MWALIMU ALIYEFUNDISHWA KUDADISI HUWAPA UJUZI WANAFUNZI WAKE

0
709

Na Christian Bwaya


MALALAMIKO mengi dhidi ya kiwango duni cha elimu nchini yanatokana na ukweli kwamba Taifa halijaweza kuzalisha wahitimu wanaojua wajibu wao. Tumekuwa na idadi kubwa ya watu waliofaulu vizuri darasani lakini wasioweza kubadilisha chochote katika jamii. Wasomi hawajui wafanye nini na maarifa yaliyonayo kwa sababu kile walichokisoma hakina uhusiano wa moja kwa moja matatizo yanayoikabili jamii yetu.

Kwa kuwa wasomi wamekosa namna ya kuthibitisha kuwa wanao mchango kwa jamii inayowazunguka, wameamua kuwa wajasiriamali. Wasomi wameanza kushawishiana kuachana na mambo waliyoyasoma na badala yake wanageukia uchuuzi. Mahubiri ya wajasiriamali wanaotoa wito kwa wasomi kuacha taaluma zao ili wawe wachuuzi wa bidhaa ni kilio cha jamii kwamba haijaona kazi inayofanywa na wasomi. Jamii nayo imeanza kukata tamaa na wasomi.

 

Mambo mengi yametufikisha hapa tulipo. Kwanza, ni utamaduni wa watu kusoma mambo yasiyoendana na vipaji walivyonavyo. Tunajua uamuzi wa kipi mtu asome umekuwa ukiongozwa na sababu zisizo na mashiko. Kwa mfano, wapo wanafunzi wengi wanaosomea fani fulani kwa sababu tu ‘kusoma vitu vigumu ni sifa fulani.’ Lakini pia wapo wanafunzi wengi wanaofanya maamuzi yanayoongozwa na misukumo ya nje kama vile soko la ajira na matarajio ya jamii isiyojitambua. Hata hivyo, pengine ni muhimu kuhoji ikiwa ni sahihi elimu kuendelea kuongozwa na soko la ajira lisilotabirika.

 

Sababu ya pili na kubwa ni ufundishaji. Tunalo tatizo kubwa la walimu kushindwa kutafsiri mtalaa katika maisha halisi. Walimu wamebaki kuwasaidia wanafunzi kukariri maarifa ya kufikirika yasiyojibu matatizo halisi ya jamii tunamoishi.

 

Nakumbuka siku ya kwanza kusikia neno ‘cell’ nikiwa kidato cha kwanza haikuwa kazi rahisi kupata picha. Mwalimu wetu alituandikia ubaoni kuwa, ‘cell is a basic unit of life.’ Tuliduwaa. Mwalimu alisubiri tuandike sentensi hiyo kwenye madaftari yetu. Tulifanya hivyo. Kazi iliyofuata ilikuwa ni kukariri sentensi hiyo bila kuelewa ina maana gani. Mtihani ulipokuja tulijibu vile vile bila kukosea na mwalimu alitupa alama za juu kwa kurudia kile kile alichokuwa ametukaririsha. Lakini ukweli ni kwamba hatukuwa na uelewa wa kile tunachoambiwa tumejifunza.

 

Huu ni mfano wa namna ufundishaji unavyochangia kwa kiasi kikubwa kufanya maarifa yanayokusudiwa na mtalaa yakose maana kwenye maisha halisi ya wanafunzi. Tunasoma vitu vingi tusivyoviona kwenye maisha yetu ya kila siku. Matokeo yake tunaishia kukumbuka na kufaulu mitihani kwa kiwango cha juu lakini thamani yetu ikibaki kuwa pale pale.

 

Ikiwa tunataka kubadili hali ya mambo, mahali pa kuanzia ni kuwekeza kwenye maandilizi madhubuti ya walimu. Kama nilivyoeleza kwa majuma kadhaa, mwalimu ndiye anayebeba dhima ya elimu. Bila mwalimu aliyeandaliwa vyema, hatuwezi kuona matunda ya sera nzuri za elimu, mitalaa mizuri, madarasa bora na hata vifaa bora vya ujifunzaji na ufundishaji.

 

Tunapozungumzia maandalizi ya walimu, tunaongelea vyuo vya ualimu na vitivo vya elimu katika vyuo vikuu. Tunalo tatizo kubwa la namna wakufunzi na wahadhiri wetu wanavyowaandaa wanafunzi watakaokuwa walimu siku zijazo. Wahadhiri vya vyuo vikuu hutumia njia ya ‘mahubiri’ kuwaandaa walimu. Hakuna mahali mwanafunzi huyu anapewa nafasi ya kushiriki mchakato wa ujifunzaji isipokuwa kukariri kitini. Hali hii inachangiwa na mtazamo walionao wahadhiri wengi kwamba wao ndio wamiliki wa maarifa na wanafunzi ni walaji wa kile wanachoambiwa.

 

Tunafahamu wapo wahadhiri wasioruhusu maswali kutoka kwa wanafunzi. Wanaamini kuulizwa swali na mwanafunzi ni kudhalilishwa na mwanafunzi bora ni yule ‘asiyesumbua darasani.’ Kama vile haitoshi, wanapotoa mitihani wanategemea kuona hoja zile zile zilizoainishwa kwenye kitini. Kinyume na hapo mwanafunzi anakuwa anajitakia kuanguka mtihani.

 

Mwanafunzi huyu anayejifunza ualimu katika mazingira haya ya kidikteta, kwa vyovyote vile atafanya yayo hayo atakapokwenda shuleni. Badala ya kuwa mwalimu, atajipachika kazi ya ‘uhubiri’ kuiga yaliyokuwa yakifanywa na wahadhiri wake vyuoni. Hatakubali kumpa nafasi mwanafunzi kuhoji kile anachokifundisha.

 

Tunahitaji kubadili namna tunavyowaandaa wanafunzi wetu vyuoni. Wakufunzi na wahadhiri wa ualimu waoneshe mfano wa kuwashirikisha wanafunzi katika mchakato wa kujifunza. Vyuo viwe na utaratibu endelevu wa kuwajengea uwezo wahadhiri katika mbinu za ufundishaji. Badala ya wahadhiri wa ualimu kufundisha kwa mbinu za kimazoea, wabadilike na kuonesha mfano wa ushirikishwaji wa mwanafunzi katika mchakato wa kujifunza. Tukifanikiwa kuwabadili hawa ambao kwa idadi yao ni wachache chachu yake inaweza kusambaa kwa haraka kuzifikia shule zetu ndani ya muda mfupi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here