24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WAVULANA WAVAA SKETI, WASICHANA MAJINA YA KIUME UINGEREZA

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA


KATIKA kile kinachoonekana mporomoko wa maadili na kuachana na uasili tuliokabidhiwa na Muumba, shule nchini Uingereza zimeanzisha sera mpya ambayo wavulana wanavalia sketi shuleni.

Mbali ya hilo kuna kampeni ambayo inalenga kuharamisha neno ‘wasichana’ kuwatambulisha wanafunzi wa kike shuleni.

Na wakati tayari wasichana huvaa mavazi ya kiume katika shule nyingi, wanafunzi wengine wa kike hutaka kutambulika kwa majina ya kiume, kitu ambacho kinaonekana kubarikiwa.

Kama hiyo haitoshi shule nchini humo, kama ambavyo imewahi kutokea wakati wa utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani zinapanga kuvifanya vyoo vitumike bila kujali jinsia.

Hilo linamaanisha mwanafunzi wa kiume au wa kike atakuwa na haki ya kuingia maliwato yoyote ambayo roho yake inamtuma kuingia.

Taarifa za karibuni zaidi ni kuhusu shule moja binafsi iliyo kaskazini mwa Jiji la London, ambayo imetangaza mpango utakaoshuhudia sare za shule ambazo zitakuwa hazitambulishi jinsia.

Lengo la kufanya hivyo ni kile kinachodaiwa kuitikia idadi kubwa ya wanafunzi wanaozidi kuongezeka wakihoji utambulisho wa jinsia zaio.

Kwa maana hiyo wavulana wa shule hiyo wataruhusiwa kuvalia sketi iwapo sheria hiyo mpya kuhusu sare ya shule itaidhinishwa.

Shule hiyo ya Highgate inapanga kuruhusu wanafunzi kuvalia sare yoyote ile ambayo wanafunzi wanaitaka bila kujali jinsia.

Wamechukua hatua hiyo baada ya kugundua watoto wengi wanauliza maswali kuhusu jinsia yao.

Shule hiyo, ambayo hutoza karo ya hadi pauni za Uingereza 6,790 sawa na zaidi Sh milioni 19.5 kwa kila muhula pia inapanga kuvifanya vyoo kuwa huru kwa watoto wa jinsia zote.

Aidha, hakutakuwa na michezo tofauti ya wasichana na wavulana.

Wasichana katika shule hiyo kwa sasa huruhusiwa kuvalia sare ya wavulana – suruali za rangi ya kijivu, jaketi za rangi ya bluu iliyokolea.

Mkuu wa Shule hiyo, Adam Pettitt anasema: "Kizazi hiki kwa kweli kina udadisi mno."

Alisema kwamba baadhi ya wanafunzi wa zamani wamelalamikia mabadiliko hayo. "Wameandika kwamba iwapo unamuacha mtoto katika vifaa vyao wenyewe, makuzi yao yataelekea kuwa tofauti na hivyo kuhamasisha mwelekeo mbaya," anasema.

Baadhi ya wazazi hawakujua kwamba watoto wao huhoji maswali kuhusu utambulisho wa jinsia zao hali iliilazimisha shule isuluhishe baina ya wazazi na watoto.

Shule hiyo tayari inaruhusu watoto kuwaomba wafanyakazi wa shule wawatambue kwa majina ya jinsia nyingine, kitu ambacho nusu ya wanafunzi wameshafanya hivyo.

Aidha mvulana mmoja tayari amesharuhusiwa kuvaa sketi shuleni hata kabla ya sheria kupitishwa kutokana na udharura.

Shule nyingine za msingi tayari zimeshaanzisha sera ya kukabiliana na watoto wanaohoji utambulisho wa jinsia zao.

Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Paul ina sera za utambulishio wa jinsia, ambayo huruhusu wanafunzi wa kike kuitwa majina ya kiume na kuvaa nguo za wavulana.

Chama cha Shule za Wasichana nchini Uingereza kimeshauri wanachama wake kuacha kutumia neno ‘wasichana’ na badala yake kuwaita kama wanafunzi.

Chuo cha Kati cha  Brighton pia kimebadili sare zake za chuo ambazo zimedumu kwa miaka 170 kwa kuanzisha ile ambayo haitambulishi jinsia.

Mwaka jana ilifichuka kwamba shule zipatazo 80 za serikali zilikuwa zikiruhusu wanafunzi kuvalia sare za jinsia tofauti na yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles