23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UDP: Wananchi wasinyang’anywe ardhi  bali waongezewe miliki 

lukuviphotoNa LEONARD MANG’OHA

KATIKA kutekeleza shughulli za kiuchumi, mambo mbalimbali hutegemeana ili kufanikisha shughuli husika ya kiuchumi iliyokusudiwa.

Ingawa huduma anayokwenda kuitoa itakuwa ni ya usafirishaji, bado atatakiwa kupata eneo (ardhi) kwa ajili ya kuegesha magari hayo, kwa maana hii ni kwamba ardhi ndiyo rasilimali muhimu kuliko zote na bila ardhi hakuna shughuli yoyote itakayofanyika.

Hapa nadhani tunapaswa kukubaliana sote kuwa ndiyo ukweli ulivyo na haupingiki kwa sababu hata ukitoa huduma ya usafiri wa anga utahitaji kutumia ardhi kama uwanja wa kutua kubeba abiria na hata kwa matengenezo ya chombo husika.

Pamoja na umuhimu mkubwa wa rasilimali hiyo, bado kuna matatizo kadhaa katika umilikishwaji wa ardhi miongoni mwa Watanzania, kwa mfano ziko baadhi ya jamii haziwapi nafasi wanawake kumiliki ardhi, jambo linalowafanya kushindwa kujiendeleza zaidi kiuchumi.

Yako matatizo kadhaa ikiwa ni  pamoja na ukosefu wa hati kwa wananchi na hati zinazotolewa kutumika kwa muda mfupi wa miaka 33 kwa baadhi ya watu hasa wasio wawekezaji.

Chama cha United Democratic Party (UDP) kupitia taarifa yake iliyotolewa na katibu wa chama hicho, Goodluck Ole-Medeye, kinaitaka Serikali kuongeza muda wa umiliki ardhi kwa wananchi kutoka miaka 33 ya sasa hadi kufikia miaka 99 ili kuwawezesha wananchi kuitumia kama dhamana kukopa kutoka katika taasisi za kifedha.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mfumo wa umiliki ardhi unaotumika sasa wa miaka 33, uliwekwa na wakoloni kwa misingi ya ubaguzi ambapo Waafrika walipewa miaka 33, Waasia 66 na Wazungu 99.

Wanaona sasa ni wakati wa kuondoa ubaguzi kwa kuwapa raia miliki ya ardhi kwa miaka 99 ili kuwawezesha kutumia ardhi hiyo kama dhamana waweze kukopa na kujenga majengo yenye uhai wa muda mrefu watakayoyatumia kama vitega uchumi vya kuwaingizia fedha na kuwapunguzia umasikini.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa gazeti la Sunday News toleo namba.32299 la  Oktoba 16 mwaka huu, lilichapisha taarifa kuwa tarehe  Oktoba 15, 2016 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliwaagiza wakazi wa Dar es Salaam waliopata barua ya toleo la ardhi (letter of offer) zilizotolewa na halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam mwaka 1980, warejeshe hati hizo katika kipindi kisichozidi miezi mitatu.

Iliongeza kuwa Waziri Lukuvi katika maagizo yake alisema hati hizo zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya watu wasio waadilifu kuwaibia masikini, lakini haikufafanua namna hati hizo zinavyotumiwa kuwaibia masikini wala kueleza mstakabali wa wamiliki hao baada ya kuzirejesha nini kitatokea.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa masharti yaliowekwa na Sheria ya Ardhi namba 4 kifungu cha 32 ya mwaka 1999, kinaeleza kuwa wamiliki halali wa ardhi wana haki ya kuongezewa muda wa kumiliki ardhi yao baada ya muda waliopewa awali kumalizika.

UDP iliongeza kuwa waziri pia hakufafanua kama wananchi hao wananyang’anywa ardhi hiyo au wanarejesha hati ili wabadilishiwe, ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa masharti ikiwamo kuongezewa muda wa umiliki.

UDP kupitia taarifa hiyo, ilitoa wito kwa Waziri wa Ardhi na Serikali kwa ujumla kuwajulisha Watanzania mustakabali wa wamiliki hao wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini kutokana na wananchi wengi kutofahamu sheria, hivyo si rahisi wao kujua kuwa wafuate taratibu zipi pale uhai wa hati zao unapoisha.

“Kuchelewa kwao kuomba kuongezewa muda wa umiliki usichukuliwe kuwa hawahitaji tena ardhi hiyo, badala yake Serikali ichukue hatua ya kuwaelimisha na kuwaongezea muda wa kumiliki ardhi yao,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Na ikiwa mipango miji mipya itakuwa imeathiri matumizi ya awali yalioidhinishwa, ni vizuri kwanza wapewe ardhi mbadala na kupewa fursa ya kuwa wabia katika uendelezaji mpya wa eneo lao badala ya kuwanyang’anya.

UDP walimwomba Rais DK. John Magufuli aingilie kati suala hilo kuzuia madhara yanayoweza kutokea endapo Serikali itawanyang’anya wananchi ardhi yao.

“Tunapenda kufafanua kuwa miundombinu iliojengwa kwenye ardhi hiyo iwe nyumba za kuishi au biashara zinazodumu zaidi ya miaka 33, hivyo kuwanyang’anya wanyonge hao ardhi yao ni kuwaonea na watafilisika na kuwafanya fukara kwani hawana chanzo kingine cha mapato yatakayowawezesha kununua ardhi na kujenga  nyumba nyingine,” ilifafanua taarifa hiyo.

Ushauri huu wa UDP si mbaya na kwa kuzingatia kuwa ardhi hutolewa kwa kuzingatia aina ya shughuli inayotarajiwa kufanyika katika eneo husika, ni vema wizara ikaweka utaratibu maalumu kwa wananchi kuomba kuongezewa muda wa umiliki pale wanapotaka kuanzisha miradi inayodumu kwa muda mrefu hata kama uhai wa hati husika haujafikia ukomo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles