24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI WILAYANI MASWA WALILIA HUDUMA ZA AFYA

 

NA SAMWEL MWANGA, MASWA


WANANCHI wilayani Maswa mkoani Simiyu, wameiomba Serikali, wadau wa afya na mashirika binafsi kujitokeza kusaidia kutoa huduma za afya ili kuwawezesha  kupata  huduma karibu.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana katika mji wa Malampaka wilayani humo katika kampeni ya utoaji huduma za afya iliyotolewa na  Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), baadhi ya wananchi hao walisema  mfuko huo  umewasaidia kuwasogezea huduma  na kuomba iwe endelevu.

Walisema utaratibu huo wa upimaji wa afya bure ulioanzishwa na Tasaf utawasaidia, kwani wilaya hiyo bado inakabiliwa na uhaba wa zahanati na vituo vya afya huku watoa huduma wakishindwa kuwafikia wananchi kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika unaosababishwa na uduni wa miundombinu ya barabara.

Rahel Charles mkazi wa Kijiji cha Malampaka, alisema huduma ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kwa akina mama wanazipata kwa kutegemea hospitali ya wilaya ya Maswa iliyoko umbali wa kilomita 30 na husafiri zaidi ya saa mbili kwa baiskeli ili kuipata.

“Tunaiomba Serikali itusogezee huduma hii lakini hata mashirika binafsi yajitokeze kutusaidia kupata huduma hizi kwa wananchi, vipimo vya shingo ya uzazi hatuvipati lakini leo Tasaf wametusogezea hadi kijijini kwetu, tunashukuru sana na mwitikio umekuwa ni mkubwa,” alisema.

Alisema watu wengi wanapopatwa na matatizo ya afya kama shingo ya kizazi wanatumia dawa za kienyeji na kuwasababishia kupoteza maisha na kuwataka wakinamama kuwahi hospitali pindi wanapobaini matatizo katika afya zao.

Kwa upande wake Ofisa Ufuatiliaji Tasaf, Wilaya ya Maswa, John Wambura, alisema licha ya wao kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini, lakini waliona ni vyema walengwa wa mradi hasa wakinamama wakapimwa ili kujua afya zao kutokana na wengi wao kutoipata huduma hiyo kutokana na umbali wa vituo vya afya.

“Tunapokuwa na zoezi la uhawilishaji   huwa tunawapatia walengwa wa mradi fedha zao za ruzuku, tunakuwa sambamba na wataalamu wa afya ambao hutoa elimu juu ya umuhimu wa mtu kupima afya yake baadaye kwa hiari yao wanakwenda kwenye mabanda tuliyoyatenga kwa ajili ya zoezi hilo,” alisema.

Naye Revina Justus ambaye ni Muuguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa, alisema zoezi hilo limefanikiwa kwani wameweza kuwapata wateja kwa wingi na mara moja tofauti na wanapokuwa kwenye huduma nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles