23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria Manunuzi na usimamizi mbaya mikataba

mitamboNa Mwandishi Wetu

Sheria ya Manunuzi ya Umma imelalamikiwa na watu wengi na taasisi  nyingi kwa kufuata taratibu zaidi kuliko kuzingatia ukweli wa mambo na hali halisi ya soko.

Wadau wanadai vitu vingi vinavyotakiwa na sheria hiyo ni vya kitaasisi zaidi na si kufanikisha tendo lenyewe la kununua bidhaa au kupata huduma na hivyo hupoteza muda na kuvuruga mwenendo wa kazi husika. Serikali imepata hasara kubwa kwa kufuata masharti ya sheria hiyo na hivyo wadau wanaomba ifutwe au kufanyiwa mabadiliko ya kina.

Sheria ya Manunuzi inafuata mfumo wa bajeti taslimu (cash budget) wakati uzoefu unaonyesha wazi Serikali au mnunuzi aghalabu huwa na pesa na hivyo kutumia urasimu wa kukosa pesa kuvuta malipo ya mzabuni, lakini hasara hizo hurundikwa kwake.

Ni uonevu mtupu kufanya kazi na Serikali kwa sababu maofisa wake wako pale kutekeleza mifumo iliyoundwa na si kufanya kazi inayokusudiwa na hivyo kuleta manung’uniko kwa kila upande.

Sheria ya Manunuzi imejaa umangimeza, urasimu, mrundiko wa taratibu usiozingatia hali halisi , kukosekana utaalamu na kukosekana modeli ya mfano ya kufanyia kazi na hayo yanabanaishwa na mkanganyiko kama unavyojitokeza na kuelezwa na Mamlaka ya Manunuzi (PPRA) kwa usimamizi wa  manunuzi.

PPRA inajitetea kuwa asilimia zaidi ya 70 ya bajeti ya Serikali hutumika katika manunuzi ya bidhaa na huduma na hivyo sekta hiyo ni nyeti kwa ustawi wa Serikali na nchi yenyewe na hivyo lazima idhibitiwe vilivyo.

PPRA  inadai  kuwa utekelezaji wa mkataba wa manunuzi ya umma ni sehemu ya mchakato wa manunuzi na humlazimu mzabuni na taasisi nunuzi  (PE) kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba huo. Inasema utekelezaji huu huhitaji usimamizi thabiti ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa, hususani kupata thamani bora ya fedha zilizotumika katika manunuzi, lakini idara  za manunuzi mara nyingi hazina wafanyakazi wengi na wenye ujuzi unaotakikana, kwani ni rahisi kunena na si kutenda. Mengi ya makosa  ni ya kutokujua zaidi na si dhamira.

Hata hivyo, kutokana na ukaguzi unaofanywa na PPRA kila mwaka, upungufu mkubwa umebainika katika kipengele cha usimamizi wa mikataba ya manunuzi ya umma kwa wazabuni, hapo ndipo kwenye kero na  usumbufu wa kila hali.

PPRA inadai kipengele hiki hutumika kuangalia kama mkataba wa manunuzi ya umma ulisimamiwa ipasavyo na kama meneja mradi alikuwa na sifa stahiki, kama gharama za utekelezaji zilidhibitiwa na pia kama mradi husika ulikuwa na ubora uliokusudiwa.

Kwa mujibu wa Kanuni 114 ya kanuni za manunuzi ya umma, Tangazo la Serikali Na. GN. 446 la mwaka 2013, taasisi nunuzi (PE) zinatakiwa kusimamia mikataba ya manunuzi na kuhakikisha kwamba, gharama za mradi zinadhibitiwa, vifaa na kazi zinafanyika na kukamilika kwa wakati na marekebisho yanafanywa pale panapohitajika.

Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi, maeneo ambayo yameonekana kuwa na upungufu ni kama ifuatavyo na yanahitaji kuzingatiwa wakati wa utekelezaji kwa pande zote mbili za mkataba.

Mosi; ni kutoteua wasimamizi wa miradi; baadhi ya miradi ilionekana kutekelezwa bila kuwapo na msimamizi aliyeteuliwa na mtendaji mkuu. Pia taasisi za umma kutoandaa taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Pili; Ukiukwaji wa taratibu za mabadiliko ya mkataba; baadhi ya taasisi za umma zilibainika kuwa zilifanya mabadiliko ya wigo wa mkataba bila kufuata taratibu; mfano baadhi ya kazi za nyongeza kufanyika bila idhini.

Tatu; ilibainika kuwa nyongeza ya muda wa mkataba imekuwa ikifanyika bila kuzingatia taratibu. Udhaifu huu umekuwa ukijitokeza mara kwa mara katika halmashauri za wilaya.

Nne; kutokuchukua hatua dhidi ya wazabuni wasiotekeleza masharti ya mikataba; jambo hili huisababishia Serikali hasara.

Tano; kuchelewesha malipo ya wakandarasi; hali hii husababisha kuongezeka kwa gharama za mikataba kutokana na riba na hivyo kuisababishia taasisi gharama.

Sita; kutopeleka mikataba kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikiwa; baadhi ya taasisi ziliingia mikataba yenye thamani zaidi ya Sh milioni 50 bila kupitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama sheria inavyoelekeza, kiwango hicho kilikuwa kabla ya maboresho ya Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2016, ambapo mara baada ya maboresho, ukubwa wa thamani (‘threshold’) iliongezeka hadi bilioni moja.

Saba; katika miradi ya ujenzi, ukaguzi pia ulipima kiwango cha usimamizi na utimilifu wa masharti ya mikataba, ambapo matokeo yalibaini kuwa baadhi ya miradi ilikuwa na upungufu, mfano wakandarasi na watoa huduma za ushauri wa kitaalamu hawakuweka bima dhidi ya miradi husika, kinyume na matakwa ya mikataba.

Nane; Upungufu mwingine hujitokeza katika bondi (amana) na bima za miradi ambazo ziliainishwa kwenye mikataba ambapo pia bima hizo hazikuwasilishwa kwenye taasisi husika.

Tisa; kuchelewa kuanza kwa kazi baada ya kukabidhiwa eneo la mradi; baadhi ya taasisi nunuzi zimekuwa zikichelewa kukabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi kwa wakati, hili huchangia katika kurefusha muda wa kazi na kuisababishia taasisi gharama zisizo na ulazima.

Kumi; kutoandaliwa kwa mpango wa uhakiki wa ubora wa miradi; taasisi zimekuwa zikishindwa kuandaa mpango wa uhakiki wa mradi mara baada ya mradi kukamilika. Jambo hili huifanya taasisi kushindwa kutambua endapo fedha iliyotumika inaendana na thamani ya mradi uliokamilika na hivyo kujikuta ikipokea mradi uliotekelezwa chini ya kiwango.

Kumi na moja; ukosefu wa ushahidi wa kufanyika kwa mikutano eneo la mradi; baadhi ya taasisi zimekuwa hazifanyi mikutano kwenye eneo la mradi, hivyo wakati wa ukaguzi zilishindwa kuwasilisha ushahidi huo.

Kumi na mbili; kutokuwepo au kutozingatia ratiba ya kazi ya mkandarasi; baadhi ya miradi imekuwa ikichelewa kutekelezeka kutokana na mkandarasi kutotoa ratiba ya kazi kwa taasisi nunuzi na kujadili jinsi ya utekelezaji wa mradi husika. Pia suala la kutozingatia ratiba husababisha ucheleweshaji wa mradi na huchangia kuongeza gharama.

Kumi na tatu; malipo yenye utata kwani baadhi ya taasisi, kwa kushirikiana na wakandarasi wasio waaminifu, wamekuwa wakifanya malipo yenye utata, ambapo wakandarasi hulipwa kwa kazi ambazo hazikufanyika au ambazo hazijakamilika.

Kumi na nne; ukamilishaji na ufungaji wa miradi; tathmini mara nyingi hufanywa kwenye miradi iliyokamilika ili kubaini ubora na utimilifu wa majengo ambapo baadhi ya miradi michoro, orodha ya maeneo yaliyokuwa na utata, utoaji wa hati ya utimilifu wa miradi, hati ya mwisho, kipindi cha matazamio, uandaaji wa taarifa ya mwisho ya kufunga mradi pamoja na malipo ya mwisho.

Aidha, PPRA katika ripoti yake ya manunuzi ya umma kwa mwaka wa fedha 2015/16, ilibaini malipo yenye utata ya Sh bilioni 1.32, yaliyofanywa na taasisi nne, ambapo wakandarasi walilipwa kwa kazi ambazo hazikufanyika, jambo ambalo huisababishia gharama taasisi na Serikali kwa ujumla.

PPRA inatoa  rai kwa umma, wazabuni na taasisi kuwa endapo taasisi za umma zitazingatia sheria na kanuni katika kusimamia miradi, zitaisaidia Serikali kupata thamani ya fedha inayoendana na miradi husika na kuwezesha kufanya ukaguzi wa kina (forensic audit), shughuli ambayo itaweka maofisa wengi matatizoni kwa kutozingatia mwenendo, kanuni na taratibu za manunuzi ya umma.

Kwa nia ya kuboresha utendaji, baadhi ya wadau wanaiomba Serikali iwe na modeli ya utendaji na orodha ya matendo (Checklist) kwa kila aina ya mradi ili iwe inatoa mwongozo kwa watendaji wake, badala ya kuviziana kama ilivyo sasa. Vilevile Serikali inaaswa kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi unaolingana na umuhimu wa zoezi zima la manunuzi na mahitaji yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles