Wanamuziki wa dansi mnakwama wapi? Fanyeni maamuzi

0
1601

INAPENDEZA unapoona muziki wa Bongo Fleva ukizidi kuchanua kadri siku zinavyokwenda lakini wakati huo huo upande wa dansi hali bado ni tete.

Jaribu kupita kwenye vilinge mbalimbali vya muziki huo utakutana na mijadala inayohusu kuunusuru.

Mijadala hiyo inapata nafasi kutokana na ukweli kwamba mambo yanayoongeza hamasa kwa mashabiki kufatilia Dansi yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Licha ya Dansi kuonekana imepoteza mvuto na haina mzuka tena kwa mashabiki, wanamuziki wake wameendelea kuzalisha muziki kila uchwao japokuwa changamoto ni namna bidhaa hiyo (Nyimbo) inavyoweza kuwafikia walaji (mashabiki).

Vyombo vingi vya habari hasa redio na runinga hazina vipindi vyenye maudhui ya Dansi. Vipindi vingi vinatumia muziki wa Bongo Fleva saa 24 kwa siku 6 angalau redio na runinga zingine hutenga siku moja wisho wa wiki kucheza muziki wa Dansi kwa saa chache.

Hivyo basi mwanamuziki au bendi ya Dansi ikitengeneza kazi mpya inakuwa ngumu kuwafikia shabiki, nyimbo zinafanyika ila haziwafikii kwa wakati mashabiki wa Dansi na hata zikiwafikia watazisikia na kuziona mara chache katika vyombo vya habari.

Kwa muktadha huo Swaggaz tuna machache kwa wanamuziki na mashabiki wa Dansi ili tuweze kutoka hapa tulipokwama maana naamini Dansi ina mashabiki wengi na wasanii ndiyo wenye jukumu la kurudisha morali iliyopotea.

Kwanza kabisa huu siyo muda wa wanamuziki kutegemea redio na runinga kufikisha muziki wao kwa mashabiki. Vyombo vingi vya habari vinaendeshwa kibiashara hivyo kila dakika kwao ni fedha, sasa ngoma zetu za Dansi ili zinoge angalau zipigwe zaidi ya dakika 5.

Sasa usitarajie wimbo wako uchezwe redioni au runingani kwa hizo kwa hizo dakika zote. Nyimbo ndefu zimepitwa na wakati, zinakera na kuchosha si rahisi mtu akasikiliza mwanzo mwisho, tutengeneze nyimbo fupi, tamu zilizojaa ubunifu wenye kukonga nyoyo.

Natamani kuona wawanamuziki wa dansi wakitumia mitandao ya kuuza na kusikilizia muziki kama vile mkito.com, Boomplaymusic, Mdundo.com.  Deezer, Spotify na sehemu zingine ambazo pia huwaingizia fedha nyingi wasanii wa Bongo Fleva.

Hakuna kinacho shindikana ni nyinyi wenyewe wana dansi kuamua kufanya mabadiliko haya, mashabiki wapo tayari kupokea chochote kizuri kutoka kwa wananamuziki, tufanye maamuzi thabiti ili tupige hatua.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here