Na SAMWEL MWANGA
WAKULIMA wa pamba mkoani Simiyu wameitaka serikali kuivunja Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kwa kuwa imekuwa na kiburi.
Wamedai bodi hiyo inataka kuua biashara ya bei ya zao hilo huku wakulima wakinyanyasika.
Vilvile wamewataka viongozi serikalini wanaoikumbatia bodi hiyo kuacha mara moja kwa kuwa imekuwa hata ikishindwa kutekeleza maagizo mbalimbali yanayofikiwa na mkutano mkuu wa wadau wa zao hilo ikiwamo kuwapo mashamba ya kuzalisha mbegu za pamba.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Bariadi, walisema wanashangazwa na kitendo cha bodi hiyo kugeuka kuwa ndiyo msimamizi mkuu wa upangaji wa bei ya pamba kwa mkulima wa pamba badala ya kusaidia kilimo hicho kikue.
Walisema umefika wakati kwa bodi hiyo kuvunjwa kwa sababu imeshindwa kuendeleza zao hilo na kila kukicha mkulima wa pamba amekuwa akinyanyasika huku watumishi wa bodi hiyo wakiendelea kuneemeka kupitia jasho la wakulima.
“Mimi nataka serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi avunje bodi hii kwa sababu kazi yake ni kupanga bei ya pamba badala ya kuwasaidia wakulima kuendeleza kilimo hicho “Hata bei wanayopanga ni ya kumnyanyasa mkulima huku wao wakiendelea kunufaika kwa kutumia jasho letu sisi wakulima,” alisema Khija Malimi.
Madirisha Saguda alisema watu milioni 16 wanategemea kilimo hicho na wamekuwa wakilia kila siku kupata soko zuri la zao hilo lakini bodi hiyo imekuwa haina faida kwao.
Alisema hivyo ivunjwe na kusisitiza kuwa ndiyo mchawi mkubwa wa zao hilo hivyo haina umuhimu ivunjwe tu.
“Wakulima tupatao milioni 16 nchini tunaolima zao hili la pamba kila mwaka tumekuwa tukililia tupate bei nzuri ya pamba kutokana na gharama kuwa kubwa za uzalishaji.
“Lakini kinachotokea ni hawa bodi ya pamba wanakuja na kutupangia bei kwa maslahi yao na kwa uhalisia mchawi wa pamba ni bodi yetu hii ya pamba, naona haina umuhimu ni vizuri ikavunjwa,”alisema Saguda.
Naye Mayunga Kisena alisema bodi hiyo imekuwa ni kikwazo cha kuendeleza zao hilo kwa vile imekuwa ikimkandamiza mkulima na wafanyabiashara wadogo wa zao hilo huku w wafanyabiashara wakubwa wakikumbatiwa kwa manufaa yao binafsi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga, alisema bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa ujanjaujanja.
Alisema bodi hiyo inashindwa hata kusimamia maagizo yaliyopitishwa kwenye mkutano wa mwaka jana wa wadau wa zao hilo ya kutaka ianzishe mashamba ya kuzalisha mbegu ya zao hilo, badala yake inatumia mashamba ya wananchi.