23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Mahakama yaamuru dhahabu iliyokamatwa Kenya itaifishwe

BENJAMIN MASESE-MWANZA

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza, imetoa amri ya kutaifishwa madini ya dhahabu kilo 35.34 yenye thamani ya Sh bilioni mbili yaliyokamatwa Februari 2018 katika  Uwanja wa ndege Kimataifa wa Jomo Kenyattai Nairobi Kenya, yakisafirishwa kuelekea Dubai.

Amri hiyo ilitolewa baada ya washtakiwa wawili wa kesi ya utakatishaji fedha na utoroshaji madini iliyokuwa ikiwakabili watuhumiwa 14, kukiri kosa huku wengine 12 wakiachiwa.

Watuhumiwa waliokiri kosa  ni Charles Warioba na Marwa Warioba, ambao wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 115 au kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo jana, Jaji wa mahakama hiyo, Rhoda Ngimilangwa, alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri, mahakama imewakuta na hatia watuhumiwa hao kwa kutenda makosa matatu ambayo ni kuongoza genge la uharifu, kusafirisha madini kinyume cha sheria na kutakatisha fedha.

Awali akiwasilisha hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, alieleza kuwa kwa nyakati tofauti, Januari Mosi na Februari 15, mwaka 2018 kwenye maeneo tofauti nchini Kenya na Uganda, watuhumiwa waliongoza genge la uhalifu na kuvunja sheria.

Pia watuhumiwa hao Februari 15,2018 walivunja sheria namba 18 kifungu cha (1) na kifungu kidogo cha 4 (a) na sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010 kwa kumuongoza Baraka Owino kusafirisha madini kilo 35.34 yenye thamani ya Sh bilioni mbili  kinyume cha sheria  kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza, Kilimanjaro hadi Jomo Kenyatta Nairobi lengo likiwa ni kupeleka Dubai.

Alisema Januari Mosi na Februari 15, 2018 watuhumiwa walivunja sheria namba 12 (a) na sheria namba 13 (a) ya mwaka 2006 ya utakatishaji fedha kwa kujihusisha na biashara ya madini ya dhahabu kilo 35.34 wakati wakijua madini hayo yalipatikana kwa njia haramu.

Upande wa Jamhuri uliwasilisha vielelezo kadhaa kama ushahidi ambavyo ni hati za safari za watuhumiwa, nyaraka za mamlaka ya mapato ya Kenya, picha za makabidhiano madini kati ya Serikali ya Tanzania na Kenya.

Pia waliwasilisha nyaraka za kuhifadhi mzigo wa dhahabu  Benki Kuu ya Tanzania (BOT), hivyo waliiomba mahakama kutoa amri ya utaifishwaaji wa madini hayo pamoja na kutoa hukumu kubwa kama fundisho na onyo kwa wengine.

Naye wakili wa utetezi, Wilbert Kilenzi, aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa jicho la huruma kwani wateja wake wamekiri makosa yote bila shuruti na wamethibitishwa kuwa ndilo kosa lao la kwanza.

Pia alisema  watuhumiwa walikuwa wameshakaa rumande kwa mwaka mmoja hivyo watakuwa wamejifunza na pia watuhumiwa wote wana matatizo ya kisukari ambapo aliomba kulingana na kifungu cha 27 kifungu kidogo cha pili (2) cha sheria ya makosa ya jinai,  mahakama itoe  adhabu ya faini zaidi kuliko kifungo cha gerezani.

Akizungumza ofisini kwake baada ya hukumu hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema  hukumu hiyo imetolewa kwa kuzingatia  misingi ya sheria na hivyo ni wakati wa kila Mtanzania kubadilika na kujifunza kutoka kwa wenzao.

Itakumbukwa madini hayo baada ya kukamatwa nchini Kenya, yalikabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania Julai 24, Ikulu Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais Dk. John Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje ya Kenya, Monica Juma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles