28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Mauaji ya watoto: Mkuu wa majeshi atia mguu Njombe

Elizabeth Kilindi-Njombe

MKUU wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, ametua mkoani Njombe   kufuatilia matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyotikisa mkoani humo.

Aamesema   Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), litakomesha matukio yote ya mauaji nchini yanayosababishwa na imani potofu.

Kauli hiyo aliitoa  mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Alisema baada ya kufikia mkoani hapa amefanya kikao hicho pamoja na vikosi maalumu vilivyopo mkoani hapa kuchunguza matukio hayo.

Jenerali Mabeyo alisema sababu za utekaji na mauaji ya watoto  yanahusisha zaidi ngazi ya familia na vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza kuchukua hatua kukomesha mauaji hayo.

“Ninapenda kusema kwamba kwa sasa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa kushirikiana   na jeshi.

“….mimi ndiye mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi hivyo ninao wajibu na si kwamba jeshi limeingia sasa, hapana hatujafikia hatua ya kuingiza jeshi.

“Na wananchi karibu nchi nzima wamesikia kinachoendelea hapa Njombe na wengine wametiwa hofu si Tanzania tu, mpaka nje ya mipaka yetu taarifa zimesambaa,”  alisema Jenerali Mabeyo.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama baada ya matukio hayo ilipeleka  timu maalumu mapema   iweze kushirikiana na vyombo vilivyopo Njombe   kufanya uchunguzi makini na wa kina.

Kutokana na matukio hayo, amewataka wananchi kutulia kwa sababu  vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake vizuri kuhakikisha waliohusika wanabainika.

Alisema  sababu ya kutekeleza mauaji hayo zinafahamika na   taratibu za  sheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote wa matukio hayo.

“Ninachosema kwa sasa pasiwepo na hofu, suala hili ni la  taifa zaidi, linahusu pengine familia moja moja, sababu zinajionyesha kabisa ni za  familia zaidi,” alisema.

Mkuu huyo wa majeshi, alisema suala hilo lazima litakomeshwa na si Njombe pekee bali nchi nzima katika maeneo mengine yenye matukio kama hayo kwa imani potofu kwa wananchi  inayotaka kuanza kujengeka.

Aliwataka wananchi waendelee kufanya kazi zao kama kawaida kwa vile  kwa sasa vyombo vya dola vinatekeleza majukumu yake.

Alisema vyombo vyote vya dola vinashirikiana   kujua ni kina nani waliohusika, sababu za kuhusika na mbinu zilizotumika na watekelezaji wa mauaji hayo.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga, alisema hadi sasa watuhumiwa 30 wanashikiliwa kwa kuhusika kwao na utekaji na mauaji ya watoto hao.

Alisema jalada la watuhumiwa hao lipo kwa mwanasheria na muda wowote   akikamilisha utaratibu wa  sheria watafikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles