25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAGOMA KUKATWA 30,000/-

Na Fredy Azzah-DODOMA


LICHA ya kila Mbunge kulipwa posho ya Sh 220,000 kila anapohudhuria kikao cha Bunge, jana walikataa kukatwa Sh 30,000 za kumsaidia, Mshindi wa Tanzania super model, Asha Mabula, huku wengine wakitishia kwenda mahakamani endapo watakatwa fedha hizo.

 Mshindi huyo anatarajiwa kushiriki shindano la dunia la World Miss Super Model litakalofanyika Macau, China.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya kipindi cha maswali na majibu.

 Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta, aliomba mwongozo kwa mwenyekiti wa kikao, Andrew Chenge, akiomba mrembo huyo achangiwe na wabunge angalau Sh 30,000 kila moja  zimsaidie anavyokwenda kuwakilisha Taifa.

Maelezo hayo yaliibua minong’ono kwa wabunge, wengi wakipinga kukatwa fedha hizo.

Wakati akijibu mwongozo huo, minong’ono iliendelea hatua iliyofanya Mwenyekiti wa Bunge, Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi, kuamua kutoa nafasi ya suala hilo kujadiliwa na wabunge.

Aliyepewa nafasi ya kwanza alikuwa ni Mama Sitta, ambaye alisema anajua wabunge wana majukumu mengi, lakini yeye anataka  wachangie Sh 30,000 tu kwa sababu mrembo huyo anakwenda kuliwakilisha taifa.

Alisema kitendo hicho siyo cha kwanza kwa vile  hata Serengeti Boys ilichangiwa na wabunge hao ilivyofuzu kwenda kwenye mashindano ya Afrika (AFCON) kwa vijana wa chini ya miaka 17.

Mbunge wa Mafinga, Kosato Chumi, alisema jambo hilo ni jema kwa sababu anayechangiwa anakwenda kuliwakilisha taifa.

Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM),  alisema wabunge wanachangia sherehe mbalimbali zikiwamo za harusi, lakini anashangaa kukataa kumchangia mrembo huyo anayekwenda kuliwakilisha taifa.

“Kwa hiyo nasema wanaotaka wachangie, wasiotaka waache,” alisema Mlata.

Lakini Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy, alisema kutoa mchango ni hiari ya mtu lakini yeye kwenye suala hilo hayupo tayari kutoa mchango wake.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema jimbo lake lina mambo mengi ya msingi ikiwa ni pamoja na wananchi wake kukabiliwa na baa la njaa ambalo serikali imekataa kulitambua.

Alisema kwa sababu hiyo  suala la mrembo huyo ni vema likaachwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

“Hili jambo ni jema sana isipokuwa wananchi wangu wanakabiliwa na njaa sana, serikali imekataa kutoa chakula hivyo hili jambo hili ni vema akaachiwa Waziri anayehusika,” alisema Lissu.

Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), alisema yeye kwa imani ya dini yake mambo ya urembo yanakataliwa na ndiyo maana Zanzibar hayapo.

“Wengine hata wakati anatambulishwa hapa tulijificha chini ya viti huku,” alisema.

Baada ya wabunge hao kujadili, Chenge alisema kwa kuwa hoja hiyo imeshajadiliwa  atawahoji ni wangapi wanataka na wangapi wanapinga   kuchanga fedha hizo.

Maelezo hayo yalipingwa na baadhi ya wabunge  huku  wengine wakiwa wanasema wapige kura na siyo kuhojiwa.

Hata hivyo, Chenge aliwahoji na baadaye kuamua kwamba  waliokubali kukatwa fedha hizo wameshinda.

Hatua hiyo ilifanya baadhi ya wabunge kuwasha vipaza sauti na kupinga hatua hiyo, huku Keissy akisema akikatwa fedha hizo atakwenda mahakamani.

Taarifa ya Idara ya Habari Maelezo inasema kuwa, juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alitembelewa na Mabula katika ofisi ya Wizara, Dodoma.

Ilisema Mabula aliishukuru Serikali kwa kuwa karibu na tasnia hiyo kwa kushiriki kwenye mashindano yaliyofanyika Arusha mapema mwaka huu.

Ilisema Mabula alimweleza Waziri kuhusu safari anayotarajia kuifanya ya kwenda  Macau kushiriki kwenye mashindano ya World Miss Super Model na kuiomba Serikali kumsaidia kupata wadhamini watakaochangia fedha za safari hiyo  aweze kuiwakilisha vema nchi kwenye mashindano hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles