28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

MAPYA YAIBUKA BOSI UN KUTIMULIWA

*Ni kigogo wa pili kuondolewa nchini kimyakimya, Mbunge ataka maelekezo ya Serikali bungeni


Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Serikali kumfukuza nchini Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo, mapya yameibuka kuhusu sakata hilo.

Gazeti hili ambalo lilikuwa la kwanza kuripoti kwa kina kuondolewa kwa mkurugenzi huyo, limebaini kiongozi huyo ni wa pili kuondolewa na Serikali kutokana na suala la Zanzibar, akitanguliwa na aliyekuwa mshauri wa UNDP, Hamida Kibwana ambaye ni raia wa Kenya.

Hamida ambaye alikuwa mshauri wa UNDP wa masuala ya uchaguzi na aliyewekwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), aliondolewa Novemba 2015 baada ya Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kufutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salimu Jecha.

Baada ya gazeti hili katika toleo lake la jana kuripoti taarifa za kuondolewa kwa Dabo, ambaye anatajwa kuponzwa na misimamo yake dhidi ya Serikali ya Tanzania na kudaiwa kuzuia baadhi ya fedha za miradi.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kuibuka kwa matukio kadhaa yanayotajwa kukiuka misingi ya haki za binadamu, kiongozi huyo aliandika taarifa mbaya dhidi ya Serikali na kuituma kwa nchi wahisani.

Hatua hiyo inatajwa kama moja ya sababu baadhi ya nchi kutoa misaada kwa masharti na hata kuhoji baadhi ya mambo ya nchi, jambo ambalo linadaiwa ni kinyume cha sheria.

“Awa (Mkurugenzi wa UNDP aliyefurushwa) ni mmoja ya watendaji wenye misimamo ya ajabu sana kama unakumbuka hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alitaka kuwapa NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) kopyuta maalumu ili matokeo yakija yanaonekana moja kwa moja lakini pamoja na hali hiyo NEC ilimtega na kumwambia teknolojia hiyo itatumika wakati mwingine.

“Lakini pia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hasa upande wa Zanzibar pia anadaiwa aliandika ripoti nzito sana kwenda Umoja wa Mataifa pamoja na nchi wahisani kwa Tanzania jambo ambalo hata wanapokuja nchini Serikali imejikuta ikihojiwa masuala ya Utawala Bora na Demokrasia.

“Inaelezwa kwa kina kuwa ripoti yake hiyo imesababisha baadhi ya fedha za miradi ya maendeleo ambazo zilitakiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa kupitia UNDP zilikwamishwa kwa baadhi ya maeneo.

“Si hilo tu hata hatua ya watu kukamatwa kwa maelezo kwamba wanakiuka sheria ya mtandao ni sababu nyingine iliyoonekana kuikaanga Serikali hasa kutokana na msimamo wake wa sasa,” alisema mtoa habari wetu ambaye hakuwa tayari jina lake kutajwa gazetini.

Akizungumza na MTANZANIA juzi kuhusu kuondolewa kwa kiongozi huyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Aziz Mlima, alisema kuondolewa kwake kulitokana na kuibuka kwa mgogoro kati yake na wafanyakazi wa UNDP waliopo nchini.

Dk. Mlima alisema baada ya kuibuka kwa mgogoro huo, Serikali iliamua kuandika barua Umoja wa Mataifa ikitaka kuondolewa kwa mkurugenzi huyo.

“Unajua unapokuwa na kiongozi kama huyo ana kinga ya ubalozi, ni lazima ufuate taratibu na si vinginevyo, hivyo baada ya tukio hilo tuliandika barua kati ya Aprili 6 au 7 na kuomba kuondolewa kwa kiongozi huyo.

“Na kikubwa unapokuja katika nchi kama yetu ni lazima ushirikiane na Serikali iliyopo na si vinginevyo na kwenda kinyume ni sawa na ukwamishaji wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025. Na UNDP ni mbia mkubwa wa maendeleo kwa nchi yetu, ila kama unakuja tofauti na malengo na kazi za UNDP, huku ni kuleta mgogoro,” alisema Dk. Mlima.

Alisema mara nyingi Serikali imekuwa ikitoa heshima zote kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwamo UNDP, lakini pindi inapobainika yanakwenda kinyume na malengo ya kazi, Serikali haiwezi kuruhusu hali hiyo.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya nchi ikiwemo Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC), lilitangaza kusitisha kuipatia Tanzania msaada wa Dola milioni 472.8 za Marekani, ambazo ni sawa na takriban Sh trilion moja kwa ajili ya miradi ya maendeleo kupitia awamu ya pili ya mkataba wa shirika hilo.

Hatua hiyo imetokana na Serikali ya Tanzania kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Mbali na hilo, MCC pia ilihitaji kupata uthibitisho kutoka kwa Serikali ya Tanzania kuhusu Sheria ya Makosa ya Mtandao kutumika kukwaza uhuru wa kujieleza na kuwakamata watu wakati wa mchakato na baada ya uchaguzi.

TAMKO JIPYA

Jana Serikali  ilitoa tamko la kuliagiza Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (United Nations Development Programs – UNDP) kwa upande wa Tanzania kumwondoa nchini Mkurugenzi wa shirika hilo, Awa Dabo.

Tamko hilo la jana lilitolewa na Kitengo cha Mawasilino ya Serikali kwa Umma, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, lilieleza kwamba Serikali ilifikia uamuzi huo kutokana na  Dabo kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya watumishi wenzake na menejimenti ya shirika hilo.

“Hivyo kupelekea kuzorotesha utendaji wa shirika hilo nchini na kupunguza kasi ya kuleta maendeleo kwa Watanzania endapo hatua za haraka zisingechukuliwa.

“Baada ya kuthibitishiwa kuondoka nchini, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imetoa rai kwa UNDP kuwakumbusha watumishi wake kuwa kipaumbele chao ni kufanya kazi na Serikali ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano na Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yamefafanuliwa katika Agenda ya mwaka 2030,” ilieleza taarifa hiyo

MBUNGE AHOJI

Baada ya MTANZANIA katika toleo namba 8526 la jana  kuripoti taarifa za kufukuzwa kwa bosi huyo wa UN sakata hilo limeibuka bungeni baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu ambapo Mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga (Chadema), kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akitaka Serikali itoe kauli kuhusu uonevu aliofanyiwa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP.

“Mheshimiwa mwenyekiti, ninaomba mwongozo wako kwa kanuni 68 (7), kuhusu jambo lililotokea leo katika gazeti la Mtanzania toleo namba 8526 limeeleza habari ya kufukuzwa kwa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP ambaye aliletwa na Umoja wa Mataifa (UN).

“Amefukuzwa ndani ya saa 24 chini ya ulinzi mkali na inadaiwa anaingilia mambo ya ndani ya Serikali ikiwepo la uchaguzi wa Zanzibar.

“Mheshimiwa mwenyekiti,  jambo hili linaweza kuleta shida kwa Watanzania ambao nchi yetu ni mwanachama wa UN na jinsi tulivyomwondoa chini ya ulinzi mkali, tumemdhalilisha sana na hili linaweza kutuletea shida kidiplomasia.

“Tunaomba kauli ya Serikali kuhusu suala hili kwa sababu binafsi naona litatuletea shida, kwa kweli linapoharibika jambo naamini tunaathirika nchi nzima,”alisema Haonga.

Kutokana na mwongozo huo, Chenge alisema Bunge ni mhimili kamili na Serikali pia kama ilivyo Mahakama, hivyo haliwezi kuingilia jambo ambalo limetolewa uamuzi na mhimili mwingine.

“Mheshimiwa Haonga kwa heshima zote, huu ni mhimili kamili na Serikali ni mhimili kamili kama ilivyo Mahakama, mhimili wa Serikali umeshaamua kuhusiana na huyo uliyemtaja kwa sababu inazozifahamu mhimili huo.

“Sisi hatuwezi kuanza kuhoji nini kifanyike hatuendi hivyo haya masuala yatasimamiwa na mahusiano yetu ya kimataifa, diplomasia itatumika kama kuna mtu atalalamika huo ndio utaratibu na sisi hatutumii magazeti kufanya maamuzi,” alisema Chenge.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles