahakama kuzuiwa kuonana na wateja wao wakiwa mahabusu pamoja na mahakamani.

Akiwasilisha malalamiko hayo mahakamani jana mbele ya Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Gwai Sumaye, wakili wa washtakiwa Anthony Nasimile kwa niaba ya wenzake Steven Makwega na Fidel Mtewele, alisema wakiwa watetezi wanayo haki ya msingi kwa mujibu wa katiba kuwasiliana na mawakili wao.

“Mheshimiwa tunayo maombi mawili la kwanza ni kuomba mahakama yako itupe fursa ya kuwaona wateja wetu (washtakiwa) kwa kuwa tumekosa fursa hiyo kutokana na utaratibu wa kuletwa hapa mahakamani na kurejeshwa rumande gerezani Butimba, jambo ambalo ni kuwanyima haki yao kikatiba.

“Na ombi letu la pili ni kuhusu tarehe ya kuwaleta na kusikilizwa kesi hii tungependekeza iwe Februari 22, mwaka huu kwani tofauti na hapo sisi mawakili tutakuwa nje ya Mwanza kusikiliza kesi za wateja wengine,” alisema Nasimile.

Akisisitiza juu ya ombi la kwanza, Wakili Nasimile aliieleza mahakama hiyo kwamba hakuna mahali ambapo sheria inakataza mawakili kuwaona washtakiwa ambao ni wateja wao na kwamba mpaka wawe na kibali cha mahakama hata wanapokwenda gerezani ambao wanashikiliwa kama mahabusu.

Awali Wakili Nasimile alitaka kujua upande wa mashtaka umefikia wapi juu ya upelelezi wa kesi hiyo ili mahakama ipange tarehe ya kuanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu.

Akitoa maelezo mahakamani hapo Wakili Mwandamizi wa Serikali, Castuce Ndamugoba alieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na wanaendelea kuukamilisha na pindi utakapokuwa tayari wataharakisha na kuwasilisha mahakamani.

Akizungumzia suala la kuwazuia mawakili watetezi kuwaona wateja wao hawana mamlaka ya kuingilia amri ya mahakama ya kuwapeleka rumande watuhumiwa.

Akijibu maombi ya mawakili wa utetezi, Hakimu Mfawidhi Gway Sumaye alisema kwamba tarehe ya kurejeshwa mahakamani kwa washtakiwa ni Februari 25, mwaka huu kwa mujibu wa kalenda ya mahakama haoni sababu ya kutoifuata na kuomba pande zote kukubaliana.

Akikizungumzia mawakili kuzuiwa, alisema mahakama haiwezi kuwapangia mawakili muda wa kuonana na washtakiwa katika kesi hiyo na kuwaomba waende kuwatembelea siku za mwishoni mwa wiki gerezani kwa kuwa ni haki yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles